Dar es Salaam. Wakati Tanzania inaungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia, taasisi hiyo imeendelea kukabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo migogoro ya ndoa, malezi duni na ongezeko la watoto wa mitaani.
Changamoto hizi zimechochea mmomonyoko wa maadili miongoni mwa watoto na vitendo vyenye athari ikiwamo kujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo, vinavyosababisha ongezeko la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwa kundi la watoto na vijana balehe.
Siku hii ambayo huadhimishwa Mei 15 duniani kote mwaka huu imebebwa na kauli mbiu: “Tukubali Tofauti Zetu kwenye Familia; Kuimarisha Malezi ya Watoto’’.
Kauli mbiu hiyo inaakisi hali inayoendelea sasa kwa familia nyingi kuvurugika kutokana na migogoro kati ya wenza, hali inayosababisha wengi kutengana na kuwaacha watoto kwenye mtanziko.
Ripoti ya utafiti uliofanywa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), inaonesha kuna ongezeko kubwa la kuvunjika kwa ndoa hasa za vijana.
Matokeo ya utafiti huo yameonesha asilimia 70 ya ndoa zinazovunjika sababu yake ni wanandoa kukosa elimu ya ndoa.
Sababu nyingine ni mmomonyoko wa maadili asilimia tisa, kukosekana uadilifu katika ndoa asilimia nane, tatizo la afya ya akili asilimia saba na sababu nyingine ikiwemo matumizi ya simu.
Mshauri wa masuala ya malezi na familia, Mchungaji Richard Hananja, anasema wazazi wanapaswa kuitumia siku hii kutafakari jukumu lao katika kuhakikisha familia inasimama imara.
“Ili familia iwe imara ni lazima wazazi wawe katika msingi mzuri wa malezi, jambo linaloonekana kulegalega kwa sasa. Wazazi hawana muda wa kuwapandikiza watoto vitu vizuri na tabia njema matokeo yake tunashuhudia watoto wamejaza uchungu moyoni.
“Mzazi anayelea mtoto vizuri ni yule anayepata muda wa kumpandikiza vitu vizuri na kumkataza mabaya. Ni muhimu kutenga muda wa kuzungumza na watoto na kukaa pamoja kama familia hapa ndipo upendo unapandikizwa,”anasema Hananja.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka anasema familia ni jiwe la msingi katika ujenzi wa jamii, hivyo ni muhimu kuwepo umakini mkubwa katika utengenezaji wa taasisi hiyo muhimu.
Anasema hata hivyo miaka ya karibuni, taasisi hiyo imekumbwa na misukosuko kadhaa kutokana na kukosekana malezi imara ikiwa ni matokeo ya wajenzi wa familia hizo kukosa malezi bora.
“Familia bora huzaa jamii bora, changamoto tuliyonayo sasa wanaotegemewa kutengeneza familia hawana malezi bora, hivyo ni vigumu kwa wao kutengeneza familia bora matokeo yake ndiyo haya tunayoyaona sasa.Unapotaka kuanzisha familia ni lazima uanzie kwenye kuchagua mtu unayekwenda naye kuanzisha hiyo familia.
“Ni muhimu awe baba au mama mwenye sifa za ulezi na kwa pamoja mkaunganishe nguvu kwenye kulea watoto ila siku hizi watu hawaangalii hilo wanachojali ni matamanio yao,” anasema.
Sheikh Mataka anasema kinachotakiwa kufanywa kwenye taasisi ya familia, ni kulea na sio kufuga kama inavyofanywa na wazazi wengi wa sasa.
“Kuhakikisha mtoto amekula au amelala sio malezi, ni lazima mtoto alelewe kiroho na apewe maadili, kwa sasa tuna wazazi ambao wenyewe wamekosa malezi tusitegemee kama wataweza kutoa malezi mazuri kama hatutaamua jamii kuwekeza kwenye malezi,” anasema.
Nafasi ya mzazi kwa watoto
Mwanasaikolojia, Jacob Kilimba anasema migogoro ya wazazi ina athari za moja kwa moja kwa watoto, kwa sababu taswira ya kwanza ya mtoto ipo kwa mzazi au mlezi wake kwa kuwa ndiye mtu wa kwanza aliyemuona au kukutana naye katika maisha yake yake.
“Mtoto anamchukulia mzazi kama Mungu wake hapa duniani. Ujasiri na hali ya kujiamini aliyonayo mtoto inaanzia kwa aina ya mzazi aliyemlea. Hii imani inakuja kupungua baadaye akishafikia umri wa balehe hivyo kabla ya hapo hakuna mtu mwingine anaweza kumuamini zaidi ya mzazi.
“Kunapokuwa na migogoro ya wazazi, mtoto anaathirika kwa kiasi kikubwa. Kitendo cha kuona mzazi wake mmoja analia, mwingine anafoka au anaondoka anaanza kuona kuna tatizo.
Sasa inamuwekea kwenye mkanganyiko na mara nyingi wazazi wanapogombana kila mmoja anamlaumu mwenzake. hapo ndipo mtoto anaposhindwa kumuelewa amuamini nani,” anasema.
