Mbeya. Timu ya madaktari bingwa 35 imewea kambi ya siku tano jijini hapa kwa ajili ya kutoa huduma bure za uchunguzi na matibabu ya kibingwa kwa wananchi.
Kambi hiyo imeanza leo Jumatatu Mei 13, 2024 itadumu hadi Mei 17 mwaka huu na itahusisha hospitali zote za wilaya zilizopo katika halmashauri saba za Mkoa wa Mbeya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo Katibu Tawala Mkoa, Rodrick Mpogolo amesema wamewapokea madakrari 35 na kila halmashauri watapelekwa madaktari bingwa watano.
Miongoni mwa huduma za uchunguzi na matibabu yatakayotolewa ni ya wanawake, wajawazito, watoto njiti, dawa za usingizi, ganzi, upasuaji wakiwepo wagonjwa wa ndani na nje.
Amesema lengo la Serikali kusogeza huduma kwa wananchi ni kutaka waondokane na changamoto za kutembea umbali mrefu.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Elizabeth Nyema amesema uwepo wa madaktari bingwa na bobezi hao utasaidia kupunguza msululu wa wagonjwa waliokuwa wanahitaji huduma za kibingwa, lakini walikuwa hawazipati kwa wakatika kutokana na upungufu wa madaktari hao katika hospitali za rufaa.
Dk Nyema amesema wana kila sababu ya kuishukuru Wizara ya Afya kwa kufikisha huduma za kibingwa kwa sababu itasaidia kupunguza changamoto ya matibabu kwa magonjwa mbalimbali.
Naye Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Getrude Naphtal amesema kambi hiyo ilizinduliwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu Mei 6, mwaka huu mkoani Iringa.
Amesema huduma za kibingwa zitatolewa kwenye kanda nane katika hospitali za wilaya 184 nchini na kila wilaya itafikiwa na madaktari bingwa na bobezi watano.
Mkazi wa Jijini Mbeya,Ester Damian amesema huduma hizo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa kipato duni ambao wanakosa huduma kutokana na kukosa fedha.