Tchakei aibeba Singida kwa Prisons Ligi Kuu

Bao la kichwa la dakika ya 50 lililofungwa na kiungo mshambuliaji Marouf Tchakei limetosha kuihakikishia Ihefu SC ushindi muhimu ugenini dhidi ya Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Tchakei amefunga bao hilo akitumia krosi ndefu ya kiungo mwenzake, Duke Abuya  likiwa bao lake la kwanza tangu arejee akitokea katika majeruhi.

Matokeo hayo ya Ihefu ndani ya Uwanja wa Sokoine yanairudisha kwenye njia ya ushindi baada ya kulazimishwa sare nyumbani kwenye mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania.

Tchakei amefunga bao hilo la tisa kwake msimu huu akiifanya Ihefu kuruka mpaka nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi kutoka nafasi ya 12 iliyokuwepo awali ikifikisha pointi 32.

Singida ingeweza kutengeneza ushindi mkubwa zaidi kwenye mchezo huo kama wachezaji wake wangekuwa makini kufuatia kupoteza nafasi za wazi za kufunga.

Hata hivyo, Prisons nao dakika za mwisho wa kipindi cha pili ilikosa umakini kutulia na kutumia nafasi ilizotengeneza baada ya kuikomalia Ihefu kwa kuishambulia kwa nguvu.

Kipigo hicho bado hakijaibadilishia kitu kwani Prisons inaendelea kusalia katika nafasi ya tano na pointi 33 ikiendelea kuutafuta ushindi ambapo mara ya mwisho kushinda ilikuwa Machi 9, 2024 ilipoichapa Simba kwa mabao 2-1.

Prisons baada ya mechi ya leo imefikisha mechi nane kucheza bila ya kupata ushindi ikitoa sare mechi zake sita zilizopita kabla ya kupoteza leo.

Related Posts