Dodoma. Serikali imesema iko kwenye mchakato wa kutumia majeketi yenye kamera watakayovaa askari wa usalama barabarani ‘trafiki’ kama sehemu ya kifaa cha kazi kwa lengo la kudhibiti rushwa barabarani.
Hayo yamesema leo Jumamosi Mei 5, 2024 na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango wakati akifungua Kituo cha Polisi Daraja A Wilaya ya Kipolisi Mtumba jijini Dodoma.
“Nitalitaka Jeshi la Polisi kuangalia upya mfumo mzima wa utoaji wa leseni za kuendesha vyombo vya moto, lakini pia ukaguzi wa magari.
“Matumizi ya teknolojia ikiwemo kamera za barabarani na matumizi ya wanachoita kama ‘body cam jackets’ (majaketi yaliyowekwa kamera za kurekodi sauti na video) katika kudhibiti rushwa barabarani na pia kuimarisha weledi na uthabiti wa vyombo vya moto.
“Nimekwisha kunong’ona na Waziri wa Mambo ya Ndani (Hamad Masauni) na bahati nzuri amenijulisha kwamba tayari wameanza mchakato wa kuhakikisha kwamba sasa tunafunga kamera za barabarani.
“Lakini pia mavazi ya hizo jaketi ambazo zinakuwa na kamera kwa askari polisi wa barabarani ambao wanapoongea na madereva barabarani, kile wanachozungumza chote kinaonekana, kwa hiyo nafasi ya rushwa inakuwa imepungua sana, kwa hiyo hili ni jambo muhimu mheshimiwa Waziri mjitahidi sana kuliharakisha,” amesema Dk Mpango.
Amesema ajali za barabarani ambazo zinaweza kuepukika, bado zinaangamiza Watanzania na sehemu kubwa ya ajali hizo ni zile ambazo zinasababishwa na ubovu wa magari, kutozingatia sheria za usalama barabarani na madereva kukoza weledi.
“Mfano mzuri ni ile ajali mbaya ya basi la shule iliyotokea kule Arusha tarehe 12/4/2024 na kusababisha tukaondokewa na watoto wetu saba,” amesema.
Amesema Jeshi la Polisi bado linao wajibu mkubwa wa kusimamia sheria za usalama barabarani na kuweka kipaumbele katika utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu matumizi salama ya barabara.
Pia, Rais Samia Suluhu Hassan aliwahi kuzungumzia mkakati wa Serikali wa kuondoa rushwa zinazosababishwa na trafiki kwa kuwaondoa barabarani.
“Tunataka kuondoa trafiki ili kuondoa rushwa, tuweke kamera.”
Pia, Agosti 25, 2021 Rais Samia, alirudia kuliagiza Jeshi la Polisi kukomesha tabia za baadhi ya askari wake hususan wa trafiki kupokea rushwa kwenye magari.
Rais Samia alitoa agizo hilo wakati akifungua Kikao Kazi cha Maofisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, akisisiza kuwa vitendo vya baadhi ya maofisa wa jeshi hilo kuomba na kupokea rushwa ni vya aibu.
Aliweka wazi kwamba zipo video fupi ambazo zimekuwa zikizunguka ndani na nje ya nchi kupitia mitandao ya kijamii zikionyesha baadhi ya maaskari wa Jeshi la Polisi hususan matrafiki wakiomba na kupokea rushwa kwenye magari.
Katika kuhakikisha anadhibiti rushwa katika utoaji wa leseni za udereva Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Mkuu wa Jeshi la Pilisi (IGP) Camillus Wambura, alitangaza kukifuta kikosi chote cha wakaguzi wa leseni za magari na watahini wa leseni na kuunda tume ya uchunguzi ili kuchunguza namna kikosi hicho kilivyokuwa kinatoa leseni, kutokana na ongezeko la ajali za barabarani.
Pia, Februari 21, 2023 IGP Wambura alitoa kauli kwamba Jeshi la Polisi limefanya uchunguzi na kuona upo umuhimu wa kurekebisha mfumo wa utoaji wa leseni za udereva ili kudhibiti ajali za barabarani.
Wambura alisema hayo baada ya kufanya kikao na wakuu wa polisi wa usalama barabarani wa mikoa yote Tanzania, wakaguzi wa magari na watahini wa madereva, akilenga kuwakumbusha wajibu na namna bora ya kuondokana na ajali za barabarani.
Majaketi yenye kamera ‘body cam jackets’ au ‘body worn camera (BWC), yenye kifaa cha kurekodi sauti na video yamekuwa yakitumiwa na polisi katika mataifa mbambali duniani kama sehemu ya vifaa vyao vya kufanya kazi.
Umuhimu wa majekti hayo ni kusaidia usalama wa wakaguzi kwa kuhimiza mwingiliano salama na wa kuheshimiana na kupunguza mizozo na kuwezesha malalamiko kuchunguzwa na kutatuliwa kwa urahisi.
Picha zilizonaswa husaidia wakaguzi kwa maswali na uchunguzi unaohusisha matukio ya mahali pa kazi kufanya kazi vizuri.