Muleba. Wakati mvua katika maeneo mbalimbali nchini zikisababisha mafuriko, baadhi ya maeneo yameshuhudia maporomoko ya tope linalotembea kama maji, jambo ambalo limewastaabisha watu ambao hawakuwahi kushuhudia jambo hilo.
Hicho ndiyo kinachotokea katika Kitongoji cha Kabumbilo kilichopo katika Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, ambapo tope linalotembea kuelekea mwambao wa Ziwa Victoria, limeibua gumzo mitandaoni huku watu wakishangaa hali hiyo imewezekanaje.
Hiyo si mara ya kwanza kutokea kwa maporomoko ya tope nchini, hali kama hiyo ilitokea wilayani Hanang mkoani Manyara Desemba 3, 2023 na kusababisha vifo vya watu 89 na wengine 116 kujeruhiwa huku miundombinu ikiharibika na mamia kukosa makazi.
Pia, maporomoko kama hayo yalishuhudiwa huko Mbeya katika Mlima Kawetele ambapo mvua iliyonyesha Aprili 14, 2024 ilisababisha nyumba 20, ng’ombe na mifugo mingine kufukiwa na tope kutoka Mlima Kawetele.
Hali hiyo imeshuhudiwa tena huko Muleba, ambako Mwananchi limepiga kambi na kushuhudia tope hilo na kuzungumza na wenyeji wa eneo hilo, ambao wamesema makazi yao yameathiriwa na tope hilo linaloshuka kutoka Mlima Kabumbilo kwenda Ziwa Victoria.
Hadi sasa, watu 220 hawana sehemu maalumu za kulala wala chakula baada ya ekari 36 za mashamba na nyumba 16 kufunikwa na mapromoko ya tope katika Mlima Kabumbilo katika Kijiji cha Ilemela, pembeni mwa Ziwa Victoria.
Mkazi wa kitongoji cha Kabumbilo, Moreen Kareni amesema tope lilianza kushuka Jumapili Aprili 15, 2024 saa nane mchana na kufunika nyumba za watu na mashamba, baadhi wamehama makazi yao huku yeye pamoja na wengine wakipata hifadhi kwa majirani.
Amesema siku hiyo walianza kuona miti ikitoka mlimani ikiambatana na udongo wa tope vikiteremka kufuata mwalo wa dagaa wa Kabumbilo na baada ya siku mbili walishuhudia nyumba zaidi ya 24 ikiwemo kambi wa wavuvi, maduka ya eneo la mwalo zikafunikwa pamoja na mashamba.
“Hatuna chakula pia hatuna makazi, hatuna pa kwenda, tupo tu tunahangaika. Tunalala nje, tunahitaji msaada, tunaomba Watanzania watusaidie mahali pa kukaa na vyakula kwa maana vyote vimefukiwa,” amesema.
Moreen ameongeza, “hapa paliku ndio center (sehemu panapouzwa vitu mbalimbali), nyumba kama 24 zimeshafukiwa na miti inatoka juu (Mlima Kabumbulo), inateremka na mawe. Watu wamehama, wengine hatujapata makazi, tupo tu kwa majirani tumetulia.”
Mkazi mwingine wa Kabumbilo, Jonathan Festo (75) aliyeishi katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 50, amesema ana hofu kuendelea kuwepo katika mazingira hayo, japo hana sehemu nyingine ya kujihifadhi, hivyo anaiomba Serikali kufanya uchunguzi kubaini chanzo cha maporomoko hayo ya tope.
Ameiomba Serikali iwasaidie kwani anaamini maporomoko hayo yamesababishwa na miujiza ya mlima huo.
Alidai kuwa zamani mwenyeji wake aliyemtambulisha kwa jina la Pankrasi, aliyekuwa akiishi mlimani, karibu na mti wa parachichi, chini yake kulikuwa na chemchemi ya maji yasiyokauka.
Amesema mti huo ulikatwa na Mzee Pankrasi lakini ulibaki umesimama, akaamua kuhama kwenda kuishi kijiji kingine, hivyo anaamini huenda ndiyo chanzo cha maporomoko ya tope hilo.
“Naomba Serikali ichunguze huku chini ya mlima kuna nini, zamani kulikuwa na chemchem chini ya mawe na pembeni, kulikuwa na mti wa parachichi na rafiki yangu Pankrasi akaukata lakini ukakataa kukatika, akaamua ahame. Huenda hii ni miujiza imeanza kujitokeza.
“Kwanini wasichunguze haraka, wananchi tunazidi kuteseka? Mimi ukisema nihame, naenda wapi na umri wangu huu. Sina nguvu kama zamani, tuna njaa, hatuna chakula, sehemu inazidi kudidimia,” amesema Festo.
