Dar es Salaam. Wizara ya Afya, imeitaka jamii kujikinga dhidi ya ugonjwa wa malaria, ikitaja hatua za kuchukua kuepuka ugonjwa huo, huku takwimu zikionyesha kuongezeka kwa wagonjwa na vifo vya malaria nchini.
Kulala ndani ya chandarua chenye dawa, kufukia madimbwi, kufyeka nyasi, kupaka dawa zinazozuia mbu na kufika vituo vya afya pindi wanapopata homa, ni miongoni mwa hatua zilizopendekezwa, ili kujikinga na ugonjwa huo.
Aprili 30, 2024, akifungua kongamano la ‘Malaria Forum 2024’ Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu alisema kuna ongezeko la zaidi ya asilimia moja la malaria nchini, lililosababishwa na ongezeko la mvua.
Takwimu zinaonyesha Tanzania Bara vifo vimeongezeka kutoka 1,430 mwaka 2022 mpaka 1,954 mwaka 2023 na wagonjwa kutoka 3,478,875 mpaka 3,534,532 sawa na ongezeko la asilimia 1.6.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili, Mei 12, 2024 kuhusu malaria kali, Meneja Mpango wa Taifa wa kuzuia Malaria nchini, Dk Samwel Lazaro amesema kuna umuhimu mkubwa wa kufika katika kituo cha afya pindi mgonjwa anapohisi dalili za homa.
Ametaja changamoto iliyopo kuwa mtu anapata dalili za ugonjwa na haendi kituo cha afya kupima, wengi wakiishia maduka ya dawa au kujitibu kienyeji.
“Badala yake ule ugonjwa unakua mkali, anapata dalili za kuathirika baadhi ya viungo kama mapafu ambapo ataanza kupata magonjwa ya mfumo wa hewa, ubongo anaanza kupoteza fahamu au kwa watoto anapata degedege wakati mwingine figo na ini huathirika.
“Ndiyo maana kwenye ugonjwa wa malaria tunashauri anaposikia dalili awahi kupima, ndani ya saa 24 awe ameanza kupata tiba. Ukichelewa ndani ya saa 48 ugonjwa unaanza kuwa mkubwa na unaathiri baadhi ya ogani. Asilimia 99 wanaopata malaria kali walichelewa matibabu,” amesisitiza Dk Lazaro.
Licha ya hilo, Dk Lazaro ameagiza watu kuhakikisha wanapima afya vituoni na wataalamu ili kupunguza ugonjwa mkali, “Wengine hajapima anaona ni dalili anaenda kununua dawa bila kupima, anajitibu kumbe ana shida nyingine anachelewesha ugonjwa mwingine ni vizuri kupima.”
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Deus Ndilanha amesema ugonjwa mkali wa malaria unaongezeka kwa kadri wagonjwa wanavyoongezeka.
“Wagonjwa wengi wanafika na ugonjwa mkali sababu wamechelewa kupata matibabu. Kuna mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha mbu kuzaliana.
“Madaktari tunaona wagonjwa na tunawaambia wahakikishe wanalala ndani ya vyandarua, wasikae nje kwenye maongezi jioni sehemu hizi zina mbu, wawe na nguo zinazowafunika miili yao au watumie dawa za kupaka, kama kuna madimbwi wajaribu kuyafukia na kama kuna majani wayakate.”
Wakati angalizo hilo likitolewa, mkazi wa Tabata Segerea jijini Dar es Salaam Aboubakar Salim (45) aliyepata malaria kali na kupoteza fahamu wiki iliyopita, amesema alianza kuumwa kwa zaidi ya siku mbili.
“Nilijisikia vibaya nikiwa dukani kwangu. Nikameza dawa kutuliza maumivu, siku ya pili hali ikawa mbaya zaidi nilirudi nyumbani nikalala mchana jasho lilinitoka sana, baadaye sikumbuki nini kilitokea nilijikuta hospitali wakiniambia nilifika hapo siku mbili nyuma nikiwa na malaria kali,” amesema.
