Machupa: Simba ya 1999 inaweza kujirudia

WAKATI Simba ikikosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo, mshambuliaji wa zamani wa Simba, Athuman Machupa ameitaka usajili ujao kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji, kiungo na beki wa kati kwa kutafuta wachezaji bora watakaoisaidia kubeba ubingwa.

Machupa ambaye amestaafu soka la ushindani, amesema kati ya mwaka 1999 hadi 2007 Simba ilisuka kikosi tishio anachoamini viongozi wanaweza wakafanya kwa mara nyingine na kurejesha ubabe wao katika mashindano mbalimbali nchini.

Machupa ambaye kahamishia makazi yake nchini Sweden, amesema anapopata muda hufuatilia kinachoendelea katika Ligi Kuu Bara na kwa mtazamo wake ari ya wachezaji wa Simba ipo chini na timu inapofanya vibaya huwa inatokea mara nyingi kwa wachezaji.

“Simba ina kikosi kizuri, ingawa sijaifuatilia sana, ila waongeze mshambuliaji, kiungo na beki ambao watakuwa wanasaidiana na waliopo sasa,” amesema.

“Kwa soka la sasa ni rahisi wachezaji kutajirika, tofauti na zamani ambapo sisi tulikuwa tunategemea mapato ya kiingilio, ila sasa wanasajiliwa kwa dau kubwa, hivyo ni juu yao wenyewe kujituma ili kufanya biashara zao ziwe bora zaidi.”

“Kipindi hiki ni rahisi zaidi kupata vipaji vikubwa, kwani soka linaonyeshwa, lakini msisitizo wangu muendelezo wa viwango uwanjani, ni jambo ambalo linahusika na wachezaji wenyewe kuheshimu kazi zao,” amesema.

Related Posts