Mke wa Balozi alalamika kuvamiwa na wasiojulikana

Unguja. Mwanaamina Farouk, mke wa Balozi wa Tanzania anayemaliza muda wake nchini Comoro, Pereira Ame Silima, amelalamika kuvamiwa na kutishiwa maisha nyumbani kwake na watu wasiojulikana.

Pia, amelilalamikia Jeshi la Polisi akidai limeshindwa kufuatilia tukio hilo.

Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limekiri kupokea taarifa za tukio hilo likieleza linalifuatilia.

Hilo linajiri mwezi mmoja ukiwa umepita baada ya Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar kudai kuna matukio ya uhalifu ambayo hayashughulikiwi na polisi kikamilifu, kikilitaka Jeshi hilo kuongeza umakini na kudhibiti matukio hayo.

Siku moja baada ya ACT-Wazalendo kutoa madai hayo kupitia kwa Katibu wa Habari, Uenezi, Mawasiliano na Umma, Salim Biman, Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamad Khamis Hamad alikitaka chama hicho kuacha kutoa taarifa za kuwapo matukio hayo na kuzua taharuki.

ACT-Wazalendo ilitoa kauli hiyo baada ya aliyekuwa katibu wa chama hicho jimbo la Chaani, Ali Bakari Ali kuuawa na watu waliodaiwa kutojulikana na kuutelekeza mwili wake.

Hata hivyo, taarifa hiyo ilikanushwa na polisi likieleza aliuawa na watu aliokuwa akifanya nao biashara.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Mei 14, 2024 Mwanaamina amesema matukio ya kuvamiwa yametokea mara mbili, la hivi karibuni amedai limetokea Mei 4, 2024 saa nane usiku nyumbani kwake Mazizini.

Amedai tukio la kwanza lilitokea nyumbani kwake hakukuwa na ulinzi.

Amesema baada ya tukio hilo aliweka walinzi wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), hivyo waliporejea mara ya pili waliwadhibiti.

Ameeleza waliovamia nyumbani kwake hakuna kitu walichochukua lakini anaishi kwa hofu kutokana na jambo hilo.

“Mara ya kwanza nilikuwa naswali baada ya kumaliza nikasikia kishindo, baadaye walipoingia ndani nikajificha na wanangu, waliingia chumbani kwangu wakaangali hawakutuona, tulipiga simu polisi wakaja,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwanaamina, watu hao walipanda ukuta kwenye varanda wakapenyeza mkono wakatoa loki na kuingia ndani.

“Kama wamekuja mara ya kwanza, wakarudi mara ya pili, sijui wanataka nini na lini kitatokea. Hapa nina watoto wadogo kwa hiyo tunaishi kwa hofu,” amesema.

“Kama wameshindwa kunipata lakini hawajaiba kitu, kwa hiyo inawezekana hawataki vitu wanataka mtu. Watoto wamekuwa na hofu hawawezi kukaa ndani,” amesema.

Amesema baada ya tukio hilo alipiga simu polisi ambao walifika kuangalia wakasema wangerudi kuchukua maelezo lakini anadai hawajarudi na hajui kinachoendelea.

“Kinachotisha zaidi hawakuiba ila wanapekua vitu, kwa hiyo hatujui kinachoendelea, anakuja na silaha, kwa sababu mwizi wa kawaida angeiba na kuondoka,” anasema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchomvu amekiri kupokea taarifa za tukio hilo la Mei 4, 2024 saa nane usiku.

“Askari waliokuwa doria walipokea taarifa kutoka uongozi wa JKU wakielezwa huko Mazizini kuna eneo wanalinda wakaomba msaada zaidi na walifika,” amesema. 

Hata hivyo, amesema baada ya askari kufika eneo la tukio waliona mazingira yapo salama na hapakuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea kwa hiyo wakaendelea na shughuli zao.

“Ni kweli taarifa zilifika kwa sababu chombo kinacholinda pale kipo imara, lakini tunaendelea kufuatilia, nimuombe huyo mama aje ofisini tujadili kuhusu suala la usalama wake, nipo tayari,” amesema Mchomvu.

Mbali na hilo, polisi mkoani humo limeanzisha operesheni maalumu kukabiliana na matukio ya unyang’anyi ambayo yametajwa na Jeshi hilo kuwa tishio.

Kwa mujibu wa Mchomvu, ndani ya miezi sita wamekamata vijana 117 kati ya hao 60 ni kwa matukio ya unyang’anyi.

“Kati ya vijana hao, watuhumiwa 60 wamekamatwa na makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha za jadi (mapanga), unyang’anyi wa kutumia nguvu, shambulio, mauaji na watuhumiwa 57 walikamatwa kwa makosa ya wizi,” amesema Mchomvu. 

Amesema unyang’anyi huo unafanywa na vijana wanaotumia dawa za kulevya kwa kuanzisha vikundi mitaani vinavyotumika kuwavizia wananchi na kuwanyang’anya mali zao kwa kutumia silaha za jadi.

“Vijana hao wanatembea wakiwa wamebeba mapanga ila wakikamatwa na kuulizwa wanadai ni utamaduni wa Zanzibar mwanamume kutembea akiwa na panga au kisu.

Kamanda amesema hilo halikubaliki kwa kuwa, hiyo ndiyo njia wanayoitumia kufanya uhalifu.

Related Posts