Hata hivyo baadhi ya wagonjwa wamesema hujikuta wakiumwa mara kwa mara na hata wanapotibiwa bado vipimo huonyesha wana maambukizi ya ugonjwa huo.
Mkazi wa Tabata Hai, Mwajuma Juma amesema: “Nimeumwa, nikaenda hospitalini wakabaini kuwa ni malaria. Nilipewa dawa nikaitumia nikajisikia vizuri nilipomaliza dozi nikarudi tena kupima, wamesema bado ipo nimebadilishiwa dawa lakini siwezi tena sitaki kulala tena kitandani.”
Mkazi wa Nyamirembe, Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita, Charles Frank amesema kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa mama yake mzazi (hakutaka kumtaja jina) amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo na ametumia dawa mbalimbali.
“Hii hatujui ni malaria gani ambayo haitaki kuisha, mama yangu anapimwa na kupewa dawa, anatumia, akirudi tena kupimwa anakutwa bado anayo, kila aina ya dawa ametumia lakini wapi,” alisema Frank na kuongeza:
“Kama miezi mwili nyuma alilazimika kulazwa Hospitali ya Kanda ya Chato kama siku tatu hivi kwa sababu hiyo. Juzi tu hali imebadilika, akapimwa presha iko sawa, malaria alivyopimwa bado imo. Nafikiri ni wakati wa Serikali kuangalia shida ni nini, hizi malaria zisizoisha.”
Kufuatia hilo, Dk Lazaro amesema mtu anapojisikia homa cha kwanza apime kama ni malaria ahakikishe anatumia dawa na anakamilisha dozi, kwani vituo vya kutokea huduma kama zahanati mpaka hospitali za mikoa wanatumia kipimo cha haraka.
Amesema mgonjwa anapotumia dawa kulingana na maelekezo, ndani ya siku tatu husikia nafuu na akishamaliza dozi anatakiwa akae ndani ya kipindi cha wiki mbili ndipo apimwe tena.
“Kipimo hakipimi wadudu, kinapima viashiria kama kulikuwa na wadudu. Ukishatibiwa huwa vinapotea ndani ya wiki mbili,” amesema.
Dk Ndilanha amesema huenda kupungua kwa kampeni za malaria, watu wakawa wameacha kuchukua tahadhari kujikinga.
“Matumizi ya vyandarua, kulikuwa na tangazo la Wizara ya Afya kabla au baada ya taarifa ya habari wananchi wanakumbushwa kuweka neti walale. Ile kampeni ilifanikiwa elimu ikawa kubwa na jamii ikafikiwa.”
Alipoulizwa iwapo kuna aina nyingine ya mbu inayosababisha ongezeko la malaria akiwemo mbu Steve aliyegundulika Kenya mwaka 2022, Dk Lazaro amesema mbu wanaosambaza ugonjwa wa malaria wapo wa namna mbalimbali tofauti.
Amesema Steve ana tabia ambazo ni tofauti na mbu tuliowazoea kwa kung’ata na kukaa nje ya nyumba ikilinganishwa na wale wanaong’ata na kukaa ndani.
“Steve tabia zake hukaa nje na kuuma watu wakiwa nje ya makazi, yeye ana usugu dhidi ya dawa tunazozitumia na anaeneza ugonjwa wa malaria kwa haraka zaidi na hupatikana mijini zaidi,” amesema.
Amesema tangu mwaka 2022 alivyobainika, Tanzania ilianza kufanya ufuatiliaji kwa kuweka vituo vya utafiti Dar es Salaam, Tanga na Kilimanjaro, “Tumefanya mara tatu kuangalia tunaowatega bado hatujathibitisha uwepo wa yule mbu ndani ya nchi.”
Dk Lazaro ameitaja mikoa inayoongoza kwa malaria kuwa ni ya Kaskazini Magharibi mwa nchi ikiwemo Tabora kwa asilimia 23.4, Mtwara 20, Kagera 18, Shinyanga 16 na Mara 15 huku iliyo chini ya asilimia moja ni pamoja na Dar es Salaam, Dodoma, Singida, Songwe, Iringa, Mwanza, Kilimanjaro, Manyara na Arusha.