Maswali yalivyowavuruga wagombea Chadema | Mwananchi

Dar es Salaam. Usaili wa wagombea wa uenyekiti, umakamu na wahazini wa kanda nne za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ngoma nzito ndivyo unavyoweza kusema. Hii inatokana na mchakato kuchukua muda mrefu tofauti na matarajio ya wagombea na hofu ya watia nia kupenya.

Usaili huo hauna tofauti na uliofanyika jana Jumapili, Mei 12, 2024 wa nafasi za mabaraza ya chama hicho yakiwemo ya wazee, vijana na wanawake mchakato uliohitimishwa usiku huku usaili wa uenyekiti na umakamu ukiwekwa kiporo kutokana na ufinyu wa muda.

Lakini katika usaili unaongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe umeibua malalamiko kwa baadhi ya wagombea wakidai wanaulizwa maswali magumu au ya kukomoa ili wasipenye kwenye mchakato huo.

Watia nia hao ni kutoka kanda ya Serengeti yenye mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu, kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma), Nyasa (Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa) na Victoria (Mwanza, Kagera na Geita).

Baadhi ya watia nia wamesikika wakieleza hayo kwenye korido, viunga na bustani zilizopo pembezoni mwa makao makuu mapya ya ofisi ya chama hicho yaliyopo Mikocheni Dar es Salaam.

Hofu ya kutokupenya majina yao inatokana na kile kilichoelezwa na baadhi ya watia nia walioingia kufanyiwa usaili na kamati hiyo kuwa,  walikuwa wanaulizwa maswali magumu yaliyokuwa yanasababisha kuwatoa kwenye mstari wa kujiamini kuyajibu kwa ufasaha.

Mwananchi Digital lililoweka kambi na kufuatilia kwa ukaribu kikao hicho cha kamati kuu juu ya mchakato huo wa usaili ilishuhudia vikao vya makundi tofauti ya watia nia hao vilivyokuwa vikijadili na kubadilishana mawazo, kuhusu yaliyokuwa yanawakumba kwenye vikao hivyo kiasi cha kuwaacha njia panda.

“Niliulizwa yaliyokuwa yanajitokeza kwenye mkoa niliokuwa nafanya kazi, kwa nini sikusimamia mchakato wa Chadema Digital hadi ikasababisha nikakatwa kwenye nafasi niliyonayo.

“Nikajitetea katika majibu yangu lakini swali hili niliulizwa na kila mjumbe na mara mwisho aliniuliza Tundu Lissu ambaye kabla alikuwa ametoka nje. Ukiangalia ni maswali ya kiuchonganishi,” amesikika mmoja wa watia nia.

Mtia nyia huyo aliyekuwa akigombea nafasi ya uenyekiti kwenye moja ya kanda aliwaambia wenzake msingi wa kuulizwa swali hilo ni kutaka kujiridhisha kama aliyeenguliwa kwenye nafasi aliyokuwa akiishilia (katibu wa wilaya) itakuaje na matumaini na nafasi mpya anayoomba.

Mjumbe mwingine aliyeingia kwenye kikao hicho, amesema licha ya kuulizwa maswali magumu kulingana na kazi ya utendaji aliyokuwa akifanya, lakini hawakupewa fursa ya kutoa ushauri kwa yale wanavyoona kwenye maeneo yao.

Ajaza fomu kwa Kiingereza

Mtia nia mwingine wa nafasi ya uhazini amesikika akiwasimulia wagombea wenzake aliulizwa namna fomu yake alivyoijaza ilikuwa tofauti na wajumbe wengine (alijaza kwa lugha ya Kiingereza).

“Ni swali hilo tu na bahati isiyokuwa nzuri niliambiwa niongee Kiingereza sasa mimi nilikuwa sijui, sikupewa nafasi nyingine ya kuulizwa swali lingine,” amesema.

Mwananchi ilimfuata mjumbe huyo kujua inakuwaje fomu akaijaza kwa lugha ya Kiingereza asiweze kuzungumza katika majibu yake amesema anajua Kiingereza kuongea tofauti na kuandika.

“Kusema ukweli fomu sikujaza mwenyewe ila nilijaziwa na baadhi ya watu mwenyewe nilikuwa nimevurugwa na majukumu mengi ndiyo maana imetokea hivi sijui wataamuaje,” amesema.

Taarifa kutoka ndani ya vikao zinadai baada ya mgombea kutoka nje ya kikao wajumbe wa kamati kuu wanapiga kura papo hapo kama anapenya au la. Hali hiyo imekuwa ikiwapa hofu zaidi watia nia wanaokwenda au kuingia katika ukumbi wa mikutano kwa  ajili ya usaili wa nafasi wanazoziomba.

Alipoulizwa kuhusu kutoa fursa kwa watia nia kutoa ushauri kwa kamati kwa masilahi ya chama, Katibu Mkuu wa Chadema, John Manyika amesema katika kikao hicho wameitwa kuhojiwa na si kutoa ushauri.

“Lazima kieleweke hivyo, kikao kinalenga kuwahoji hivyo kama wanaulizwa maswali wanapaswa kujitetea kulingana na wanavyojibu na sisi tutapima,” amesema Mnyika

Majibu hayo yalikaziwa na Mkurugenzi Itifaki na Mawasiliano ya Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliyesema wajumbe wanaolalamika hawaijui katiba na wanapaswa kwenda kuisoma ili kuelewa.

“Katiba imefafanua haya yote kwenye namba 7 (5) ukiitwa kwenye kikao hiki unahojiwa na si kuja kutoa ushauri. Mjumbe anayelalamika tafsiri yake haijui katiba yetu inavyosema,” amesema.

Mrema amesema maswali hayo yalikuwa yamejikita maeneo mawili kwanza kama ulishika nafasi ya uongozi lazima mtia nia aulizwe kujua uadilifu na utendaji wake ulivyokuwa.

“Kama ulikuwa na makandokando lazima uulizwe lakini kwa wanaogombea mara ya kwanza wataulizwa namna wanavyokijua chama,” amesema Mrema.

Katika hatua nyingine, Mwananchi lilimuuliza tena Mnyika kuhusu uwezekano wa mkutano huo kutamatika katika majibu yake amesema:”Sijui ila tukimaliza tutawajuza kuweni na subira bado tunaendelea.”

Msingi wa swali hilo ni kutokana na idadi ya wagombea wa nafasi hizo na hadi jioni walikuwa hawajamaliza hata kanda mbili kati ya nne zinazofanya uchaguzi ambazo ni Serengeti, Victoria, Magharibi na Nyansa.

Kikao hicho cha kamati kuu kilianza Jumamosi ya Mei 11,2024 na kilikuwa kifanyike kwa siku tatu hadi leo Jumatatu, kisha maazimio kutolewa kwa umma na Mbowe. Hata hivyo, hadi saa 1 usiku wa leo Mei 13,2024, bado usaili unaendelea kwa kanda ya pili kati ya nne zinazopaswa kusailiwa.

Kikao hicho cha kamati kuu ndicho kitakachopanga ratiba ya mchakato wa uchaguzi wa kanda za nne za Chadema ambazo zinatekeleza jukumu hilo baada ya kumaliza uchaguzi katika ngazi ya chini hadi mkoa.

Related Posts