Dodoma Jiji dakika 270 bila bao ikitoka suluhu na Namungo

DODOMA Jiji FC, imetoka suluhu na Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Mchezo huo ulizikutanisha timu zote ambazo zinapambana kukimbia kwenye hatari ya kushuka daraja kwani kabla ya kushuka dimbani, Namungo ilikuwa ya 10 ikikusanya pointi 30 baada ya mechi 26, wakati Dodoma Jiji ya 12 na pointi zake 29 ikishuka dimbani mara 25.

Katika mchezo wa leo uliokuwa na mashambuliz ya kupokezana, imeshuhudiwa Dodoma Jiji ambao ni wenyeji wakikamilisha jumla ya dakika 270 sawa na mechi tatu mfululizo bila ya kufunga bao.

Dodoma Jiji ambayo baada ya leo imebakiwa na michezo minne kukamilisha msimu huu, mechi tatu zilizopita ambazo haikufunga bao ilikuwa hivi; Singida Fountain Gate 2-0 Dodoma Jiji, Dodoma Jiji 0-0 Tanzania Prisons na Dodoma Jiji 0-0 Namungo.

Suluhu hiyo imeifanya Dodoma Jiji kupanda nafasi moja hadi ya 11 ikifikisha pointi 30 baada ya mechi 26 ikiwa pointi sawa na Singida Fountain Gate tofauti yao ni mabao ya kufunga ba kufungwa.

Katika mechi nne zilizosalia ambazo Dodoma Jiji inapaswa kuzipiga vizuri hesabu zao ili kuepuka kushuka daraja itacheza dhidi ya Simba na Yanga ambazo itakuwa nyumbani, baada ya hapo itaenda ugenini kupambana na Ihefu na Mashujaa.

Namungo yenyewe suluhu imeipandisha nafasi mbili kutoka 10 hadi 8 baada ya kufikisha pointi 31 sawa na JKT Tanzania na Kagera Sugar huku tofauti yao ni mabao ya kufunga na kufungwa.

Namungo mechi tatu zilizobaki ni dhidi ya Mtibwa Sugar ugenini kisha itamalizia nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons na Tabora United.

Timu hizo zote bado hazina uhakika wa kusalia Ligi Kuu kwa msimu ujao kutokana na namna msimamo ulivyo.

Hadi sasa ambapo Yanga ndiyo bingwa wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani kwa mechi zilizosalia, kule chini haijafahamika ni timu gani imeshuka daraja jambo linalowapa wasiwasi waliopo kuanzia nafasi ya mwisho 16 hadi ya tano.

Hiyo inatokana na mechi zilizobaki na namna timu zilivyopishana pointi chache kwani yeyote kati ya hao akizichanga vizuri karata zake atakuwa sehemu salama.

Coastal Union ambayo hivi sasa inapambana imalize nafasi ya nne katika ligi ambapo ndiyo inaishikilia kwa sasa na pointi zake 38, ikitokea imepoteza mechi tatu zilizobaki haiwezi kuangukia kwenye hatari ya kushuka daraja moja kwa moja wala kucheza play off, hivyo ipo salama sambambana zile tatu za juu, Simba, Azam na mabingwa Yanga.

Kuanzia nafasi ya tano, Tanzania Prisons hadi ya 16 inayoshikiliwa na Mtibwa Sugar, lolote linaweza kutokea mwisho wa msimu.

Ikumbukwe kwamba, timu mbili za chini zitashuka daraja moja kwa moja, huku zitakazoshika nafasi ya 13 na 14 zitalazimika kucheza kwanza zenyewe play off, mshindi atabaki ligi kuu, wakati yule atakayepoteza akicheza play off nyingine na timu moja ya Championship ambayo nayo itakuwa imeshinda mchezo wa play off kuwania kupanda daraja. Mshindi wa jumla hapo ndiye atakayecheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Kutokana na msimamo ulivyo sasa, Mtibwa Sugar iliyopo mkiani, hesabu zake zinambana zaidi kwani akifanikiwa kushinda mechi tatu zilizobaki huku wa juu yake wakiteleza wote, basi atamaliza na pointi 29 ambazo zitamuweka kwenye kundi la kucheza play off kupambania kubaki ligi kuu.

Geita Gold inayoshika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 25, endapo ikishinda mechi tatu zilizobaki itafikisha 34, pointi ambazo ukiangalia msimamo timu iliyopo nafasi ya tano, Tanzania Prisons haijazifikia kwani inazo 33, hivyo kipindi hiki ligi inapoelekea ukingoni, timu hizo zote hazipo salama.

Related Posts