Sikia alichosema beki mpya Yanga, awataja Bacca, Azizi KI

WAKATI Yanga ikiwa katika hatua za mwisho za kukamilisha mazungumzo kwa ajili ya kumsajili beki wa FC Lupopo, Chadrack Boka anayetakiwa kuja kuziba nafasi ya Lomalisa Mutambala, mwenyewe amefunguka kwamba: “Najua mashabiki wanachotaka, waambie wasubiri nakuja kuwafurahisha kwa kuipa timu kazi nzuri.”

Boka ambaye ni mrefu kwa umbo, amefichua kwamba anasubiri uhamisho huo ukamilike haraka huku akisisitiza kwamba, “wachezaji wanaocheza kule mbele watafunga sana, nitapiga krosi lakini pia nitasaidia vizuri kujilinda, wataona kazi nzuri.”

Yanga hesabu zake zipo kwa Boka ikimtaka kuziba nafasi ya Lomalisa ambaye haitamuongezea mkataba mwisho wa msimu huu huku ikitaka mtu mwingine bora zaidi wa ulinzi upande wa kushoto.

Lomalisa ambaye mkataba wake uko mbioni kumalizika amekitumikia kikosi hicho kwa misimu miwili, lakini katika kipindi cha hivi karibuni amekuwa na majeraha ya mara kwa mara yanayomfanya kushindwa kucheza mechi muhimu kama ile ya Al Ahly (Ligi ya Mabingwa Afrika) na ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba, jambo lililowapa ugumu mabosi wake kumuongeza mkataba.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka jijini Lubumbashi, Boka amesema kama kuna kitu anakisubiri kwa hamu ni kukamilika kwa dili lake ili atue Yanga kwani anaamini itakuwa ni njia muhimu kuelekea mafanikio anayoyataka katika soka.

Mkongomani huyo alieleza kuwa Yanga ni timu nzuri inayoundwa na mastaa wenye ubora ambao alivutiwa nao alipowaona kwa mara ya mwisho ilipokutana na TP Mazembe Lubumbashi, huku akiwataja mabeki Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na kiungo mshambuliaji Stephanie Aziz KI walivyo noma.

“Yanga ni timu kubwa hakuna mchezaji anayetaka mafanikio atakataa kuitumikia kutokana na mafanikio yao na mashabiki wao ambao wanaipenda sana timu yao, niliiona ilivyokuja kucheza na Mazembe hapa Lubumbashi,”alisema Boka.

“Kikosi chao nacho kina wachezaji bora sana wakati ule walikuwa na Fiston (Mayele) lakini naona ameondoka na kuna yule anavaa jezi namba kumi (Aziz KI) anajua sana mpira kule kwa mabeki yule anayevaa jezi namba mbili (Bacca) naye ni beki mzuri sana, kiujumla wana timu nzuri  lakini nisimsahau yule ndugu yangu Maxi (Nzengeli) nae yuko vizuri mno.

“Nakumbuka wakati wanakuja hapa mashabiki wao ni watu wanapenda sana mpira na hata nikiangalia mechi zao naona jinsi mashabiki wana furaha na kuishangilia kwa wingi timu yao, kwenye mechi zake  hii inanifanya kusubiri kwa hamu sana kujiunga na timu hii kubwa.

Alisema anafahamu anakwenda kujiunga na klabu kubwa Afrika ambapo mashabiki na viongozi wanasubiri kuona krosi nyingi na uchezaji mzuri hasa kwenye eneo la kulinda. “Viongozi wa Yanga wameonyesha mambo makubwa kwa kuamua kuja hapa Lubumbashi na kuniona na baadaye tukazungumza na wakaongea pia na viongozi wangu, Hii ni namna bora ya kufanya mambo kwa usahihi.”

MPOLE, NINJA WAMZUNGUMZIA

Akimzungumza na Mwanaspoti, beki wa Lubumbashi Sport ya DR Congo, Mtanzania Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amewaambia Yanga kwamba Boka wanayemuwania kutoka FC Lupopo ni mchezaji mzuri. “Jamaa muda wote anapambana unamuona kwenye maeneo mengi uwanjani, vitu vya kipekee kwake nilivyoviona ana uamuzi wa haraka, mfano akipandisha kusaidia mashambulizi hajisahau kurudi kwa haraka kukaba,” alisema Ninja

“Endapo atafanikiwa kusaini Yanga itakuwa imepata beki atayewasaidia kuongeza nguvu safu ya mabeki, ukiachana na ubora wake wa kupiga klosi anajitolea kwa timu maana wakati tumecheza nao muda wote alikuwa anapambana na ana uwezo wa kuwasababishia wapinzani wafanye makosa ambayo yanawapa faulo.”

Naye mshambuliaji wa FC Lupopo, George Mpole anayecheza na Boka alisema kitu kikubwa alichokiona kwake ni nidhamu ya kazi kuanzia kwenye mazoezi hadi wakati wa mechi. “Nikimzungumzia uwanjani kama kweli Yanga itamsajili itakuwa imepata beki ambaye ana uwezo wa kupiga krosi, kukaba na kushambulia. Jamaa ana nguvu na kasi. Nimeona hilo tukiwa tunafanya mazoezi, kwani haogopi kujaribu kufanya majukumu mbalimbali uwanjani. Ukabaji wake anakukaba kama vile mnacheza na wapinzani na ndio kitu anachokuwa anakwenda kukifanya wakati wa mechi,” alisema Mpole mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22.

Related Posts