RAS LINDI AHIMIZA UTUNZAJI WA VYANZO VYA MAJI ILI VITUMIKE KWA MUDA MREFU.

Serikali Mkoani Lindi imeendelea kuhimiza wananchi na taasisi mbalimbali zilizopo ndani ya Mkoa huo kutunza na kulinda vyanzo vya maji ili viendelee kutoa ya maji kwa usalama na kwa muda mrefu. 

Katibu Tawala wa Mkoa  huo Zuwena Omary amehimiza hayo Mei 13,2024 kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa mradi wa maji na Usafi wa mazingira Mkoani humo.

Mradi huo unatekelezwa  na taasisi isiyo ya kiserikali ya ‘Heart to Heart’ chini ya ufadhili wa Shirika la Kimataifa la KOICA katika halmashauri ya Mtama kwa gharama ya bilioni 1.6 .

Katibu Tawala huyo ,Zuwena amesema upatikanaji wa maji safi na ya uhakika unategemea na utunzaji wa mazingira kuzunguka vyanzo vya maji  ikiwemo upandaji miti huku pia akitaka kamati za maji na mazingira zishirikishwe ili kufikia malengo ya mradi huo.

Mratibu wa mradi kutoka Heart to Heart Innocent Deus ameeleza mradi utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu (3) katika halmashauri ya Mtama na wanatarajia kuvifikia vijiji 87 na  kaya zaidi ya elfu 40  kukiwa na dhumuni la kupeleka huduma ya maji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha usafi wa mazingira unazingatiwa kuanzia ngazi ya vijiji hadi Wilaya.

Hata hivyo inaelezwa mradi huo wa maji  utasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo na kuboresha usafi wa mazingira kwa Wananchi.


Related Posts