Dar es Salaam. Unaweza kusema siku ya kwanza ya kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ilikuwa sawa na moto.
Kinaelezwa kuwa kilikuwa kikao cha kusemezana, kuonyana na kuambiana ukweli.
Kikao hicho kilichoanza juzi saa tano asubuhi, licha ya kuwa na ajenda kadhaa, kilishuhudia Makamu Mwenyekiti-Bara, Tundu Lissu akiwasilisha ushahidi wa kauli yake kuhusu tuhuma ya rushwa kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Awali, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema, alieleza pamoja na mambo mengine, kikao hicho kingepokea taarifa ya uchaguzi katika ngazi mbalimbali.
Pia, kupokea taarifa ya tathmini ya maandamano ya awamu ya kwanza ya mikoa katika ‘wiki ya maandamano’ na kuweka mwelekeo awamu ya pili ya maandamano.
Pia kufanya usaili na kuteua wagombea nafasi za uongozi katika kanda nne za Nyasa, Serengeti, Victoria na Magharibi.
Hata hivyo, licha ya ajenda hizo, Mwananchi lilidokezwa kuwa kauli ya Lissu kuhusu tuhuma za rushwa, iliibua joto kikaoni.
Chanzo kutoka ndani ya chama hicho, kilieleza kuwa Lissu aliyewahi kuwa mbunge wa Singida Mashariki, aliwasilisha ushahidi wake kuhusu kauli yake aliyoitoa Mei 2, mwaka huu mkoani Iringa, akidai uwepo wa fedha zilizomwagwa kwenye uchaguzi wa ndani wa Chadema.
Katika hotuba yake siku hiyo Lissu alisema: “Wakati nakuja hapa Iringa jana na juzi kulikuwa na mtafaruku mkubwa sana, sijui kama mnafahamu, ndani ya chama chetu kuna pesa nyingi ajabu kwenye uchaguzi huu.’’
Kauli hiyo ya Lissu iliibua mjadala ndani na nje ya Chadema. Makada wa chama hicho waligawanyika wapo waliomuunga mkono na wapo waliodai inakigawa chama kuelekea uchaguzi wa kanda.
Baada ya mjadala huo kushika kasi, Mei 5, mwaka huu, alipoulizwa na gazeti hili, Lissu alisema kauli yake hiyo haina tofauti na ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa akikemea rushwa ndani na nje ya CCM.
Mbali na makada wa chama hicho, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, Mei 7 mwaka huu, alipofanya ziara ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini, jijini Dar es Salaam, aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufanyia kazi madai hayo ya Lissu.
Baada ya Makalla kueleza hayo, gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni aliyesema wanaendelea kufanyia kazi taarifa hizo za Lissu.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema: “..Sisi hatuwezi kuendeshwa na vitu vinavyosemekana kwenye mitandao ya kijamii. Ofisi yetu inafuatilia si kwamba imepuuza au kukalia kimya lakini pia suala hili tunashindwa kutumia nguvu, inawezekana kuna ushindani ndani ya vyama ndiyo maana mtu anakurupuka na hayo maneno.
Taarifa za ndani zinaeleza Lissu aliwasilisha ushahidi huo saa 2 usiku baada ya wajumbe wa kamati kuu kutoka mapumzikoni na kuingia ngwe nyingine ya mwendelezo wa kikao hicho cha siku tatu kitakachomalizika leo, kisha maazimio kusomwa kwa umma na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
“Kilikuwa ni kikao cha kusemezana, kuonyana na kuambizana ukweli kwenye upungufu ili kuweka mambo sawa kwa mustakabali wa chama, lakini pia makamu mwenyekiti (Lissu), aliwasilisha ushahidi wake wa kauli ya rushwa,” alisema mmoja wajumbe wa kikao hicho.
Hata hivyo, Mwananchi lililokuwa limeweka kambi katika mkutano huo unaofanyikia ofisi mpya za chama hicho Mikocheni jijini Dar es Salaam, lilimfuata Lissu leo Jumapili Mei 12 2024 na kumuuliza kuhusu suala hilo.
Alijibu:”Nitafute siku nyingine nikwambie sio leo.”
Mwananchi halikuishia hapo, lilimtafuta Mrema ambaye alijibu kwa kifupi: “Hilo silijui naomba umtafute mwenyewe (Lissu).”
Licha ya wawili hao kutoweka bayana, gazeti hili limedokezwa kuwa Lissu aliwasilisha ushahidi wake, huku akiwataja baadhi ya wanachama waliohusika katika mchakato huo.
“Hili suala ni zito na leo hatukulimaliza vizuri. Labda litaendelea kesho. Unajua Lissu si muoga, kama ana ushahidi anakusema waziwazi hana kificho,” alisema mjumbe mwingine wa kikao hicho.
