Dar es Salaam. Denis Mfumbulwa (44) ambaye ni mkazi wa Goba Kulangwa, amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, kujibu shitaka la kujipatia huduma ya chakula na malazi yenye thamani ya Sh 21.4 milioni kwa njia ya udanganyifu katika Hoteli ya Serena.
Mfumbulwa amefikishwa mahakamani hapo leo Mei 13, 2024 na kusomewa shitaka lake na Karani wa mahakama hiyo, Aurelia Bahati mbele ya Hakimu Mkazi, Gladness Njau.
Bahati amedai mshtakiwa anadaiwa kwa nyakati tofauti kuanzia Machi 6, 2022 hadi Machi 28, 2024 katika Hoteli ya Serena iliyopo mtaa wa Ohio Wilaya ya Ilala, alijipatia huduma ya chakula na malazi yenye thamani ya Sh21,491,866.97 milioni bila kulipa, mali ya mlalamikaji Desdery Dotto.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo baada ya kutumia huduma hizo, alitoweka kusikojulikana.
Karani Bahati alidai kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, huku akijua kitendo hicho ni kinyume na sheria. Ambapo Mfumbulwa alikana shitaka linalomkabili na kuomba apatiwe dhamana.
Hakimu Njau ametoa masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wenye barua zinazowatambulisha na mmoja kati yao anatakiwa kusaini bondi ya Sh10 milioni.
Mfumbulwa ameshindwa kutumiza masharti ya dhamana na hivyo kurudishwa rumande.
Hakimu Njau ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 15, 2024 kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.