MBUNGE wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi (CCM) ameishauri Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) kutumia simu za mkononi ili kuwapeleka wananchi taarifa muhimu pale inapotokea kuna hali tete katika maeneo mbalimbali kuhusu hali ya hewa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Prof. Ndakidemi ametoa rai hiyo leo Jumatatu bungeni jijini Dodoma wakati akiuliza swali la nyongeza kwamba ni lini Serikali itapeleka watumishi wa TMA katika ngazi za kanda, mkoa na wilaya ili kuboresha huduma za mamlaka hiyo kwa wananchi.
Katika swali la msingi, Prof. Ndakidemi alihoji Serikali ina mpango gani wa kuboresha utendaji wa Mamlaka ya Hali ya Hewa ili waweze kutoa utabiri sahihi.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alisema alisema licha ya kwamba taarifa za TMA zimekuwa zikifika karibu nchi nzima, tayari Serikali kupitia mamlaka hiyo imeanzisha mchakato kutengeneza mfumo wa farmer sms kwa wakulima.
Amesema ikikamilisha mfumo huo wa kutuma taarifa kwa wakulima, itaendelea kuboresha huduma za taarifa kwa makundi mengine na hatimaye kuifikia jamii nzima.
Aidha, Kihenzile amesema hadi sasa TMA ina watumishi 537 lakini pia imeshaajiri watumishi wengine wapya 31 lakini kwa mwaka wa fedha ujao inatarajia kuajiri watumishi 64.
Kuhusu mpango wa kuboresha utendaji wa TMA, Kihenzile amesema katika kuiwezesha TMA kufikia lengo la kutoa utabiri sahihi wa hali ya hewa nchini, Serikali kupitia Bajeti ya Maendeleo ya mwaka 2023/24 imetenga jumla ya Sh 13 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa rada, vifaa na miundombinu ya hali ya hewa ambapo utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali ikiwemo, ufungaji wa Rada mbili za hali ya hewa unaofanyika katika mikoa ya Mbeya na Kigoma.
Aidha, amesema TMA imeingia mkataba wa kununua rada nyingine mbili za hali ya hewa zitakazofungwa katika mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro na hivyo kufikisha lengo la muda mrefu la kuwa na Rada saba za hali ya hewa nchi nzima.
Pia TMA imeingia mkataba wa kununua mtambo ya kisasa ya kuandaa utabiri wa hali ya hewa (complete forecasting system) ambayo itaimarisha uwezo wa kupokea data za hali ya hewa, picha za satellite, kuchakata na kuchapisha kidigitali matokeo ya utabiri wa hali ya hewa
’’TMA imenunua mitambo mitatu ya uangalizi wa hali ya hewa katika Bahari ya Hindi ambayo itafungwa katika pwani ya Zanzibari, Dar es Salaam na Bagamoyo na hivyo kuongeza mchango wa huduma za hali ya hewa katika uchumi wa buluu.
‘’Aidha, mitambo 15 ya kupima hali ya hewa mahasusi kwa sekta ya Kilimo imeshanunuliwa na itafungwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Jumla ya mitambo 10 ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe (Automatic Weather Stations) imepkelewa ambapo mitambo mitatu (3) meshafungwa katika vituo vya hali ya hewa vilivyopo Mtwara, Songea na Arusha, maandalizi ya ufungaji wa mitambo saba iliyobaki yanaendelea,’’ amesema.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuimarisha shughuli za Mamlaka ya hali ya hewa kwa kujenga Ofisi ya hali ya hewa ya Kanda ya Mashariki na kituo cha Tahadhari za Tsunami Jijini Dar es Salaam ambapo kazi hiyo ya ujenzi imefikia asilimia 39.