Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, atakuwa mwenyekiti mwenza katika mkutano wa nishati safi ya kupikia kwa Afrika utakaofanyika nchini Ufaransa.
Anatarajiwa kuondoka nchini kesho Mei 12, 2024 kuhudhuria mkutano huo utakaofanyika Paris, Ufaransa.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Rais Samia anashiriki mkutano huo kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuifanya nishati safi ya kupikia kuwa kipaumbele cha kimataifa.
Mkutano huo utafanyika Mei 14, 2024 na amealikwa na Dk Fatih Birol, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati (IEA). Wawili hao hao watakuwa wenyeviti wenza katika mkutano huo.
Pamoja nao, wengine watakaoshiriki ni Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Støre, na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinwumi Adesina.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema mwaliko kwa Rais Samia unatokana na mchango wake katika kutambua umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuweka msukumu katika kutokomeza matumizi ya nishati chafu ya kupikia na athari zake.
“Zaidi ni kulinda mazingira ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema January.
Mkutano huo unalenga kulifanya suala la matumizi ya nishati safi ya kupikia kuwa la kipaumbele katika ajenda ya kimataifa.
Pia kuainisha mabadiliko madhubuti ya kisera yatakayoharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, na kutoa fursa ya washiriki kutoa ahadi za kifedha, sera na ubia ili kufikia azma ya kukuza matumizi ya nishati safi.
Mwishoni mwa mwaka 2023, katika Mkutano wa 28 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28), Rais Samia alizindua Programu ya Nishati Safi ya Kupikia ya Kusaidia Wanawake Barani Afrika (AWCCSP) ambayo ilipokewa vyema kimataifa na sasa utekelezaji wake unaendelea.
Mkutano huo unatarajiwa kujumuisha watu zaidi ya 900 wakiwemo wakuu wa nchi, taasisi na kampuni za kimataifa zinazohusika na nishati safi ya kupikia.
Kati ya washiriki, imeelezwa ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus na Mo lbrahim, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mo Ibrahim.
Mbali ya mkutano huo, Rais Samia atafanya mazungumzo na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron katika Ikulu ya Elysee, Paris.