Sh500 bilioni kutumika kuboresha miundombinu Muhimbili

Dodoma. Sh500 bilioni zitatumika kuijenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kuwezesha huduma zote za kibingwa na ubingwa bobezi kupatikana.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hayo leo Jumanne Mei 14, 2024 alipojibu swali la mbunge wa Konde, Mohamed Said Issa.

Katika swali, mbunge huyo amehoji kwa kuwa matibabu ya kibingwa na bobezi bado hayapatikani ni lini Serikali itakamilisha upatikanaji wa matibabu hayo.

Pia, amehoji kwa kuwa mifumo haisomani kati Muhimbili na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ni lini Serikali itahakikisha inasomana na kuokoa maisha ya wananchi.

Waziri Ummy amesema wanaendelea kuanzisha huduma mpya kwa kadri zinavyopatikana na utaalamu unavyopatikana.

Amesema ndiyo maana kuna huduma za kufanya upasuaji mgumu na kutumia roboti.

“Hivi karibu huduma zote za ubingwa na ubingwa bobozi zitapatikana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Kinachotukwamisha kidogo ni miundombinu, tunatarajia kutumia Sh500 bilioni kuijenga upya miundombinu ya Hospitali ya Muhimbili,” amesema.

Kuhusu mifumo kutosomana, amesema wanaenda kusimika upya mifumo ya Tehama, hivyo hospitali zote zitakuwa zikisomana.

Waziri Ummy amesema si masuala ya vipimo tu kati ya Jakaya Kikwete na Muhimbili bali hata waliofanya vipimo na majibu yaliyotolewa na hospitali zingine nchini yataonekana.

Katika swali la msingi, Issa amehoji ni lini Serikali itakuwa na hospitali kuu ya Taifa moja, ambayo itakuwa ikitoa huduma zote za afya bila ya kutegemea hospitali nyingine.

Waziri Ummy amesema tayari Serikali ina hospitali ya Taifa ambayo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Amesema kwa sasa hatua za kuiboresha hospitali hiyo zinatekelezwa ili kutoa huduma zote za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi.

Related Posts