Dar es Salaam. Mtumishi wa Halmashauri ya Kisarawe mkoa wa Pwani, Salum Kunikuni (29) amepotea tangu Aprili 23, 2024 alipokuwa anaelekea kazini akitokea nyumbani kwao Zingiziwa.
Salum ambaye ni dereva wa Halmashauri ya Kisarawe akiendesha magari ya kitengo cha kilimo, tangu kutoweka kwake bado juhudi za kumtafuta hazijazaa matunda.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 12, 2024 mke wa Salum, Nuru Jumanne (26) amesema mumewe aliondoka kuelekea kazini saa 11:45 alfajiri na ilipofika saa mbili asubuhi alipowasiliana naye iwapo amefika kazini kwake, hakufanikiwa kumpata.
“Kwa kawaida huwa anaondoka asubuhi na ikifika saa mbili lazima nimuulize kama amefika salama, lakini siku hiyo nilituma ujumbe lakini sikujibiwa na nilipopiga simu haikuwa hewani hivyo nikafikiria kuwa itakuwa ni tatizo la mtandao,” amesema.
Amesema ilipofika mchana alijaribu tena kumtafuta lakini simu yake haikupatikana, hata alipojaribu jioni majibu yalikuwa yaleyale, ndipo alipoamua kutoa taarifa kwa mama mzazi wa Salum.
Kufahamu kama Salum alikuwa na changamoto yoyote, amesema hakuwa na jambo linalomtatiza wala kugombana na mtu, kwani hana tabia za ugomvi isipokuwa kipindi cha nyuma alipotea siku mbili na baadaye walimpata lakini safari hii imekuwa ni muda mrefu.
Kwa upande wake mama mzazi Zaina Mahimbo, amesema kijana wake alimuaga asubuhi kuwa anaondoka lakini kutokupatikana kwake taarifa amepewa na mkwewe.
“Nilipoambiwa kuwa mwanangu hapatikani ikabidi niende kazini kwake, lakini nilipofika niliambiwa hakufika hiyo siku na nilijaribu kupigia marafiki zake wa karibu, mmoja alisema alimuona siku moja kabla ya kupotea,” amesema Zaina.
Katika kufahamu kama ofisi yake ina taarifa ya kupotea kwakwe, Zaina amesema waliongea na Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Kisarawe.
Pia, amesema ameshatoa taarifa katika kituo kikuu cha Polisi Chanika ya kupotea kwa kijana wake ambapo amepewa RB namba CNK/RB/1990/2024 na mpaka sasa hajaonekana na simu zake hazipatikani.
Aidha, amesema kijana wake ana watoto wawili ambapo mmoja wa miaka saba yupo darasa la pili na mwingine ana miezi sita na ameshazunguka maeneo yote aliyoelekezwa lakini hakumpata.
Ofisa Utumishi Halmashauri ya Kisarawe, Baptista Kihanza amekiri kupokea taarifa ya mtumishi wao huyo kutoka kwa wazazi wake na aliwapa ushauri wa kuripoti polisi.
“Nikweli huyo ni mtumishi wetu na taarifa ya kupotea kwake nilizipata kwa wazazi wake, niliwashauri waende polisi ili wakipata lolote watupe taarifa,” amesema Kihanza.
Amesema kupotea kwa kijana huyo inakuwa ni mara ya pili, kwani awali hakuonekana siku mbili na altoa ruhusa ya kutibiwa kwanza kwa kuwa hakuwa kwenye hali nzuri.
Mwananchi ilipomtafuta Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Yustino Mgonja simu yake iliita bila mafanikio.