Dar es Salaam. Aliyekuwa Msajili wa Ardhi Msaidizi, kutoka Wizara ya Ardhi mkoani Kilimanjaro, Emmanuel Bundala (41) ameileza Mahakama jinsi alivyofanya uchunguzi wa hati ya umiliki wa ardhi na kubaini mmiliki halisi alikuwa ni Stella Mwasha na siyo Rajesh Kumar.
Bundala ameeleza hayo leo Jumanne, Mei 14, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakati akitoa ushahidi kwenye kesi ya kujipatia Sh100 milioni kwa njia ya udanganyifu, inayomkabili Abubakari Hassan.
Hassan ambaye ni mkazi wa Nyangao mkoani Lindi, anakabiliwa na mashtaka manne yakiwamo ya kujipatia fedha, kughushi hati ya kiwanja na kughushi kitambulisho cha kupigia kura.
Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi, shahidi huyo amedai Februari 28, 2014 akiwa ofisi kwake Moshi mkoani Kilimanjaro, alisaini taarifa ya umiliki wa Kiwanja namba 17, Kitalu D kilichopo Moshi chenye namba ya usajili 171.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali, Aaron Titus, Bundala amedai aligundua hati ya umiliki wa Stella Mwasha ni sahihi baada ya kuleta vielelezo halisi vya umiliki huo na kufanya ulinganishi wa vielelezo vya hati aliyowasilisha ofisini hapo ilikuwa inafanana na iliyoko ofisini.
“Baada ya kufuatilia nilibaini hati ya Stella ilikuwa sahihi na hati za Rajesh zilikiwa ni feki kwani unaposajili hati kuna zingine zinabaki ofisini, tunazihifadhi ambapo tulifanya ulinganishi wa hati ya Stella ikawa sahihi lakini ya Rajesh ilikuwa feki,” amedai.
Ameendelea kuieleza Mahakama hiyo mmiliki wa kiwanja ambaye alituma maombi ya kufanya uamisho baada ya kuuziwa kiwanja kilichoko Moshi mjini, alitumia nyaraka ambazo zilikuwa siyo sahihi.
Amedai baada ya kuendelea na taratibu za kusajili Mei, 2014, alipokea zuio kutoka kwa Stella kwa kujitambulisha yeye ni Msimamizi wa Mirathi kwamba mmiliki wa kiwanja ni Ebeneza Mwasha (marehemu) ambaye alikuwa ni mume wake.
“Baada ya kupokea zuio hilo kutoka kwa Stella, tumepokea pingamizi lingine kutoka kwa Rajesh amenunua kiwanja kutoka kwa Abeneza Mwasha ambapo tulisaini zuio hilo na kutofanyika uamisho wowote,” amedai.
Shahidi amedai hati iliyowasilishwa na Rajesh ilikuwa tofauti kwa sababu mhuri wa moto uliogongwa ulikuwa haonekani vizuri na haukuonyesha umetoka ofisi gani na aliyesaini ni Kamishna yupi wa ardhi.
Ameendelea kudai katika hati ya Stella, mhuri wa moto ulionekana vizuri na ilisainiwa na mkurugenzi wa maendeleo ya ardhi na ulionyesha vizuri majina ya watu walioshuhudia.
“Ramani ya Stella katika hati hiyo ya ardhi inafanana na ambayo iko katika jalada ambalo liko ofisini kwa msajili wa hati na Ramani ya Rajesh ilikuwa tofauti kwani hata karatasi zilizotumika zilikiwa tofauti na zile zilizoko ofisini,” amedai.
Kutokana na maelezo hayo, Bundala ameomba maelezo yake yapokewe na Mahakama na kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka.
Mahakama hiyo imepokea maelezo hayo na kuwa kielelezo kwa upande wa mashtaka.
Shahidi baada ya kumaliza kutoa ushahidi, Hakimu Msumi, ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 28, 2024 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka.
Katika kesi ya msingi, Hassan anadaiwa kutenda makosa yake, Machi Mosi, 2014, mtaa wa Azikiwe, eneo la Benjamin Mkapa Tower, Dar es Salaam.
Inadaiwa siku hiyo, mshitakiwa alijipatia Sh100 milioni kutoka kwa Rajesh Kumar, baada ya kumdanganya atamuuzia shamba lililoko Moshi mkoani Kilimanjaro.
Shtaka la pili, mshitakiwa alighushi hati ya kiwanja kilichopo Moshi ikionyesha hati hiyo ilitolewa Wizara ya ardhi
Shtaka la tatu, Hassan ameghushi kadi ya kupiga kura kuonyesha imetolewa na Tume ya uchaguzi, wakati akijua kuwa ni uongo.
Pia, Hassan akiwa Mtaa wa Azikiwe, jiji hapa Dar es Salaam, alijitambulisha kwa Kumar kuwa yeye ni Ebeneza Mwasha na kisha alijipatia Sh100 milioni.