Taarifa nyingine zinadai huenda suala la kufutwa uchaguzi wa Mkoa wa Njombe unaodaiwa kugubikwa na ‘figisu’ likajadiliwa na kutolewa uamuzi kesho, sambamba na kupanga tarehe rasmi ya mchakato wa uchaguzi wa kanda nne ambapo wagombea wake walifanyiwa usaili kuanzia jana.
Hadi leo jioni wagombea wa nafasi za mabaraza ndani ya Chadema yakiwemo ya wazee (Bazecha), wanawake (Bawacha) na vijana (Bavicha), ndio waliokuwa wakiendeleaa na usaili, wakati wagombea wa uenyekiti na umakamu wa kanda, walikuwa wakisubiri kuanza kwa mchakato huo nyakati za usiku.
Baadhi ya watia nia waliozungumza na Mwananchi walisema hatua ya usaili kufanyika makao makuu ya chama, imepunguza baadhi ya makandokando yaliyokuwa yanajitokeza wakati mchakato ukifanyikia kwenye kanda.
“Kulikuwa na misuguano ya hapa na pale kwa sababu wote mnataka nafasi moja lazima changamoto, lakini tumekuja huku hakuna watu wala wapambe ambao wanaweza kusema fulani tunamtaka. Tupo wenyewe tunabadilisha mawazo na kucheka,” alisema Ester Jackson anayewania umakamu uenyekiti wa kanda ya Serengeti.
Mtia nia nafasi ya Mwenyekiti kanda ya Magharibi, Wakili Dickson Matata, alionyesha kufurahishwa na mchakato wa usaili kuletwa Dar es Salaam na kusimamiwa na Kamati Kuu.
“Ni vizuri imekuja kufanyika Dar es Salaam kwa sababu imetoa fursa kwa watia nia kutumia nauli zao kufika hadi hapa, kuonyesha namna gani wanavyohitaji kukitumikia chama.
Alisema changamoto ya kufanyia usaili ngazi ya kanda siasa zake zinakuwa si rafiki kutokana na baadhi ya viongozi kuwa wajumbe ngazi ya kamati kuu.
“Itasaidia kupunguza lawama zilizokuwa zinajitokeza baada ya usaili kufanyika,” alisema Wakili Matata.
Wakili Matata alisema joto la uchaguzi huo ni kubwa kutokana na kuwapo wagombea wengi kwenye kila nafasi.
Mathalani katika nafasi ya Mwenyekiti, alisema katika kanda ya Magharibi wapo wanne.
“Wote ni wazuri lakini usaili utaamua tupite wote na tukipita wanachama watakuwa na fursa ya kuchagua kulingana na vipaumbele vya kila mgombea atakayekuwa amepitishwa na Kamati Kuu,” alisema.
Afichua sababu usaili kufanyika Dar
Meya wa zamani wa Iringa, Alex Kimbe anayegombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti kanda ya Nyasa, alifichua sababu ya kanda hizo kuja kufanyiwa usaili na Kamati Kuu ya chama hicho Dar es Salaam.
Alisema ndani ya chama hicho kanda ya Nyasa, Serengeti na Victoria, zinaongoza kwa kuwa na wababe wengi na iwapo michakato hiyo ingefanyika kwenye maeneo hayo haki isingetendeka.
“Binafsi nina amani bora kamati kuu imekuja kutufanyia usaili haki itatendeka. Mfano katika kanda yetu tuna mwenyekiti wetu lakini yeye ni mgombea halafu ni mjumbe wa Kamati kuu lazima kusingekuwa na haki.”
“Sijisifii nina uzoefu na uwezo wa kujenga hoja na wataalamu wanasema divai ikikaa muda mrefu inatoa utamu, hivyo nafaa sasa hivi nipo kwenye utamu watu wanahitaji ili wainywe vizuri,” alisema.
Mtia nia nafasi ya uenyekiti kanda ya Serengeti, Emmanuel Ntobi alisema akipitishwa na wanachama wakimchagua, shabaha yake ni kuhakikisha wanashinda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
“Nikishinda naweka mipango ya kutafuta fedha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu katika mikoa yote na kufanya ugatuzi wa madaraka kikanda kwa kuzingatia haki , nitaendesha kanda kwa kuzingatia fikra mpya,” alisema.
Alisema joto la uchaguzi huo lipo juu kwa sababu kila mkoa umetoa mgombea na wana uhitaji mkubwa na mwakilishi wao kwa hiyo si uchaguzi rahisi hata ukipenya kwenye mchujo.
Baada ya kuzungumza watia nia hao, Mwananchi lilizungumza na Lissu ambaye kwa nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti-Bara ndiye mwenyekiti wa kamati ya maadili ya chama hicho.
Alisema kama utaratibu wa chama chochote ulivyo, watia nia hao watapenya iwapo tu watakuwa wamekidhi vigezo stahiki.
Kikao hicho kinachowaleta pamoja vigogo mbalimbali wa chama hicho kikubwa cha upinzani Tanzania Bara, kinatarajiwa kufikia tamati kesho.