Dar es Salaam. Huenda athari zaidi za kukosekana kwa huduma ya mtandao wa intaneti, zikaendelea kuonekana kutokana na mazingira yanayoonyesha huenda tatizo hilo likachukua zaidi ya siku 10 tangu lilipoanza.
Tatizo la kukosekana kwa mtandao huo, zilianza asubuhi ya Mei 12, mwaka huu baada ya kukatika kwa mkongo wa mawasiliano baharini wa SEACOM na EASSy kati ya nchi ya Msumbiji na Afrika Kusini.
Tatizo hilo la kukosekana mtandao au upatikanaji wa kiwango cha chini wa huduma hiyo, umeathiri zaidi nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda. Miongoni mwa walioathiriwa ni wafanyabiashara wanaotegemea mtandao na hata vyombo vya habari.
Pia, mikutano ya mitandaoni baadhi wamekuwa wakishindwa kushiriki, kujaza maombi ya ajira mitandaoni nazo ni sehemu ya kadhia inayoendelea kuwatesa wananchi na huenda hadi mtandao utakapokuwa umekaa sawa, baadhi ya ajira muda wake wa kutuma maombi ukawa umekwishapita.
Vyanzo mbalimbali vya taarifa mtandaoni, vinaonyesha ukarabati wa mkongo wa chini ya bahari unaweza kuchukua kuanzia siku sita hadi wiki nane kulingana na ukubwa wa tatizo.
Kuhusu lini changamoto hiyo itafika mwisho, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari, alisema ni vigumu kutamka ni lini hali ya mawasiliano itarejea kama kawaida, isipokuwa jitihada zinaendelea ili kuhakikisha mambo yanakuwa mazuri.
“Kila mtoa huduma anaendelea kupambana kuhakikisha anapata kiunganisho mbadala. Hata jana (juzi) kuna ambao walikuwa wamekwisha anza kurejesha huduma, hali itaendelea kuimarika kadiri wanavyopata link (kiunganisho),” amesema Dk Bakari.
Hata hivyo, amesema kuna wawekezaji wapo mbioni kuanza kutoa huduma nchini, ikiwemo kampuni ya 2Africa ambayo inatajwa kuwa mbioni kuanza huduma nchini.
Akizungumzia suala hili katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Mkuu wa ufundi wa kampuni ya Tigo, Emmanuel Mallya amesema kabla ya kukatika kwa mkongo huo, kuna mkongo mwingine wa SEACOM wa kwenda Kaskazini ulikatika kuanzia Februari mwaka huu na bado haujaweza kupata suluhisho, ndiyo maana tatizo limekuwa kubwa.
Mallya alisema kwa sababu Tigo ni mbia wa EASSy, hitilafu ilipotokea kati ya Msumbiji na Afrika Kusini, wao waliendelea kutumia mkongo wa kuelekea kaskazini katika njia ya EASSy na hivyo kuendelea kutoa huduma bila matatizo kwa wananchi.
“Sisi pekee ndiyo tumekuwa na ustahimilivu wa huduma tangu kuanza kwa tatizo hili, kama jana (juzi) tulielekea kwenye hali yetu ya kawaida, lakini kwa kuwa tunatumia link moja wakati wa jioni matumizi yakiwa makubwa tunarudi nyuma tena,” amesema.
Amesema Tigo wanaendelea kuangalia namna bora na wanawasiliana na wabia wengine ili kuhakikisha huduma zao zinarudi kama ilivyokuwa awali, huku akisisitiza ufumbuzi wa kudumu ni kuwa na watoa huduma wa mkongo wengi zaidi.
“Ukiachilia mbali changamoto kama hizi za kukatika, lakini mkongo ni mzuri kwa intaneti kuliko hata satelaiti, kwani unaweza kupitisha kiwango kikubwa cha data na gharama zake za huduma ni nafuu, hivyo wengi wanaweza kuimudu,” amesema Mallya.
Mmoja wa watoa huduma za mtandao, ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema kwa ratiba waliyonayo urekebishaji wa nyaya hizo zinazoelekea Afrika Kusini utakamilika Mei 23, mwaka huu.
“Tunafuatilia kwa karibu sana kwa wamiliki wa nyaya hizo ili kuhakikisha huduma zinarudi kama kawaida, mpaka sasa tumepata ratiba ya kutengeneza hizo nyaya kwa uelekeo wa Afrika Kusini, mpaka Mei 23, 2024, kila kitu kitakuwa tayari katika uelekeo wa Afrika Kusini,” amesema.
Wakati changamoto hiyo ikiendelea, watoa huduma za simu na zile zinazotegemea mtandao wa intaneti, wameendelea kutuma ujumbe wa kuomba radhi wateja wao kufuatia usumbufu wanaokutana nao katika shughuli zao za kila siku.
“Ndugu mteja tunapenda kukutaarifu kwamba huduma za intaneti zinaendelea kurejea katika hali ya ubora wa kawaida, jitihada zinafanyika kurudisha huduma katika ubora. Ahsante kwa uvumilivu wako,” ni ujumbe kutoka mtandao wa Airtel.
Upande wa benki nako kilio kikubwa kimekuwa kwa mawakala ambao sasa wanashindwa kufanya baadhi ya huduma, ikiwemo za malipo ya Serikali.
