Kisa Wydad, Ayoub aandaliwa miaka miwili Simba

UBORA aliouonyesha kipa wa Simba, Ayoub Lakred kwenye mechi alizocheza tangu atue umewakuna vigogo wa timu hiyo ambao wamepanga kumpa mkataba mpya utakaomfanya abaki kwa miaka miwili na kuzuia dili la kujiunga na Wydad Casablanca ya nchini kwao.

Ayoub alitua Simba mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea katika Klabu ya FAR Rabat ya Morocco baada ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu timu hiyo ambayo kwa sasa inanolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Nassredine Nabi.

Wakati mkataba wa Ayoub ukikaribia ukingoni, Simba imeshtuka kipa huyo aliyewahi kupita RS Berkane kuwa ana ofa zaidi ya tatu mezani kwake ikiwemo ya Wydad na fasta imeanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya wa miaka miwili.

Tayari Simba imemvuta wakala wa Ayoub jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo ya mkataba mpya na inaelezwa kwamba mazungumzo yanakwenda vizuri na kwamba muda wowote atasaini mkataba mpya mnono.

“Tukimuacha Ayoub tutapata wapi kipa mwingine wa daraja lake? Ni kweli tumeanzisha mazungumzo na upande wake na tunaelekea kufika mwisho. Huenda ukawa mkataba wa kihistoria kwa Simba katika upande wa Kipa. Ataishi Kifalme kwani ni mkataba mnono kwake,” kimeeleza chazo chetu kutoka ndani ya Simba.

Mwanaspoti imepenyezewa miongoni mwa vitu vitakavyomfanya Ayoub kuishi kifalme Simba ni pamoja na kupewa nyumba kali ya kuishi yeye na familia yake, sambamba na kupewa gari kali atakayoitumia kwenda na kurudi mazoezini sambamba na kwenye misele yake.

Hivi karibuni kamera za Mwanaspoti zilimnasa Ayoub akiwa na mkewe katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye mechi ya ligi ambayo kipa huyo aliingoza Simba kushinda 3-0 mbele ya Azam na inaelezwa huo ni mwanzo wa familia ya nyanda huyo kuhamia Bongo.

Mke wa Ayoub atakuwa Bongo hadi mwisho wa msimu huu akiangalia mazingira na kama ataridhika, basi atakuwa na sababu ya kusaini Simba na msimu ujao familia yake itahamia nchini.

Usajili wa Ayoub ulikuwa wa ghafla Simba kwani tayari ilikuwa imesajili kipa Mbrazili Jefferson Luiz ambaye aliishia Uturuki kwenye kambi ya maandalizi ya msimu huu (pre season) baada ya kupata majeraha.

Hata hivyo, Simba ilikuwa kama inabahatisha kwa Ayoub kwa kuwa wakati anatua alisajiliwa kipa mwingine Hussein Abel kutoka KMC aliyeungana na Ally Salim, Ahmed Feruzi na Aishi Manula aliyekuwa na majeraha na kufikisha makipa watano.

Ayoub hakuanza vyema maisha ndani ya Simba licha ya kipa namba moja wa muda mwingi kikosini hapo Manula kuwa majeraha, nafasi kubwa ya kucheza alikuwa akipewa Ally Salim lakini baadae Mmorocco huyo alipindua meza na sasa ndiye kipa namba moja wa Simba huku Manula akiendelea kuuguza majeraha.

Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally amethibitisha kuwepo mazungumzo ya kuwaongezea mikataba wachezaji wa chama hilo akiwemo Ayoub na kusisitiza kila anayetakiwa na timu hiyo atabaki.

“Nikuhakikishie kila mchezaji tunayemtaka Simba atabaki, lakini pia tutafanya maamuzi magumu kuachana na ambao tutaona wanastahili kuondoka. Mazungumzo yameanza na kila kitu tutawatangazia kitakapokamilika,” amesema Ahmed Ally.

Tangu ametua Simba, Ayoub amecheza mechi  14 za ligi kwa dakika 1260 na kuondoka na ‘clean sheets’ nane akiruhusu mabao 10.

Ukiachana na Ayoub, Simba tayari imemuongeza mkataba wa miaka miwili kiungo mshambuliaji, Kibu Denis aliyekuwa akiwindwa kwa karibu na wapinzani wao, Yanga.

Related Posts