Benki ya NMB imetanua wigo wa kushiriki katika masoko ya mitaji kimataifa kwa kuiorodhesha Hati fungani ya NMB Jamii (NMB Jamii Bond) katika Soko la Hisa la London (LSE) leo Jumatatu.
Hatua hiyo inaifanya NMB kuwa taasisi ya kwanza Tanzania kuwa na hati fungani katika soko hilo na Benki ya Kwanza Afrika Mashariki kuorodhesha Hatifungani ya Uendelevu LSE. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Hati Fungani ya NMB Jamii inalenga kuchochea uwekezaji katika miradi yenye tija kijamii na kimazingira, na toleo la Dola za Marekani 73 milioni ndio limeorodheshwa kwa wawekezaji wa LSE.
Uzinduzi wa mauzo ya Hati fungani ya Jamii ulifanyika wakati wa ufunguzi wa shughuli za wiki hii za LSE, na kuhudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mbelwa Kairuki; Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna; Mhazini wa NMB, Aziz Chacha; Afisa Mtendaji Mkuu wa LSE, Julia Hoggetts na viongozi wengine waandamizi kutoka Serikali ya Uingereza na taasisi mbalimbali.
“Tulianza kwa kuiorodhesha hati fungani hii katika Soko la Hisa la Dar es Salaam mwaka jana, Soko la Luxembourg mwezi uliopita, na leo tunaiorodhesha hapa LSE ili kuwapa wawekezaji wanaozingatia uendelevu, fursa ya kuchangia mabadiliko huku wakipata faida nzuri ya uwekezaji wao,” Zaipuna alieleza.
Zaipuna alisema masoko ya kimataifa yanaiwezesha benki yetu kuwa na wigo mpana wa kupata fedha kwa ajili ya kufadhili miradi inayosaidia kuboresha maisha, kubadilisha jamii na kuwa na mustakabali bora kwa watu wote.
“Mafanikio haya kipekee yanadhihirisha imani waliyokuwa nayo wawekezaji wa Kitanzania na Kimataifa katika uthabiti wa Benki ya NMB na dhamira yake ya uendelevu katika utendaji wake, biashara, jamii na masuala ya mazingira,” alisema.