Dodoma.Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka viongozi wa dini, kuishi wito wao wa kinabii, kusema na kuutetea ukweli kwa ajili ya maslahi ya wananchi hasa wanyonge na wafanye hivyo kwa uhuru bila woga.
Ameyasema haya leo Jumapili Mei 12, 2024, jijini Dodoma kwenye Misa Takatifu ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Msaidizi Wilbroad Kibozi iliyofanyika Kituo cha Hija Miyuji jijini Dodoma
“Kanisa na madhehebu ya kweli ndio dhamira ya jamii na tunatarajia viongozi wa dini kuishi wito wenu wa kinabii, mkisema na kuutetea ukweli kwa ajili ya maslahi ya wananchi hasa wanyonge tena.
Mfanye hivyo kwa uhuru bila woga lakini angalizo langu mfanye hivyo bila kuathiri amani na umoja wa kitaifa,” amesema Dk Mpango aliyekuwa akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Amewataka waendelee kuwakumbusha waumini na Watanzania kuwa haki inaambatana na wajibu.
Aidha, Dk Mpango amesema kuna changamoto za malezi ya watoto ambazo husababishwa na mambo mengi ikiwemo matumizi mabaya ya maendeleo ya teknolojia ya habari, mawasiliano na mwingiliano holela wa mila na desturi za mataifa mbalimbali.
Amesema mathalani moja ya matumizi mabaya ya Tehama ni kudhoofika kwa muunganiko wa kindugu au kirafiki kati ya wazazi au walezi na watoto wao ambao umesababisha kukosa upendo kutoka kwao.
“Lakini ukatili unaowezeshwa na mitandao unatishia usalama wa watoto ambapo watoto wetu wanarubuniwa ili kujihusisha na vitendo viovu. Nawaomba wazazi na walezi kutenga muda kujenga urafiki na watoto ili kufahamu maendeleo yao na marafiki zao,”amesema.
Alisema kwa kufanya hivyo kunawezesha watoto kuwa huru kueleza changamoto zote wanazokumbana nazo na hivyo kuwasaidia mapema.
Pia, Dk Mpango alisema wapo vijana wengi wenye umri wa kufanya kazi lakini hawajishughulishi na kazi yoyote ili kujikimu na maisha, jambo ambalo limewafanya kuwa tegemezi.
“Ukiacha, wazee, watoto na walemavu, ukiwa tegemezi hadhi yako inapungua mbele ya jamii. Nitumie hadhara hii kuwataka vijana kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato kitakachowawezesha kujikimu kimaisha,” amesema.
Dk Mpango amewataka vijana kutochagua kazi na kuwa kazi nyingi za staha hivi sasa zipo katika kilimo cha mbogamboga, matunda, ufugaji.
Pia amesisitiza kuhusu utunzaji wa mazingira, kupenda kufanya usafi, kutunza na kuhifadhi mazingira.
Aidha, amesema Rais Samia ameahidi kuchangia ujenzi wa Kituo cha Hija Sh50 milioni na ujenzi unaoendelea wa Basilika katika Parokia ya Kizota jijini Dodoma Sh50 milioni.
Dk Mpango aliambatana na mawaziri, Jenista Mhagama (Sera, Uratibu na Bunge), Innocent Bashungwa (Ujenzi) na Anthony Mavunde (Madini). Pia, alikuwapo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillius Wambura na Mkuu wa Majeshi mstaafu (CDF), Venance Mabeyo.
Askofu Mkuu Kinyaiya amsimulia Kibozi
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya amesimulia jinsi ilivyokuwa ngumu kwa Wilbroad Kibozi kupokea taarifa za uteuzi wa kuwa Askofu Msaidizi kutoka kwa Baba Mtakatifu, Francisko.
Katika mahubiri yake, Askofu Kinyaiya amesema anafahamu Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Mkuu Angelo Accattino alipompigia simu kumweleza kuhusu uteuzi wake, alihangaika kama ilivyokuwa kwa Mtume Jeremiah.