Hali hiyo imefanya baadhi hata kukosa hamu ya kufanya miamala na pindi wanapojua unataka kulipia huduma fulani watakueleza kuwa huduma hiyo haipatikani.
“Huduma kama za kulipia faini, sijui maji, tozo mbalimbali zinasumbua, labda ujaribu mara mbili mara tatu,” amesema Mwajuma Mzee, wakala wa huduma za kifedha eneo la Tabata, Dar es Salaam.
Dickson Mapunda, ambaye ni wakala katika eneo la Mtoni Kijichi, Dar es Salaam, alisema baadhi ya wateja hivi sasa hawahangaiki hata kuomba mtoa huduma ajaribu kufanya muamala.
“Zaidi ya kutoa na kuweka hela kwenye mitandao ya simu hatuna kazi nyingine na benki sasa hivi kupitia mawakala ndiyo ilikuwa suluhisho, ila watu wanakimbia ukiwaambia mtandao hakuna,” amesema Mapunda.
Kauli hizi zinaungwa mkono na taarifa mbalimbali za benki zinazotumwa kwa wateja, zikiomba radhi juu ya hali hii.
“Ndugu mteja, kuna changamoto ya upatikanaji wa baadhi ya huduma zetu kutokana na hitilafu ya mtandao. Wadau wetu wanaendelea kushughulikia tatizo hili, Asante,” ni ujumbe wa benki ya NMB kwa wateja wake.
Taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Benki (TBA), Theobald Sabi, ilisema benki zimeimarisha uwezo wa uendeshaji wa matawi yao ili kukidhi utitiri wa wateja wanaoingia kupata huduma ambao walikuwa wakihudumiwa kwa njia mbadala.
“Tunafahamu usumbufu unaosababishwa na kukatika kwa mtandao kwa sasa ambao pia umeathiri shughuli zetu mbadala za kibenki. Kipaumbele chetu kinabakia kuhakikisha kuwa huduma za kibenki zinaendelea ili kudumisha uzoefu wa wateja wetu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Grace Michael alisema mpaka sasa hawajapokea malalamiko kutoka kwa watoa huduma, ikiwa ni ishara bado hawajaathiriwa na changamoto hiyo.
Katika hilo amesema tayari watoa huduma wao wameshaelekezwa njia mbadala inayoweza kutumika ili huduma zisisimame.
“Tunatoa huduma kwa wagonjwa hivyo ni lazima tuhakikishe kunakuwa na njia mbadala ikiwa kuna changamoto ya mtandao,” amesema Grace.
Uchakataji, uwasilishaji maudhui
Changamoto ya intaneti imeitafuna pia tasnia ya habari katika utoaji wa maudhui jambo ambalo linaongeza muda wa ufikaji wa taarifa kwa wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu ameelezea namna hali hiyo inavyosababisha ugumu katika ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa habari.
“Hatuwezi kuandaa na kuchapisha habari kwa wakati. Maudhui yetu hayawezi kuwafikia wateja kupitia majukwaa yetu kwa sababu pia hawana intaneti ambayo itawawezesha kutembelea Youtube yetu, majukwaa ya mtandaoni na kununua magazeti yetu kupitia ePaper,” amesema Machumu.
Alisema hali iliyotokea inatoa changamoto kwa mamlaka husika kuja na njia mbadala ambayo itahakikisha uwepo wa uendelevu wa biashara inapotokea hali kama hii.
“Inaweza kuwa gharama lakini si kitu kisichowezekana. Pia ni muhimu kama itahitajika Serikali inaweza kushirikiana na wengine ndani ya ukanda huu, ni namna tu ya kupata rasilimali za kutekeleza mradi kama huo,” amesema Machumu.
Mkuu wa Kitengo cha Maudhui mtandaoni na Ubunifu wa MCL, Zouhra Malisa amesema baada ya kugundulika kuwapo kwa tatizo hilo ilikuwa ngumu kuhabarisha umma juu ya uwepo wake.
“Ilituchukua saa mbili kuchapisha taarifa iliyohusu tatizo hilo katika mitandao ya kijamii ya kampuni. Kwa kawaida chapisho kama hili huweza kutuchukua chini ya dakika moja,” amesema Zourha.
Amesema kama kampuni inayozalisha maudhui, sehemu ya mapato yake yanatokana na uuzaji wa maudhui kwa wasomaji wake kupitia mtandao.
“Bila intaneti, wasomaji wetu hawawezi kufikia bidhaa zetu. Tunapoteza mapato na wasomaji,” amesema Malisa.
Huko mitandaoni, baadhi ya wafanyabiashara wameanza kuomba wateja kuendelea kuwaunga mkono kwa kile wanachoeleza kuwa kama watasubiri hali iwe kama awali watakufa njaa.
“Sawa mtandao unasumbua lakini msisahau kutuungisha (kununua) maisha yaendelee tutakufa njaa wengine maana huku ndiyo maisha yetu yalipo,” ameandika mmoja wa wafanyabiashara.
Yeye akiomba wateja, mwenzake alionyesha wasiwasi wa kupatikana kwa fedha anazotakiwa kulipia huduma mbalimbali.
“Hii hali isipopatiwa ufumbuzi kwa haraka tutalipaje mikopo jamani, mbona mambo ni magumu hivi, kampuni za simu zijitahidi basi kutafuta mbinu walau waongeze kidogo upatikanaji wa mtandao ili maisha yaendelee,” ameandika.