JICHO LA MWEWE: Chasambi anakitu mguuni, amahitaji kuwa ‘kiburi’

ALHAMISI nilikwenda uwanjani kutazama mechi ya Simba na Azam. Simba na Azam? hapana. Ni Azam na Simba. Azam walikuwa nyumbani siku hiyo. Siku hizi mechi zao kubwa huwa wanacheza katika uwanja wa taifa hata kama wapo nyumbani.

Nilikutana na winga wa Simba anayeitwa Ladack Chasambi. Naambiwa Simba walilipa pesa nyingi kupata huduma za kinda huyu ambaye kwa mujibu hati yake ya kusafiria ana miaka 20 tu. Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia pia ana miaka hiyo.

Awali niliambiwa ni winga mkali. Wakati ule akitokea Mtibwa Sugar kutua Simba. Baada ya kutua Simba nikaona kimya. Naambiwa kwamba kocha wa Simba wa wakati huo, Abdelhak Benchikha hakuwa anampa nafasi kama ilivyotegemewa.

Nilimwona Chasambi Alhamisi jioni katika pambano dhidi ya Azam. Ana kitu. Kitu cha kwanza ni namna ambavyo anakokota kwa kujiamini mpira ukiwa katika miguu yake. Ana kasi lakini anajaribu kukokota kwa uhakika zaidi katika miguu yake. Sio kwamba anataka kuwaonyesha mashabiki kitu, hapana. Ndivyo alivyo.

Kitu kingine ambacho kilisababisha nimpende zaidi ni namna anavyojaribu kucheza winga ya kisasa. Unakaa upande wa kushoto lakini unatumia mguu wa kulia.

Ni kama ilivyo kwa kinda mwenzake, Edwin Baluwa ambaye alikaa upande wa kulia huku akitumia mguu wa kushoto. Sikuwa nawajua hapo awali sasa sijui kama walikuwa wanatumia staili hizo au wamekuja kubadilika Simba.

Ninachojua ni kwamba Chasambi alinikosha zaidi. Unapotumia mguu wa kulia halafu unakaa upande wa kushoto kama kina Gabriel Martinelli wanavyofanya ni kwamba unalazimika kuwa mpiga chenga mzuri, pia unalazimika kuwa mkatizaji mzuri kutoka katika winga yako na kuingia katikati.

Unapocheza kwa staili hii unamaanisha lengo kubwa ni kujaribu kukatisha katikati na kuingia ndani na haupaswi kupiga krosi kwa sababu unakuwa hauna raha sana na mguu wa kushoto ambao unatumika kupiga kwa wanaoutumia mguu wa kushoto na kisha kukaa upande wa kushoto.

Unalazimika kuingia ndani kama Mbwana Samatta anavyofanya wakati anapotoka katikati na kwenda upande huo. Zamani tulikuwa tunamuona Thierry Henry akifunga mabao mengi au kupika mengi kwa staili hiyo.

Chasambi kwa kujipeleka upande huo ni lazima awe na kasi lakini pia awe na uwezo mkubwa wa kupangua mabeki huku akijaribu kuingia kati. Hiki ndicho alichokuwa anajaribu kukifanya wakati siku ya kwanza nilipomtia machoni Alhamisi jioni, kisha usiku.

Kwanini Benchikha alikuwa hamchezeshi? Ni swali ambalo Benchikha hata kama amerudi kwao lakini ataendelea kukumbana nalo katika siku za usoni kama Chasambi akiendelea kujiamini katika jezi za Simba na kisha akaibuka kuwa mchezaji tegemeo.

Kuna mambo mawili hapa. Jambo la kwanza naweza kumjibia Benchikha. Nadhani alikuwa hataki masikhara na mshahara wake. kuna makocha ambao wanakuja kufanya kazi ya muda mfupi na kisha kuhitaji matokeo haraka. Hii inaitwa ‘Big results now’. Benchikha hakuwa na muda wa kukuza vijana au kuwapa muda wajiamini.

