SASA ni rasmi kwamba Yanga ni bingwa mpya wa Ligi Kuu Bara baada ya jana kuwachapa Mtibwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Manungu Turiani Mkoani hapa.
Mabadiliko matatu yaliyofanywa na Yanga kipindi cha pili, yalitosha kubadili matokeo kwenye mchezo huo ambao Mtibwa ilikwenda mapumziko ikiongoza bao 1-0 ambalo liliwapa matumaini kwamba wangeweza kushinda na kuendeleza kampeni yao ya kujinasua mkiani.
Yanga imechukua ubingwa huo ikifikisha pointi 71 kileleni ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote iliyo chini yake ikipata wepesi huo baaada ya Simba kung’ang’aniwa ugenini juzi dhidi ya Kagera Sugar kwa sare ya bao 1-1. Sasa kilichobaki ni vita ya Simba na Azam kwenye nafasi ya pili kuwania kuungana na Yanga kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ubingwa huo wa Yanga ni wa tatu mfululizo lakini kihistoria ni taji la 30 kwa mabingwa hao wa kihistoria hapa nchini wakiendelea kutanua rekodi yao ya kibingwa.
Ushindi huo wa Yanga haukuja kirahisi kwani Mtibwa licha ya mapambano yao ya kujinasua isishuke daraja iliuanza mchezo huo kwa kasi ikitangulia kupata bao dakika ya 32 likifungwa na mshambuliaji Charles Ilamfya kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo wake Jimson Mwanuke na kufunga kirahisi kwa kichwa.
Kuingia kwa bao hilo Yanga ilikuja kwa kasi ikishambulia Mtibwa lakini mashambulizi yao yakakosa umakini kwenye kumalizia na timu hizo kwenda mapumziko huku wenyeji wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili Yanga ikarejea na mabadiliko ya kwanza ikimtoa kipa wake namba moja aliyeuanza mchezo huyo Djigui Diarra nafasi yake ikichukuliwa na Aboutwalib Mashery aliyesajiliwa na Yanga akitokea Mtibwa Sugar.
Dakika 15 baada ya kuanza kwa kipindi cha pili Yanga ikafanya mabadiliko mengine matatu kwa pamoja ikimtoa beki Lomalisa Mutambala, Maxi Nzengeli na Joseph Guede nafasi zao zikichukuliwa na Nickson Kibabage, Clement Mzize na Pacome Zouzoua.
Mabadiliko hayo yakaibeba Yanga na kuongeza kasi ya mashambulizi langoni kwa Mtibwa na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha likifungwa na mshambuliaji Kennedy Musonda.
Mtibwa ikajikuta inaitanguliza Yanga dakika ya 66 kufuatia beki wake Nasri Kombo kujifunga wakati akipambana kuokoa mpiora uliopigwa na Kibabage.
Yanga ikahitimisha ushindi wao kwa bao la Mzize dakika ya 81 akimalizia kirahisi pasi ya beki na nahodha wao Bakari Mwamnyeto.
Mtibwa licha ya kuonyesha kiu ya kutaka ushindi lakini kukosa utulivu kwenye kumalizia nafasi pamoja na yale ya safu yake ya ulinzi watayajutia kwenye mchezo huo baada ya kushindwa kuhimili presha ya Yanga.
Mabadiliko ya Yanga ya dakika ya 60 yaliifanya timu hiyo kuongeza kasi ya kutengeneza mashambulizi mtego ambao Mtibwa ilishindwa kuushtukia na kujikuta wanajichanganya wenyewe na kuwarahishia ushindi wageni.
Baada ya ushindi huo wachezaji wa Yanga wakiwa wamevalia fulana maalum za kusheherekea ubingwa wa 30 zilianza uwanjani hapo huku huku wakimwagiana shampeni wakiongozwa na Rais wa klabu yao Hersi Said huku mashabiki wao wakiwa na vaibu kubwa la ubingwa huo.
Ilikuwa ni furaha kubwa kwa wachezaji wa Yanga wakimbeba juu ya mabega kwa shangwe kocha wao Miguel Gamondi ambaye alitwaa taji la kwanza ndani ya klabu hiyo tangu aichukue timu hiyo kutoka kwa mtangulizi wake Nasreddine Nabi.
Wakati Yanga wakiwa wanafuraha baadhi ya wachezaji wa Mtibwa wao hawakuwa na nguvu hata ya kutembea wakibaki kiwanjani wakitafakari namna timu yao inavyozidi kujikusanyia pointi za kushuka daraja ikibaki mkiani mwisho wa msimamo wa ligi na pointi zao 20.
Baada ya kutoka uwanja wa Manungu msafara wa mashabiki wa Yanga wakiwa na furaha kubwa ulianza wakiwa kwenye msafara wa magari na wengine wakisimama barabarani wakishangilia ubingwa huo waliouchukua mapema kabla ya ligi kumalizika wakibakiza mechi tatu.