AZAM FC imedhamiria kwa dhati kumrudisha aliyekuwa kipa namba moja wa kikosi hicho, Aishi Manula baada tu ya msimu huu kuisha.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimekaririwa na Mwanaspoti kwamba viongozi wanataka kumrejesha nyota huyo aliyeondoka ndani ya kikosi hicho Agosti 9, 2017 huku akiwa ni moja ya makipa bora nchini kutokana na kiwango chake anachokionyesha.
Hesabu hizo zinakuja baada ya Azam kutaka kuwaondoa makipa wawili waliopo Mcomoro, Ali Ahamada anayelipwa kiasi kikubwa cha fedha na Mghana, Abdulai Iddrisu ambaye pia inaelezwa hana uhusiano mzuri kikosini humo na Kocha, Youssouph Dabo.
Ahamada na Iddrisu ambao wote kwa sasa ni majeruhi inaelezwa huenda wakatolewa ili kupisha usajili wa Manula ili aende kusaidiana na kipa, Mohamed Mustafa aliyepo kwa mkopo akitokea Al-Merrikh kwani viongozi wanahitaji kumsajili moja kwa moja.
Manula alihitajika mwanzoni tu kujiunga na timu yake ya zamani ingawa dili hilo lilishindikana kwa kile ambacho Simba ilihitaji kubadilishana na kiungo nyota wa kikosi hicho, Sospeter Bajana jambo ambalo viongozi wa Azam hawakukubaliana nalo.
Hata hivyo taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza viongozi wa Azam wameanza kumfuatilia Manula ili kutaka kujua ukubwa wa jeraha la oparesheni ya nyonga aliyofanyiwa huku madaktari wa timu hiyo wakielezwa kumtibia ili apone haraka.
“Ni kweli kumekuwa na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Simba na viongozi wa Azam wakihitaji kumrudisha tena ndani ya timu hiyo, jambo nzuri ni kwamba mchezaji mwenyewe ameonyesha nia ya kuondoka mwisho wa msimu,” kilisema chanzo hicho.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema, jambo lolote ambalo linawahusu kama klabu wana utaratibu wao mzuri wa kulitolea taarifa kupitia vyanzo vyao mbalimbali ikiwa kuna ulazima.
“Taarifa zote huwa tunaziweka katika mitandao yetu rasmi ya klabu hivyo nisingependa kulizungumzia hilo kwa sasa kwa sababu ni tetesi kama zilivyokuwa nyingine, mashabiki zetu watapata ukweli wowote pale ambapo tutakamilisha kila kitu.”
Kwa upande wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema suala la mchezaji kubaki au kuondoka litafahamika baada ya msimu kuisha ingawa wao kama viongozi lengo lao ni kubaki na wachezaji wao wote waliokuwa bora kikosini humo.
Manula ameonyesha uwezo mkubwa hadi kuitwa ‘Tanzania One’ ambapo sio bahati mbaya kwani tangu ajiunge na Simba ametwaa mataji mengi yakiwemo ya Ligi Kuu Bara kwa mara nne mfululizo kuanzia msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.
Mbali na mataji hayo ila amechukua tuzo nyingi binafsi huku akikiwezesha kikosi hicho kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara tano kati ya sita mfululizo huku mara moja ikiwa ni la Kombe la Shirikisho la Afrika.
Kipa huyo ambaye amekuwa panga pangua ndani ya Simba, kwa sasa amekuwa na msimu mbovu kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara huku akiachia nafasi kwa Mmorocco Ayoub Lakred anayeonyesha kiwango bora tangu alipotua msimu huu akitokea FAR Rabat ya nchini humo.
Tayari Azam imeanza usajili mapema kwa ajili ya msimu ujao kwani tayari imenasa saini ya beki wa kati, Yoro Mamadou Diaby aliyetokea akademi ya Yeleen Olympique na kiungo mshambuliaji Franck Tiesse kutoka Stade Malien zote za Mali.