WAKATI Ihefu ikishusha presha katika vita ya kushuka daraja, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime ameelezea siri ya kiwango cha nyota wake Marouf Tchakei na Duke Abuya.
Wawili hao wamekuwa bora uwanjani na kuchagiza matokeo mazuri kwa timu hiyo, wakihusika katika jumla ya mabao 15 kwenye michezo yote ya mashindano yote ya timu hiyo.
Tchakei raia wa Togo amefunga mabao tisa Ligi Kuu na asisti mbili, huku Mkenya Abuya, akifunga sita ikiwamo mawili ya Kombe la Shirikisho (FA) na kuiwezesha Ihefu kufuzu nusu fainali.
Ihefu (Singida Black Stars), ikicheza juzi kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons na kupanda nafasi ya saba kwa pointi 32.
Katika mchezo huo, bao pekee la straika Tchakei raia wa Togo ndilo lilitosha kumaliza dakika 90 na kuiwezesha timu hiyo iliyotimkia mkoani Singida kujihakikishia alama pointi tatu.
Maxime amesema ushindi huo ulipunguza presha kwa kiasi fulani katika jitihada za kupambana kukwepa kushuka daraja na kwamba kwa sasa hesabu ni michezo mitatu iliyobaki.
Amesema hawakuwa na matokeo mazuri kiasi cha kuwapa wakati mgumu na presha kubwa, lakini kwa sasa wanahamishia nguvu kwenye mechi dhidi ya Tabora United, Mei 20.
“Presha imepungua kwa kiasi fulani, japokuwa bado tunahitaji ushindi ili kujihakikishia kubaki salama, kwa sasa ligi imekuwa ngumu na kupata pointi tatu dhidi ya Prisons ya sasa haikuwa rahisi,” amesema Maxime.
Kuhusu pacha ya Mkenya Abuya na Tchakei ambao wamekuwa na muunganiko bora, Kocha huyo alisema nyota hao wanafanya kazi nzuri wanayoelekezwa na kwamba kuwaandaa haikuwa kazi nyepesi.
Amesema kama ilivyo timu kwa ujumla amekuwa akitumia muda aliokabidhiwa kikosi ili kuwanoa na wanachofanya ni kuonesha uwezo na matokeo ya wanachoelekezwa.
“Niwapongeze vijana wote wanafanya vizuri, hao kina Tchakei na Abuya wanatekeleza vyema maelekezo na kufanya timu kubadilika kila mara, kujua vita ya ufungaji hiyo siwezi kuelezea,” amesema kocha huyo.