Kilimba anaongeza:“Wapo wazazi wanaoenda mbali zaidi.Unakuta anamwambia mtoto kwamba baba yako mbaya au mama yako mbaya, hii inampa wakati mgumu mno mtoto na inamuondolea ile imani aliyonayo kwa wazazi wake.”
Mwanasaikolojia huyo amefafanua kuwa mtoto akianza kupoteza imani kwa wazazi au mzazi wake anaanza kujiona hana thamani, hivyo anatafuta njia ya kujitenga na hilo linaweza kumsukuma kufanya maamuzi magumu ikiwemo kutoroka nyumbani, kujidhuru au hata kujiua.
Kuna hoja ya umuhimu wa vikao katika familia kama inavyoelezwa na mtaalamu wa malezi ambaye pia ni mkurugenzi wa taasisi ya Maadili Centre, Florentine Senya, anayesema ni familia chache zenye utaratibu wa kukutana na kuzungumza jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili.
Anasema kutokana na maendeleo ya teknolojia, kinachofanyika kwa sasa kwenye familia nyingi ni kupeana taarifa, lakini sio muda wa kukaa kwa pamoja na kujadili mambo ya pamoja.
“Siku hizi watu wa familia moja wanafungua makundi sogozi na kupeana taarifa, hivyo inaweza kutokea hata mwaka mzima hawajakaa pamoja na kuzungumza. Wasichojua wengi ni kwamba vikao vinasaidia kuongeza mshikamano baina ya wanafamilia…
“Mambo ya kuzungumza kwenye simu upo uwezekano hujui unayezungumza naye yupo katika hali gani anapitia yapi au huenda ameshaharibikiwa kimaisha. Mnapokutana inatoa nafasi ya kushauriana, kuonyana inapobidi na kusaidia pale inapohitajika kufanyika hivyo. Kingine pamoja na maendeleo ya teknolojia nafasi ya wazazi kukutana na watoto wao bado inahitajika na ni msingi imara wa familia,” anasema Senya.
Mbali na hilo anasema kuna watu kwao ni rahisi kutafuta msaada kwa marafiki au watu wengine wa mbali kuliko ndugu au mwanafamilia mwenzie.
“Hili linaweza kusababishwa na mfumo wa maisha wa sasa, ambao kila mtu anapambana na hali yake au hata tabia ambayo imejijenga kwa mtu kutotaka kuzungumza na wanafamilia wake.”
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Sebastian Kitiku anasema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili 2024 jumla ya familia 14,600 zilitoa taarifa ofisi za ustawi wa jamii kuwa na migogoro katika ndoa na uhusiano wa wenza.
Kwa mujibu wa Kitiku, mifumo kandamizi inayoendelea katika jamii inayochochewa na mila na desturi za baadhi ya makabila hapa nchini, imesababisha wanandoa hasa wanawake kukaa kimya bila kujadiliana na kumaliza tofauti zao.
Sababu nyingine alizozitaja ni maendeleo ya Tehama, mwingiliano wa mila na desturi za mataifa mbalimbali vimechochea taasisi ya familia kupata athari hasi.
“Mabadiliko hayo yamekuja na baadhi ya changamoto ambazo zina athari katika malezi na matunzo ya watoto katika familia. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na wazazi au walezi kukosa muda wa kutosha wa malezi.
“Watoto wengi hawapati mahitaji yao ya msingi lishe bora, huduma za afya, elimu changamoto nyingine ni kukosekana kwa muunganiko kati ya wazazi au walezi na watoto.
Anasema wazazi kukosa muda na watoto wao kumechangia kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kimwili, kingono na kihisia huku kukiwa na aina mpya ya ukatili wanayopitia watoto katika mitandao ya kijamii.
Taarifa ya Hali ya Ukatili wa Watoto Mtandaoni ya 2022, inaonesha watoto 67 katika 100 wenye umri wa miaka 12 – 17, wanatumia bidhaa za mawasilisano ikiwa pamoja na simu janja, kompyuta na runinga zenye intaneti.
Utafiti huo unaonesha watoto wanne katika 100 waliotumia mitandao, walifanyiwa aina mojawapo ya ukatili mtandaoni ikiwemo kulazimishwa kujihusisha na vitendo vya ngono.
Pia, kusambaza picha na video zenye maudhui ya kingono bila ridhaa yao na kurubuniwa kujihusisha na shughuli za kingono kwa kuahidiwa fedha au zawadi zingine.
Kitiku anasema athari ya hilo ni watoto kutumbukia kwenye vitendo vya ngono akieleza kuna wimbi kubwa la watoto chini ya miaka 18 kufanya mapenzi tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Watoto na kundi la vijana balehe wameingizwa kwenye uhalifu, ujambazi na usafirishaji haramu wa binadamu na dawa za kulevya.
Utafiti umebainisha kuwa simu na vifaa vingine vya kielektroniki wanavyotumia watoto hupatiwa na wazazi na ndugu wa karibu, bila kujua madhara wanayokumbana nayo watoto bila kusimamiwa matumizi yake.
