MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umeitaka Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kufanya jitihada za kutafuta njia mbadala ya kurejesha mtandao (intaneti) katika hali yake ya kawaida, kwani kukosekana kwake ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Wito huo umetolewa leo Jumatatu na Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, ikiwa Tanzania inaingia siku ya pili huku wananchi wake wakikabiliwa na changamoto ya intanenti ambapo TCRA inasema tatizo hilo limesabishwa na hitilafu katika nyaya zinazopitisha huduma hiyo zilizoko baharini.
Katika hatua nyingine, Olengurumwa amesema athari wanazokutana nazo wananchi kwa kukosa intanenti hususan za kiuchumi kwa wanaofanya shughuli zao mtandaoni, ni sababu tosha kwa mamlaka kufahamu kwamba huduma hiyo ni ya msingi na ni haki ya binadamu hivyo haipaswi kukosekana.
“Nadhani mmeona wenyewe kwa nini siku zote tumekuwa tukisema kwamba mtandao yaani intaneti ni haki za binadamu, ni sawa na unapohitaji chakula na maji. Leo mmeona ni siku moja tu imetokea lakini madhara tunayopata ya kukosa intaneti ni makubwa,” amesema Olengurumwa na kuongeza:
“Ni wakati wa kujifunza kuona umuhimu wa kutosumbua mtandao wakati wote, tujifunze kupunguza gharama za intaneti sababu ndio kiunganishi cha uchumi wa jamii yetu.”