UN wakaribia mkataba wa kusitisha uharamia wa kibayolojia – DW – 13.05.2024

Mzunguko wa mwisho wa mazungumzo kuhusiana na mkataba mpya wa Umoja wa Mataifa kuhusu uharamia wa kibayolojia umeanza Jumatatu baada ya zaidi ya miaka 20 ya mazungumzo.

Lengo kuu la mazungumzo hayo ni kuukamilisha mkataba huo ifikiapo siku ya mwisho ya mkutano huo Mei 24.

Mkataba huo mpya unalenga kuzuia kile kinachoitwa uharamiawa kibayolojia ambao umeelezewa kama wizi wa raslimali za vinasaba au elimu ya kiasili na kuitumia elimu hiyo kibiashara kama vile kutengeneza madawa na bidhaa za kiafya. Mkataba huo mpya utapendekeza nchi asilia zinufaike na faida au zilipwe fidia.

Mkataba kuleta uwazi

Jumla ya wawakilishi 1,200 wa serikali tofauti duniani wanashiriki mkutano huo na mwakilishi wa Kenya ambaye hakutaka kutajwa jina amesema, mkataba huo utaleta haki.

Uswisi | Umoja wa Mataifa
Wajumbe katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa Ulaya, UswisiPicha: FABRICE COFFRINI/AFP/Getty Images

Rasimu ya mkataba huo inazitaka kampuni zioneshe ni lini zinapowasilisha ombi la haki miliki kuhusiana na chimbuko la bidhaa au elimu wanayotumia. Baada ya hapo, nchi zilizotoa elimu hiyo zinastahili kuhakikisha iwapo vibali vyote vinavyohitajika vipo na makubaliano yote yametiwa saini.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Haki Miliki Ulimwenguni, WIPO, linasema mkataba huo utaleta uwazi na ubora katika mfumo wa haki miliki na kuzuia haki hizo kutolewa kimakosa. Wanaopinga mkataba huo lakini wanahofia kwamba utakuwa kizingiti kwa ubunifu.

Mkuu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa Daren Tang, lakini, ametahadharisha kwamba mazungumzo hayatokuwa rahisi ingawa akasema vile vile kuwa, mataifa yanayoshiriki yako karibu sana kufikia makubaliano ya kihistoria.

Raslimali za vinasaba kama zile zinazopatikana katika mimea inayotumika kama dawa, mazao ya kilimo na aina tofauti za wanyama, haziwezi kulindwa kama mali za kimataifa ila ubunifu unaotokana nazo unaweza kupewa haki miliki.

Marekani na Japan zajitenga

Kwa hali ilivyo sasa hivi, si lazima kuchapisha chimbuko la ubunifu na nchi nyingi zinazokuwa kiuchumi, zinahofia kwamba haki miliki zinazotolewa ama zinazunguka haki za watu asili au zinatolewa kutokana na ubunifu wa sasa. Visa kama hivyo vinaweza kusababisha kesi zitakazodumu kwa muda mrefu mahakamani.

Ousman Belay, kijana mbunifu
Kijana mbunifu kutoka Ethiopia Ousman BelayPicha: Privat

Malumbano bado yanaendelea hasa kuhusiana na hatua ya kuwekwa vikwazo na masharti ya kufutilia mbali haki miliki.

Miaka miwili iliyopita, mataifa yalikubaliana kufanya mkutano wa kidiplomasia mwaka huu wa 2024 ili kufikia makubaliano kuhusiana na suala hilo. Marekani na Japan ndizo nchi pekee zilizojitenga na uamuzi huo wa kuitwa mkutano.

Ujumbe wa Japan mjini Geneva umeliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa, linatarajia kwamba yatakayojitokeza katika mkutano huo yatakuwa “wazi, yenye tija na yanayoweza kutumika vyema.”

Vyanzo: DPA/AFP

Related Posts