Mbeya/Songwe/Sumbawanga. Madaktari bingwa na bobezi wametia kambi katika mikoa mitatu ya nyanda za juu wiki hii.
Madaktari hao ambao wameanza kutoa huduma za kibingwa na bobezi kwa wananchi wa halmashauri zote za mikoa hiyo ya Songwe, Mbeya na Rukwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo leo Jumanne Mei 14, 2024 katika Hospitali ya Wilaya Mbeya Vijijini, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Richard Machange amesema kwa muda waliodumu katika kazi hiyo, wamebaini ndoa za mke na mume kuishi mbalimbali huchangia wanawake kukosa uzazi kiasi cha kudhaniwa ni wagumba.
Hata hivyo, amesema sababu zipo hivyo wakati wanaendelea na kazi za kitabibu, pia watatoa elimu kwa wanawake na waume juu ya umuhimu wa kuishi pamoja ili kuendeleza uzao.
“Unakuta mwanamume yupo mkoa fulani na mke anaishi sehemu nyingine wanakutana baada ya miezi sita, hiyo inaharibu mzunguko wa siku za mwanamke na wakati mwingine hujikuta wanapokutana, kinakuwa si kipindi cha kutungisha mimba,” amesema Dk Machange.
Amesema kutokana na hali hiyo, wanawake wengi wakikaa muda mrefu bila kupata ujauzito hujihisi ni wagumba.
Daktari bingwa wa usingizi, ganzi na mahtuti, Daniel Gurishi amesema bado kada hiyo ina wataalamu wachache ukilinganisha na mahitaji.
Hivyo, amesema anaimani wakimaliza kambi hiyo, watakuwa wamewaambukiza utaalamu baadhi ya madaktari watakoshikirikiana nao kutoa matibabu katika halmashauri za mkoa huo wa Mbeya.
Mmoja wa wananchi waliofika hospitalini hapo kwa ajili ya kupata huduma, Hope Ngamiro amesema ujio wa madaktari hao umewarahisishia kupata matibabu kwa gharama nafuu zaidi ukilinganisha na awali.
“Mara nyingine mtu anaweza kukata tamaa kwa kuwa huduma za kibingwa zinapatikana mbali, hawezi kuzifuata anaishia kunywa mitishamba hali inayomuweka katika hatari ya kifo,” amesema Ngamiro.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amewataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo akieleza kuwa Serikali imeamua kuwafikishia huduma pale walipo.
“Uongozi unatofautiana, Rais wetu Samia Suluhu Hassan anawafikia wananchi kwa vitendo na leo madaktari bingwa wamefika hapa na watakuwapo kwa wiki moja hivyo wenye matatizo wafike kupata huduma” amesema Malisa.
Wanachi mkoani Songwe wamesema ujio wa
madaktari umewapunguzia gharama na hata wagonjwa waliokuwa wanashindwa kufuata huduma hizo sasa watazipata kwa wepesi.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo,
Mariamu Mwashambwa mkazi wa Vwawa Mjini amesema wanatumia fedha nyingi kufuata huduma za kibingwa Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
“Naishauri Serikali iendelee kutoa huduma hii mikoani kila baada ya miezi sita ili kuwarahisisha wananchi kupata huduma hii,” amesema Mwashambwa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Boniface Kasululu amesema madaktari hao watatoa huduma ya magonjwa ya ndani, upasuaji, usingizi, watoto,wanawake na huduma za uzazi.
“Tangu tumewapokea madaktari hao, wanawake ndio wanajitokeza kwa wingi kupata huduma,” amesema Dk Kasulu bila kutoa takwimu.
Kiongozi wa timu ya madaktari hao bingwa na bobezi, Anna Magembe kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili amesema lengo la kufika Songwe ni kutaka kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo akizungumza wakati wa kuwapokea madaktari hao amewaomba watoe huduma kulingana na miongozo sambamba na kuwapa ujuzi madaktari wa hospitali za wilaya ili wasaidie kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi pindi wao wakiondoka.
Mratibu wa timu hiyo kutoka Wizara ya Afya, Celphen Budodi ametoa wito kwa wale wote wanaohitaji huduma hizo wajitokeze kupata huduma.
“Wito wangu wananchi wote wajitokeze kupata matibabu kwa sababu madaktari bingwa wapo na watapatiwa huduma stahiki,” amesema Budodi.
Akizungumzia kambi yao, daktari bingwa na bobezi wa magonjwa ya watoto, Faraja Mwaipopo amesema ndani ya siku tano watakazokuwapo kambini hapo, watajitahidi kutoa huduma ili kutimiza malengo ya kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan anayetaka kila Mwananchi apate huduma bila kikwazo.
Dk Mwaipopo amesema watoto wengi hivi sasa hasa wale wa pembezoni wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa lishe bora.
Hivyo, watatumia fursa hiyo pia kutoa elimu ya lishe bora ya mtoto kwa wazazi.
Anna Wilson aliyefika kupata huduma za kibingwa amesema ujio wa madaktari hao umewapunguzia mzigo wa gharama.
(Imeandikwa na Denis Sinkonde (Songwe), Sadam Sadick (Mbeya) na Denis Sinkonde (Sumbawanga)