Morogoro. Mradi wa ufungaji kamera maalumu za usalama kwa ajili ya kunasa matukio (CCTV) pembezoni mwa barabara ya Tanzania –Zambia, unatarajia kuanza siku yoyote.
Kamera hizo zitakazofungwa katika kipande cha barabara yenye urefu wa kilomita 50 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, zinalenga kudhibiti matukio ya mauaji ya wanyamapori ndani ya hifadhi hiyo.
Akizungumza leo Jumanne Mei 14, 2024 na waandishi wa habari waliotembelea Hifadhi ya Mikumi, Ofisa uhifadhi mkuu wa hifadhi hiyo, David Kadomo amesema kuna matukio mengi ya wanyamapori kugongwa katika barabara hiyo inayokatiza kwenye hifadhi kutokana na madereva kuendesha magari kwa mwendo kasi.
“Tayari upembuzi yakinifu umeshafanyika na kutambua gharama za mradi na kinachosubiriwa ni fedha tu kwa ajili ufungaji wa kamera zenyewe,” amesema Kadomo.
“Kukamilika kwa mradi wa uwekaji kamera utasaidia kupunguza kama sio kumaliza kabisa mauaji ya wanyama barabarani, madereva watafuata sheria na watakuwa makini zaidi kwa sababu sasa wanajua watakuwa wanafuatiliwa na kukamatwa,” amesema Kadomo.
Hawa Msimbe kutoka Kijiji cha Kikwazara amesema uwekaji wa taa hizo sio kusaidia tu wanyama, bali utasaidia pia binadamu ambao hugongwa na malori katika barabara hiyo na kisha kukimbia.
Hivyo, ameiomba Serikali iharakishe kuzifunga ili kuokoa maisha ya watu na wanyama pori hao.