Gamondi apiga marufuku shamrashamra kambini

KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi amecharuka na kupiga marufuku shamshamra za ubingwa huku akitoa masharti mapya ya kufuatwa ili kufikia malengo ya klabu.

Gamondi amewasisitiza mastaa na viongozi wasahau kabisa kwamba wameshatwaa taji hilo la tatu mfululizo kwani wakizembea kidogo wanatoka kwenye mstari na watatoa faida kwa wengine.

Yanga ilibeba ubingwa baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 3-1 jioni. Ghafla Gamondi akawaita viongozi na kuwasisitiza usiku huohuo timu irudi Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa viongozi wa Yanga, Gamondi aliwaambia kwamba timu ingerudi mjini jana Jumanne mchana, ingekutana na maelfu ya mashabiki barabarani jambo ambalo lingewatoa wachezaji kwenye programu zake na itawachosha na kuwasahaulisha mtihani mkubwa wa nusu fainali ya FA dhidi ya Ihefu uliopo mbele yao.

Mei 19 mwaka huu Yanga itakutana na Ihefu pale Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kwenye nusu Fainali ya pili ya Kombe la FA ambapo mshindi wa mechi hiyo atakutana na mshindi wa Nusu Fainali ya kwanza kati ya Coastal Union dhidi ya Azam itakayopigwa Mei 18 Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo ameliambia Mwanaspoti kuwa baada ya uamuzi wa kocha wao haraka kikosi kilirejea jijini Dar es Salaam usiku wa juzi Jumatatu muda mfupi baada ya mchezo kumalizika ambapo leo kitaingia kazini kuanza maandalizi ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).

Gumbo alisema sio wao kambini tu hata mashabiki na wanachama wao wanapaswa kuahirisha kwa muda tambo za ubingwa na waanze kujipanga na mchezo huo ambao utawapa nafasi ya kwenda kucheza fainali ya tatu mfululizo ya michuano hiyo.

“Hakuna nafasi ya kuendelea na sherehe kwani bado operesheni makombe inaendelea na akili ambayo imetoka kwa kocha wetu tunataka hata mashabiki wetu washtuke na kuanza kujipanga na mchezo wa nusu fainali na baadaye fainali,” alisema Gumbo ambaye tangu aongoze kamati hiyo ameweka kabatini makombe saba.

“Yanga inayataka haya makombe makubwa yaliyosalia na akili yetu sasa ni hii nusu fainali,” alisema.
“Tunafahamu utakuwa mchezo mgumu ndio maana hatukutaka kujipa ugumu kama ambao tulifanya huko nyuma wakati tumechukua ubingwa na baadaye kwenda kucheza fainali ngumu dhidi ya Coastal Union.”

Gumbo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga alisema watakapokamilisha operesheni ya makombe hayo watakuwa na sherehe kubwa za makombe mara baada ya kufunga msimu.

“Tumechukua ubingwa wa 30 msimu huu na tukimaliza kuchukua kombe la pili tutakuwa na sherehe kubwa zaidi za ubingwa ambazo hapo wanachama na mashabiki wetu watajumuika na timu yao lakini kwa sasa tuhamishe akili zetu huko Arusha.”

Related Posts