Akizungumzia kauli mbiu ya maadhimisho hayo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, anasema inakumbusha umuhimu wa kumaliza tofauti za wazazi katika familia ili kutoathiri malezi na makuzi ya watoto.
“Inatukumbusha wazazi au walezi kuwa jukumu lao la msingi ni malezi, ikiwa pamoja na kumpatia mtoto mahitaji yake ya msingi, kumlinda dhidi ya ukatili, kuwasiliana na mtoto mara kwa mara ili kufahamu changamoto zinazomkabili na maendeleo yake kwa ujumla. Inatukumbusha wazazi wajibu wa kudumisha upendo na amani katika familia zetu,’ anasema.
ili kuzuia migogoro isiyo ya lazima inayoweza kusababisha watoto kukosa huduma muhimu za malezi na makuzi yao,” anasema.
Waziri huyo anabainisha ukatili dhidi ya watoto na ukatili wa kijinsia katika familia umechangia kuongezeka kwa migogoro ya kifamilia hususan kati ya wenza au wanandoa jambo lenye athari kubwa katika malezi na ustawi wa watoto wa familia na jamii kwa ujumla.
Mbali na migogoro kuchangia kuivuruga taasisi ya familia, hali ya kiuchumi nayo imetajwa kusababisha upweke kwa baadhi ya wanafamilia hasa zile ambazo zina watoto wakubwa ambao huwaacha wazazi wao au kumcjukua mzazi mmoja.
Dk Dorothy anasema wizara yake imeendelea kuratibu huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia kupitia Baraza la Usuluhishi wa Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii lililopo Makao Makuu ya Wizara, Mabaraza ya Kata na Mabaraza ya Jumuiya.
Katika taarifa yake aliyoitoa mwanzoni mwa mwezi huu Dk Dorothy alieleza kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 jumla ya mashauri 14,600 yalishughulikiwa, yaliyohusu migogoro ya ndoa yalikuwa 5,306 (36%), yaliyohusu migogoro ya kifamilia na matunzo ya watoto 5,944 (41%), yaliyohusu matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa yalikuwa 3,350 (23%).
Aidha, mashauri 3,411 yalifikishwa kwa maofisa Ustawi wa Jamii ambapo 1,642 yalipatiwa ufumbuzi na 443 yanaendelea kufanyiwa kazi.
Mashauri 1,326 yalipewa rufaa kwenda kwenye vyombo mbalimbali vya usuluhishi ikiwamo Mahakama (921) na mabaraza ya kata na jumuiya (405).
Kwa upande wake Kitiku amesema ili taasisi ya familia iwe salama ni muhimu kwa wazazi kutokuwa na migogoro na wote kwa pamoja washirikiane kuimarisha malezi na usalama wa watoto.
Mzee mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe anaeleza jinsi maisha ya uzeeni yanavyokuwa ya upweke haswa pale watoto wanapoamua kumchukua mama yao ili waishi naye huko waliko.
Mzee huyu ambaye watoto wake wanaishi nje ya nchi waliamua kumchukua mama yao na kuishi naye huko waliko na kumuacha mzee huyu akiishi na wafanyakazi.
Anaeleza kuwa watoto walipomwambia aende huko alikataa kwa kuwa anataka kuishi maisha yaliyo huru na kujiamulia anachomkitaka hivyo akaamua kubaki nchini.
“Ukienda huko nje utakuwa hauko huru lakini kama unavyojua nyie watoto mnaegemea kwa mama zenu sana bila kuangalia madhara yake. Mimi niko hapa huyo kijakazi wangu ana mtoto namuona kama mjukuu wangu tunaishi lakini upweke unakuwepo sana kwa kuwa mwenza wangu amechukuliwa.”
Mstaafu mwingine ambaye aliwahi kufanya kazi nje ya nchi akiwa na mkewe anasema aliporudi nchini mkewe alibaki huko nje akiendelea na kazi na hadi sasa hajarudi hivyo maisha yanaendelea lakini ni tofauti kwa kuwa sasa amestaafu na jumba ni kubwa watoto hawapo, mama hayupo hivyo ni upweke mtupu hata kama hela zipo za kutosha benki.
Akizungumzia hilo mwanasaikolojia Kilimba alisema kisaikolojia ni vigumu kwa mwanaume kuishi chini ya uangalizi wa mtu mwingine.
“Mwanamume ndani yake kuna hisia kwamba yeye ndiye mkuu, ndiye anapaswa kutengeneza familia sasa kulazimisha umchukue au unapomchukulia mke wake ni kama unamshusha thamani yake ndiyo maana anaona ni heri achague upweke kuliko kujishusha.
“Hapa ushauri kwa watoto kama unajiona una kipato kikubwa ni heri uwapatie wazazi wako ili waendelee kuwa pamoja lakini usiwe sehemu ya kuwatenganisha kwa sababu unawatengenezea upweke,” anasema.