Mtwara. Baada ya ufuta kuuzwa kwa Sh4,000 katika mikoa ya Lindi na Mtwara msimu uliopita Mkoa wa Songwe umeweka rekodi kwa kuuza zao hilo kwa Sh4,500 kwa kilo msimu huu hali ambayo inaongeza matumaini kwa wakulima.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Mratibu wa programu ya ufuta kitaifa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) Kituo cha Naliendele, Joseph Nzunda amesema kuwa bei hiyo inaleta matumaini kwa wakulima wa mikoa mingine wanaolima zao hilo hasa Lindi na Mtwara.
Amesema kuwa zao hilo lina mahitaji makubwa nchini na duniani ambapo uzalishaji ni mdogo hali ambayo imewalazimu kuhamasisha wakulima kwa kuwapa mbegu bure, ambapo katika msimu uliopita zaidi ya tani 250,000 zilirekodiwa baada ya kuuzwa kwenye njia rasmi ya minada.
“Bado uzalishaji ni mdogo ndio maana soko halitetereki kwa kuwa mahitaji ni makubwa na walimaji duniani ni wachache, mfano juzi tumeuza ufuta kwa Sh4,500 mkoani Songwe naamini bei zitaendelea kupanda, yaani ukiwa na tani moja ambayo ni sawa na kilo 1000 hapo unazungumzia zaidi ya Sh4 milioni” amesema Nzunda.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tari Kituo cha Naliendele, Dk Furtunus Kapinga amesema kuwa wana jukumu la kuangalia ubora wa ufuta kuanzia shambani hadi unapopelekwa sokoni.
“Wakati mwingine mkulima anaweza akawahi kuvuna au kuchelewa akapoteza ufuta mwingi shambani hii inaweza kusababisha ufuta sokoni ukiwa hauna , hivyo ni vema wakavuna muda muafaka wakati majani yakiwa na rangi ya njano.”
“Wakulima wahakikishe unakomaa sana usivunwe ukiwa mbichi italeta shida kwenye sokoni lazima kutambua kuwa kilimo ni biashara tuzingatie ubora ili mnunuzi anunue kile ambacho amedhamiria kukinunua,” amesema Kapinga
Mohamed ,mkulima wa ufuta katika Kijiji cha Kipelele wilayani Liwale amesema kuwa bei za ufuta mkoani wa Songwe zinawapa hamasa zaidi.
Amesema kuwa katika msimu uliopita alivuna tani 4.3 ambapo aliuza kwa Sh4,000 na mwaka huu ana matumaini kupata zaidi ya mavuno ya awali .
“Kwa kweli tuna matarajio makubwa na zao hili la ufuta tunatamani kuona na sisi bei ikipanda kwa kuwa tunatumia pesa nyingi kuandaa mashamba, dawa na kulima tukiuza kwa bei ya SH5,000 itasaidia.”