Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeidhinisha Sh102 bilioni ili kulipa fidia kwa wakazi wa Dar es Salaam ambao watalazimika kupisha ujenzi wa mradi waawamu ya nne na tano wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).
Hatua hiyo si tu upanuzi wa mradi ili kuboresha usafiri wa umma pekee bali unathibitisha kutambuliwa kwa umuhimu wa kuunga mkono jamii zilizoathiriwa wakati wa utekelezji wa mradi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Athuman Kihamia, akizungumza na gazeti Dada la The Citizen leo Jumatatu, Mei 13, 2024 amesema Serikali imeidhinisha bajeti ya Sh32 bilioni kwa fidia ya wakazi 229 wa Dar es Salaam watakaopisha mradi wa awamu ya nne wa BRT, na Sh70 bilioni kwa fidia ya wakazi walioathiriwa na awamu ya tano.
“Pesa imethibitishwa na Mkadiriaji wa Serikali na ombi limepelekwa kwa Wizara ya Fedha. Kwa BRT awamu ya nne, jumla ya Sh14 bilioni zitatolewa kwa wakazi 114 wa Mbuyuni, wakati Sh17 bilioni zitatolewa kwa wakazi 15 katika eneo la Mlalakuwa,” amesema.
Kihamia amesema:”Mara tu tutakapopokea fedha, tutaanza kuzitoa kwa watu waliopitiwa. Hii itawezesha mkandarasi kuchukua maeneo hayo na kuendelea na ujenzi wa BRT awamu ya nne.”
“Kwa kuwa ujenzi wa awamu hii tayari unaendelea, tunatumai kuwa fedha zitatolewa haraka iwezekanavyo ili kuepuka kucheleweshwa.”
Ujenzi wa BRT awamu ya nne utachukua miezi 14 ambapo ujenzi ulianza Novemba 1, 2023, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 2025.
Akifafanua kuhusu BRT awamu ya tano, Kihamia amesema Sh70 bilioni zitatolewa kwa baadhi ya wakazi katika mitaa 32 katika eneo la Kigogo roundabout na Segerea.
“Awamu ya nne ya BRT yenye urefu wa kilomita 30.4 ina vipande vitatu, cha kwanza kinaanza katika makutano ya Bibi Titi na Maktaba kinaendelea kupitia Barabara ya Ali Hassani Mwinyi hadi Bagamoyo hadi Mwenge na kisha inapita barabara ya Sam Nujoma hadi simu 2000.
Amesema kipande cha pili kinaanza kutoka Mwenge kupitia Bagamoyo hadi Dawasa, kipande cha tatu kinajumuisha upanuzi wa kituo cha Kivukoni na ujenzi wa vituo viwili simu 2000 na Mbuyuni.
Awamu ya tano ya BRT yenye urefu wa kilomita 25.7 inaanzia Ubungo Kijazi kupitia Barabara ya Nelson Mandela hadi Daraja la Nyerere.
Kisha inapita Segerea kupitia Barabara ya Tabata hadi kufikia Kigogo roundabout, matawi mengine yanatokea katika kliniki ya Chang’ombe kupitia Barabara ya Mbangala Kwa Azizi Ali.