Tatizo Prisons hili hapa, Mashujaa kazi ipo

KICHAPO cha bao 1-0 walichopata Tanzania Prisons juzi dhidi ya Ihefu, kimemuamsha Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ahmad Ally akitaja sababu tatu zilizowanyima ushindi kwenye mchezo huo.

Prisons ikicheza nyumbani juzi ilifikisha mchezo wa nane mfululizo bila kushinda ikiwa ni kupoteza miwili dhidi ya Ihefu na Mtibwa Sugar na sare sita na kuwa nafasi ya tano kwa alama 33.

Maafande hao mara ya mwisho kushinda ilikuwa Machi 16, dhidi ya Simba 2-1, kisha kufululiza sare dhidi ya JKT Tanzania, KMC, Kagera Sugar, Geita Gold, Coastal Union na Dodoma Jiji.

Ally amekiri nyota wake kucheza chini ya kiwango, uchovu wa safari na majeruhi kwa baadhi ya wachezaji akieleza kuwa iliwagharimu na kujikuta wakipoteza mchezo huo.

Amesema baada ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji Ijumaa, walianza safari usiku ambapo walipumzika Jumapili kisha kuamkia uwanjani dhidi ya Ihefu.

“Kuna wachezaji watatu tegemeo ni majeruhi, Samuel Mwaituka, Ibrahim Abraham na Mussa Haji, lakini kwa ujumla mchezo wetu na Ihefu tumecheza chini ya kiwango” amesema kocha huyo.

Amesema baada kukosa ushindi kwa muda mrefu, kazi inahamia rasmi kwa mechi ijayo dhidi ya Mashujaa kuhakikisha wanashinda ili kujihakikishia kuwa salama.

“Tumebakiwa na mechi tatu muhimu sana, kati ya hizo tunataka kuanza na Mashujaa Mei 20 tushinde ili kufikisha alama 36 zitakazotuweka salama kabla ya kumaliza msimu,” amesema Ally.

Timu nyingi ndogo na za kati zimekuwa zikitumia usafiri wa barabara kwa safari zote, zikiwamo zinazozigharimu kuwa safarini kwa zaidi ya siku mbili, jambo ambalo huwafanya wachezaji kufika wakiwa wamechoka.

Akizungumza na Mwanaspoti, mtaalamu wa viungo na mazoezi, Idrisa Rajab amesema wanamichezo wanatakiwa kupata muda mwingi wa mapumziko baada ya kufanya mazoezi au kucheza ili kurejesha ufiti wa miili yao.

“Na hapo tu katika kusafiri muda mrefu baada ya kumalizika kwa mchezo mfano wa soka ni wazi kwamba (wachezaji) wanakuwa hawajapumzika na ni uchovu ukizidi madhara yake huja pia na maumivu ya muda mrefu yanayoshusha ufanisi uwanjani au mchezoni,” amesema.

Related Posts