Ameiomba Serikali kuwasaidia sehemu ya kuishi kwa sasa kwa maana baada ya kuwaambia watoke eneo hilo, waliomba msaada vitongoji jirani lakini kwa sasa wameanza kulala na kushinda njaa.
Mkazi wa Kijiji cha Ilemela, Verediana Stephen amesema maporomoko ya tope yamesababisha madhara makubwa kwenye jamii yao, akidai hali imebadilika akitolea mfano shamba lake ekari moja ambalo limefunikwa na chakula kimekuwa shida huku akiwa na familia ya watoto saba.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kabumbilo, Marchades Chrisant amesema wananchi hao wapo katika wakati mgumu kwa kuwa hakuna huduma muhimu za kijamii.
Alisema kila siku watalaamu wanaenda na kuondoka bila kuwapatia majibu kamili kuhusu chanzo cha tope hilo.
Amesema imefika hatua wananchi wameanza kuingia kwenye hatari ya kurudi kwenye maeneo yaliyoathiriwa.
“Wananchi walikuwa wanategemea mwalo wa Kabumbilo kama sehemu ya kupatia riziki, lakini kwa sasa eneo hilo limefunikwa na tope, mawe na miti, hawana msaada wowote wa chakula na mahitaji mengine, naingiwa hofu ya kuwapoteza wananchi wangu kama tatizo hilo litakuwa halijapatiwa ufumbuzi,” amesema.
Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu kinachoendelea Kabumbilo, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Abel Nyamahanga amesema tayari wataalamu wamekwenda kuchunguza eneo hilo ili kubaini chanzo cha udongo huo kuporomoka, hata hivyo amesema kwa macho ya kawaida tope linaonekana kutoka chini ya ardhi.
“Hatujapewa majibu kwamba ni nini kinasababisha, bado tunasubiri majibu kwa sababu kilichojitokeza katika sehemu ya mlima iliyokuwa imepandwa mazao, ghafla ilitumbukia chini, tafsiri ya haraka haraka isiyo ya kitaalamu ikaonekana tope linatoka chini.
“Lilipokuwa linatoka maana yake sehemu ile ikabaki ombwe(nafasi tupu), ikafanya hili la juu lidumbukie chini, hayo ni mawazo yasiyo ya kitaalamu…sasa kama lile tope lilianza kutoka pale chini, ndiyo hayo majibu sasa ambayo tunategemea wataalamu watwambie tatizo ni nini,” amesema.
Kuhusu mkakati wa Serikali kuwasaidia wananchi walioathirika, Dk Nyamahanga amesema waliwaondoa wananchi wa mwanzoni waliokuwa hatarini zaidi na kuwapatia mabati kwa ajili ya kuanzia maisha maeneo mengine.
“Ambacho tulikifanya, tuliwaondoa wananchi wale wa kwanza waliokuwa kwenye hatari, wapo kwenye mkondo wa tope linapotiririkia, tuliwaondoa na nyumba pale zilikuwepo nyingi tu zimefunikwa.
“Tukawawezesha na mabati kama Serikali kwa ajili ya kuanzia maisha maeneo mengine, kwa sababu wengi walikuja maeneo hayo kwa ajili ya uzalishaji lakini wana viwanja maeneo mengine. Kwa hiyo, ndipo huko wengine wamerudi kuweka makazi. Kama mwananchi yupo pale, tafsiri yake yupo pembezoni, hajapatwa na hilo janga,” amesema.
Mtaalamu wa jiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa yuko kwenye kamati ya wataalamu waliotumwa na Serikali kuchunguza chanzo cha maporomoko ya tope ya Hanang, alisema kipindi hiki cha mvua nyingi, udongo unashiba maji, hivyo unalegea na kuporomoka.
“Tungefika tukafanya uchunguzi, tungesema specific (mahsusi) kinachoendelea Muleba ni hiki, lakini tunashindwa kusema kabla hatujaenda. Lakini kimantiki, zinapoanza kunyesha mvua za mwanzo, hupati maporomoko kwa sababu ardhi inakuwa kavu.
“Lakini mvua zinapoendelea kunyesha na kunyesha, ardhi inashika maji, yanakuwa hayawezi tena kwenda chini, kwa hiyo yanamomonyoa ardhi iliyo kwenye mteremko, ndipo tope linaporomoka,” amesema mtaalamu huyo.
Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuchukua tahadhari inapotokea hali kama hiyo pamoja na kuzingatia tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa (TMA). Amesema kinachoelezwa ni hali halisi inayoweza kutokea kama tahadhari hazitachukuliwa.