“Nafahamu Balozi wa Baba Mtakatifu alipokupigia simu, ulikuwa safarini kuelekea Kahama (Mkoa wa Shinyanga), na baada ya kukueleza kwa kifupi alichotaka kutoka kwako, ulimwambia mzee nadhani ulichanganya majina,” amesema.
Hilo amesema hiyo ndio sababu ya Balozi huyo kuamua kumuita (Kibozi) jijini Dar es Salaam ili waonane uso kwa uso.
“Nashukuru Mungu kwamba mwisho ulikubali, lakini kwangu mimi ni dalili ya uteuzi wako ulitoka kwa Mungu,”amesema.
Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga alimpongeza na kumtakia heri Kibozi katika huduma aliyoanza kuitumikia.
“Wewe mwenyewe umesema wakaacha yote wakamfuata bwana basi uwe na moyo mkuu katika kuacha yote, umfuate bwana ukiandamana na watu utakaowasaidia kushika Imani yao,” alisema Askofu Mkuu Nyaisonga.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu, Accattino aliwataka Watanzania kuwa makini katika kuyatunza, kuyalinda mazingira kwa kuhakikisha yanakuwa mazuri wakati wote.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Kardinali Protase Rugambwa amewataka waamini wa dhehebu hilo kuungana kwa pamoja kwa kutembea kama kanisa la kiisinodi kuifanya kazi ya unjilishaji.
“Tunawaombea hawa lakini pia tunajiombea sisi, tunapenda sote tuifanye kazi hiyo kwa pamoja ya uinjilishaji. Tuifanye tukiwa tumeungana, sisi kama kanisa na sisi kama wananchi Watanzania. Kama Watanzania tukiwa tunayajenga hayo yote kwenye misingi ya upendo, amani, mshikamano pamoja na umoja,” amesema Kardinali Rugambwa.
Akizungumza Askofu Kibozi alimshukuru Askofu Mkuu Kinyaiya kwa kuona anaweza kuwa msaada na kupokea kwa imani uteuzi wake wa kuwa miongoni mwa wasaidizi wake wa karibu.
“Nakushukuru kwa sala zako kuanzia mwanzo hadi sasa na nategemea utaendelea kuwa mwema na mwelekezi kwangu katika utumishi wetu,” alisema.
Askofu Kibozi aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko Februari 12, mwaka huu baada ya kukubali ombi la Askofu Kinyaiya la kutaka msaidizi wa shughuli za kitume katika Jimbo Kuu la Dodoma.
Askofu Kibozi ambaye hadi uteuzi alikuwa ni Makamu Gambera na Profesa wa Seminari kuu ya Familia Takatifu, Kahama, alizaliwa Aprili 30 Aprili 1973 kata ya Lumuma, Wilayani Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma.
Kwa mujibu wa tovuti ya Vatican, Askofu Kibozi alisoma masomo yake ya falsafa katika seminari kuu ya Ntungamo na masomo ya thiolojia katika seminari kuu ya Kipalapala, jimbo kuu Katoliki la Tabora.
Baada ya kufanya shughuli za kichungaji kwa muda wa mwaka mmoja katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji huko Chalinze (Dodoma), aliendelea na masomo na kupata leseni na Shahada ya Udaktari wa Taalimungu katika Kitivo cha Taalimungu cha Italia ya Kati huko Firenze.
Askofu Kibozi aliwahi kuwa Paroko Msaidizi wa Lumuma (2010 -2012), Mkurugenzi wa Miito jimbo Kuu la Dodoma (2012-2014) na Muunganishi katika nyumba ya malezi Livorno, Italia (2017-2019).
Pia amehudumu kama mkufunzi wa waseminari katika Chuo Kikuu cha Jordan, Morogoro (2019-2020) kabla ya kuwa Makamu Gombera katika seminari kuu ya Mwendakulima, Kahama.