Red Cross yaadhimisha miaka 62 ikizikumbuka ajali za Mv Bukoba, treni Dodoma

Dodoma. Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross Society) kikiadhimisha miaka 62 tangu kilipoanzishwa, kimekumbuka ushiriki wake katika kuhudumia waathirika wa ajali za MV Bukoba na treni Dodoma.

 Red Cross iliyoanzishwa nchini mwaka 1963 ilishiriki kutoa huduma kwa waathirika wa ajali ya MV Bukoba mwaka 1996 na ya treni ya mwaka 2002.

Zaidi ya wanachama milioni moja wa chama hicho wameendelea kujitolea kutoa huduma za kibinadamu nchini.

Hayo yamebainishwa na Rais wa chama hicho Tanzania, David Kihenzile leo Jumamosi, Mei 11, 2024 wakati wa maadhimisho yaliyofanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.

Kihenzile amesema shirika limekuwa likitoa huduma ya kwanza, kuhudumia wakimbizi, kushiriki kampeni za chanjo ikiwemo ya Uviko-19, kushiriki shughuli za uokoaji, na kutoa mafunzo.

Amesema mbali na matukio hayo, wameshiriki kutoa huduma baada ya kuzama boti ya MV Spice Islander, tetemeko la ardhi, kivuko cha Mv Nyerere kilipozama na sasa kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko.

Wakati Kihenzile akisema hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi amesema analikumbuka shirika hilo wakati wa ajali ya Mv Bukoba, wakati huo akiwa mwendesha mashtaka kwenye kesi ya meli hiyo.

Amesema watumishi wa shirika hilo walienda kwenye kina cha maji ilikozama meli kufanya uokozi.

“Nilipokuwa naendesha kesi ya Mv Bukoba tuliona umuhimu wa Red Cross walivyojitosa kwenda kwenye kina cha maji, meli ilipozama kufanya uokozi,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mlezi wa chama hicho nchini, ametoa hati maalumu kukipongeza kwa namna kilivyojitoa kutoa huduma kwa waathirika wa maporomoko ya tope wilayani Hanang.

Kihenzile anasema licha ya shirika kutoa huduma kwa zaidi ya miaka 62, bado Tanzania haijalitambua Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC) jambo analoeleza linaikosesha fursa ambazo lingepata.

Kihenzile ameiomba Serikali kumalizia mchakato wa kuitambua jumuiya hiyo ili kufikia hatima ya kuridhia.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Biteko aliyemwakilisha Rais Samia katika maadhimisho hayo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Red Cross.

“Red Cross ni mfano wa kuigwa kwa kuthamini utu na uhai wa binadamu, kaulimbiu yenu ambayo mmekuwa mkiisema hapa, ‘natoa kwa furaha na furaha yangu ni zawadi kwako’ kama baba angeiambia familia yake basi tungekuwa na familia zenye furaha na kama kila mmoja angemfanya mwenzake kuwa na furaha basi tungekuwa na jamii yenye furaha,” amesema.

Ilianzishwa na mfanyabiashara wa Uswisi, Henry Dunant baada ya mapigano ya Solferino wakati wa vita ya Austria dhidi ya Italia na Ufaransa mwaka 1859.

Siku hiyo inaelezwa wanajeshi 6,000 walikufa na 25,000 walijeruhiwa jambo lililomshangaza Dunant, akisikitika juu ya mateso ya wanajeshi walioachwa mara nyingi mahali pa mapigano.

Aliacha biashara kwa siku kadhaa akawasaidia majeruhi wa vita hivyo.

Baadaye alianzisha kampeni na kuunda shirika litakalotunza majeruhi wakati wa vita.

Mwaka 1860 na 1863 aliunda Kamati ya Kimataifa ya shirika za kutunza majeruhi na kufanya mkutano wa kwanza wa kimataifa ambao watu binafsi na wawakilishi wa Serikali walihudhuria.

Kamati hiyo imekuwa chanzo cha Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ya Geneva ya leo hii.

Related Posts