Morogoro. Profesa Mussa Assad anatarajia kuongoza timu ya wachumi na wataalamu wa mahesabu hapa nchini, kupitia na kubadili mitalaa ya kufundishia katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) ili kuwawezesha wahitimu kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Mei 14, 2024, Ofisa Mtendaji mkuu wa taasisi hiyo, Profesa William Pallangyo amesema katika kufanikisha azma hiyo, wameunda timu maalumu kutoka nje ya taasisi kwa ajili ya shughuli hiyo.
“Tumeamua kuchagua timu ya wataalamu watakaounda timu ya ushauri wa kitasnia na kamati hii ina lengo la kuwasaidia wahadhiri wetu kwenye maboresho ya mitalaa na tunaipitia ya zamani na mipya, ya zamani itaboreshwa na mipya itatengenezwa itaongozwa na Profesa Mussa Assad (Mkuu wa chuo cha Kiislamu Morogoro (MUM),” amesema Profesa Pallangyo.
Naye Profesa Assad amesema kamati hiyo itahakikisha inakuwa kiunganishi kizuri na mitalaa watakayoitoa, watahakikisha inakidhi mahitaji ya jamii.
“Siku hizi teknolojia imeendelea maana kila kitu kinafanyika kwa teknolojia, hivyo kwenye mitaala tunayoandaa tutahakikisha kila mwanafunzi anajifunza ili kuendana na teknolojia itakayomsaidia kutekeleza majukumu yake,” amesema Profesa huyo.
Sostern Kweka ni Rais wa Serikali ya Wanafunzi TIA, amesema ubadilishwaji wa mitalaa hiyo utawasaidia kukidhi matakwa ya ajira.
“Awali, wanafunzi wenzetu waliohitimu walikuwa wakisema wanachokisoma darasani na kile wanachokutana nacho kwenye mazingira ya kazi ni tofauti, sasa ubadilishwaji huu utatusaidia sisi ambao bado tunasoma kuendana na soko la ajira tutakapo hitimu,” amesema.
Spika wa Bunge la Wanafunzi chuoni hapo, Erick Gabriel amesema: “Kuna wanafunzi wanaohitimu, lakini wana changamoto ya ukosefu wa ufanisi kwenye kazi zao, kwa hiyo tumeenda kuipitia na kubadili baadhi ya mitalaa iliyokuwa ikitumika zamani ili hata wahitimu watakaosoma wakimaliza wakidhi mahitaji ya ajira kwenye maeneo yetu.”