Alikuja akitafuta matokeo katika kila mechi ambayo ilimkabili usoni hasa kwa Simba hii ambayo ilikuwa haieleweki. Kila mechi kwake ilikuwa ngumu na sidhani hata kama alikuwa na muda wa kutembelea mechi za timu za vijana za Simba achilia mbali kuwaamini vijana ambao walikuwa katika timu yake ya wakubwa.

Kuna makocha wa namna hiyo. Hata Jose Mourinho ni kocha wa namna hiyo. Katika orodha yake anaweza kukuorodheshea wachezaji makinda ambao aliwapa mechi zao za kwanza timu ya wakubwa (debut) lakini alikuwa anafanya hivyo kwa kukokosha tu. Hakuwa na muda wa kumuamini kinda kama ambavyo Pep amewahi kufanya kwa kina Sergio Buqsuets au Phil Foden.

Benchikha anaonekana kuwa kocha wa namna hivyo. Mbele ya safari Chasambi anaweza kuwa mchezaji mkubwa lakini sidhani kama Benchikha atakuwa na majuto yoyote dhidi yake. Alikuja kusaka matokeo na sio kutengeneza timu.

Lakini kuna jambo la pili ambalo linamkabili Chasambi. Inabidi akomae kiakili mapema kwa nafasi chache ambazo ameanza kupewa Simba. kuna huu ukweli hapa mchezaji kama Clement Mzize amepata nafasi na kuitumia kwa sababu anacheza katika Yanga inayopitia kipindi kizuri.

Ilikuwa rahisi wa kocha wa Yanga, Mohammed Nabi kumtoa Mayele katika dakika ya 75 wakati Yanga inaongoza mabao 3-0 na kumuingiza Mzize. Leo Simba haina raha hiyo.

Ni ngumu kwao kuongoza pambano la soka kwa idadi kubwa ya mabao.

Pia Mzize alikomaa haraka kwa sababu alikuwa anacheza katika Yanga ambao muda mwingi ina mpira. Yanga ambayo inashambulia. Yanga ambao inaogopwa na wapinzani. Ni rahisi kumkuza mchezaji katika mazingira hayo. Hata Foden na Trent Alexander Arnold wamekulia katika timu za namna hiyo.

Ile Yanga ya akina David Molinga sidhani kama Mzize angekuwa na raha hii. Hapa ndipo na Chasambi inabidi akomae kiakili kwa haraka kwa sababu makocha wanaweza kukuamini lakini viongozi na mashabiki wakawa na wasiwasi mkubwa juu yako.

Niliona katika pambano lile. Mwanzoni alikosea mara mbili tatu lawama za mashabiki zikawa nyingi. Wakati mwingine inaweza kukutoa mchezoni. Unahitaji kuwa na ukomavu wa akina. Simon Msuva alipotua Yanga akiwa kinda alijikuta katika mazingira haya lakini akawa na ukomavu wa akili na ujeuri wa kutoogopa chochote mwishowe kila kitu kikakubali akawa miongoni mwa mastaa wa timu.

Wakati huu Simba ikiwa inapitia katika majaribu ya hapa na pale Chasambi inabidi awe hivi. Inabidi awe ‘mjeuri’, mwenye kujiamini katika uwezo wake na kufanya maamuzi makubwa uwanjani. Mashabiki watamkubali tu.

Nimeona ana kitu katika miguu yake. Asikubali kupotea kirahisi. Nawajua wachezaji kadhaa ambao miaka ya karibuni wamepita Simba na Yanga na walionekana mali huko walikotoka lakini baada ya kuvaa jezi za hizi timu wakakosa kujiamini.

Jiulize kuhusu Waziri Junior. Alitua zake Yanga akitokea Mbao ambako alikuwa amefunga mabao lukuki. Akatua mjini akawa anakosa mabao ya wazi pale Yanga.

Leo amerudi KMC anawafukuza kwa mabao Aziz Ki na Feisal Salum. Ukiona hivyo, alikosa ukomavu wa kiakili wakati akiwa katika ile timu ya Kariakoo.

Related Posts