Uvunjaji mikataba usiofuata sheria wamliza wakili mkuu

Dar es Salaam. Kwa mara nyingine Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Boniface Luhende ametaja mambo matano yanayoweza kuathiri utendaji wa taasisi yake, akirejea uvunjaji wa mikataba kwa taasisi za umma bila kuzingatia sheria unavyoitia hasara Serikali.

Uvunjaji huo wa mikataba licha ya kutozingatia sheria na kanuni, amesema unapofanyika ofisi yake haishirikishwi.

“Baadhi ya taasisi za umma zinavunja mikataba au makubaliano ziliyoingia na kampuni au taasisi mbalimbali binafsi bila kuihusisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, hivyo kusababisha wingi wa migogoro,” alisema.

Dk Luhende alieleza hayo jana Mei 10, 2024 alipoainisha changamoto za taasisi hiyo mbele wa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini aliyefika kwenye taasisi hiyo kwa lengo la kujionea utendaji kazi.

Hii ni mara ya pili kwa Luhende kutoa kauli hiyo, baada ya Septemba 13, 2023 kuzungumzia pia jambo hilo kuwa ni miongoni mwa changamoto kwenye ofisi yake.

Alisema hayo wakati wa hafla ya kumpokea Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana, alipoitembelea ofisi yake jijini Dar es Salaam.

Dk Luhende alimweleza waziri kuwa changamoto hiyo haiishii kuwa mgogoro, hufikia hatua ya kuisababishia Serikali hasara kwa kutozwa fidia.

Naibu Waziri Sagini akizungumzia changamoto hiyo juzi alisema, “Suala la taasisi kutozingatia sheria ripoti zenu zitusaidie kuzibaini, unaweza kukuta ni wizara fulani, halmashauri au mkoa fulani, tukijua hayo Serikali inaweza kushauriwa ipasavyo,” amesema Sagini.

Amesema hatua hiyo itawezesha kuona mashauri hayo ni yapi, yapo katika maeneo gani na udhaifu uliopo.

Sagini ameshauri Ofisi ya Wakili wa Serikali kufanya utafiti mdogo kubaini udhaifu ulipo na kuandaa ripoti itakayowasilishwa kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Amesema ni bora mikataba hiyo ikavunjwa kwa kupitiwa, kwani wanapokurupuka na kuvunja wanaiingiza Serikali kwenye gharama.

“Kwenye kikao cha mawaziri na makatibu wakuu tutapewa taarifa hizo na wakielewa wanaweza kuchukua hatua za kujirekebisha,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan Machi 2024 akiwaapisha viongozi wapya aliowateua aliwataka kuzingatia sheria wakati wa kuvunja mikataba na makandarasi kuepuka kuisbabishia hasara Serikali.

“Uvunjaji wa mikataba ufuate taratibu jamani, vinginevyo mnatutia hasara sana, (mkandarasi) akienda mahakamani. Wakati mwingine kweli inaudhi lakini mfuate utaratibu katika uvunjaji wa mikataba,” amesema Rais Samia.

Tatizo la uvunjaji mikataba bila kufuata taratibu mara kadhaa limeisababishia Serikali hasara pale inaposhtakiwa kwenye mahakama za kimataifa.

Kwa mfano, Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) Julai 14, 2023 kilitoa uamuzi wa kuitaka Serikali ya Tanzania kuilipa kampuni ya Indiana Resources Ltd ya nchini Australia takribani shilingi 250 bilioni baada ya kujiridhisha uwepo wa ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji katika Mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill mwaka 2018.

Mbali hiyo, mwaka 2016, Serikali ilivunja mkataba na kampuni ya Symbion Power Co. Ltd wa uzalishaji umeme na baada ya shauri hilo kupelekwa katika Mahakama ya Kimataifa, Serikali ilitakiwa kulipa zaidi ya Sh10 bilioni.

Dk Luhende alitaja changamoto zingine kuwa ni taasisi za umma kutozingatia sheria na miongozo wakati wa kuwachukulia hatua watumishi wa umma na kuchelewesha malipo ya makandarasi, hivyo kuchangia migogoro na ushirikiano hafifu baina ya taasisi yake na taasisi zingine za umma.

Changamoto nyingine ni taasisi zinazojishughulisha na masuala ya ardhi kuwa na mchango kwenye migogoro ya ardhi kwa watu wawili kuuziwa eneo moja.

Malalamiko yanayotolewa na Waziri Mkuu wa Serikali pia yamekuwa yanaelezwa mara nyingi kwenye Ripoti Kuu ya Ukaguzi wa Serikali za Mitaa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) 2022/23, ikionyesha ucheleweshwaji wa malipo kwa kazi zilizofanyika yenye thamani ya Sh2.22 bilioni.

“Nilipitia uzingatiwaji wa sheria na masharti yaliyobainishwa kwenye mikataba na kubaini kuwa, mamlaka saba za Serikali za mitaa zina madai ya wakandarasi kiasi cha Sh2.22 bilioni ambayo hayajalipwa kwa muda wa kati ya siku 55 hadi 270 tangu tarehe ya kuthibitishwa kwa madai hayo,” inaeleza ripoti ya CAG.

Ripoti imebainisha masharti ya jumla ya mkataba (GCC) yanawataka waajiri kuwalipa wakandarasi kiasi kilichoidhinishwa na wasimamizi wa miradi ndani ya siku 28 kuanzia tarehe ya kuwasilishwa cheti cha madai ya malipo ya mkandarasi.

Kutokana na hilo, CAG alipendekeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kuhakikisha fedha za miradi ya ujenzi zinatolewa kwa wakati.

“Hii itarahisisha utekelezaji mzuri wa miradi hiyo na kuepusha riba na adhabu zisizo za lazima,” alisema.

Katika hatua nyingine, Dk Luhende alisema kwa mwaka wa fedha Julai 2023 hadi Aprili 2024 ofisi yake imeendesha mashauri ya madai 7,813, kati ya hayo 7,798 yakitoka ndani ya nchi na 15 nje ya nchi.

Alisema mashauri 705 ambayo ofisi yake ilishinda yameisaidia Serikali kuokoa zaidi ya Sh300 bilioni.

Dk Luhende alisema katika mashauri mapya waliyonayo ni 1,700, mengine yakiwa ya miaka iliyopita.

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali iliyoanzishwa mwaka 2018 ina jukumu la kuratibu, kusimamia na kuendesha mashauri ya madai, yakiwemo ya haki za binadamu na Katiba yaliyofunguliwa na Serikali au dhidi ya Serikali.

Related Posts