RC Malima atamani watalii zaidi Morogoro

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amewataka waandishi wa habari kufanya utafiti wa kina wenye lengo la kuibua vivutio vipya ya utalii, ikiwa ni njia ya kutanua wigo ya kuhamasisha watalii zaidi kutembelea vivutio vya utalii.

Akizungumza na Mwananchi baada ya ufunguzi wa mafunzo ya nafasi ya mwandisi wa habari sekta ya utalii, leo Mei 11.2024 mjini hapa, Malima amesema Tanzania ina vivutio vingi ambavyo havijatangazwa na vingine kutojulikana wakiwemo samaki aina ya Tigerfish wanaopatikana katika Mto Kilombero pekee.

Malima amesema sekta ya utalii ni pana na waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuibua zaidi vivutio vipya, akitaja ufugaji wa nyuki kuwa ni eneo lingine la utalii linalopaswa kuhamasishwa ili watu wafahamu uzalishaji asali na maisha ya nyuki.

“Ili kufikia idadi ya watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025 ni wajibu wetu kuibua vivutio vipya ili kuongeza idadi ya watalii.” amesema Malima.

Malima amesema wakati hatua zikifanyika kuibua vivutio vipya, wanahabari waendelee kuhamasisha wawekezaji kujenga hoteli zinazokidhi mahitaji tofauti ya watalii.

“Kama nusu ya simba duniani, wapo katika hifadhi za taifa za Tanzania ikiwemo hifadhi ya Mikumi ambayo baada ya kuanza safari za treni ya kisasa, usafiri wa kuiofikia utakuwa rahisi kutokea Kilosa,” amesema.

Kwa upande wake Mkufunzi Mwandamizi Chuo cha Taifa cha Utalii, Agapiti Lasway amesema idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii milioni 1.5 mwaka 2022 hadi kufikia watalii milioni 1.8 mwaka 2023.

Rais wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (Tampa), Simon Mkina amesema utafiti uliofanywa na chama hicho unaonyesha kuwa mkoa wa Morogoro una vivutio vingi, wakiwemo vinyonga wenye pembe moja na wenye mbili pamoja na vipepeo vyenye rangi za Bendera ya Taifa la Tanzania.

Related Posts