Dodoma. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpeleka katika wizara hiyo kwa sababu miaka miwili iliyopita ustaarabu ulikuwa ni mdogo kwake.
Hayo yamesemwa leo jioni Jumanne, Machi 14, 2024 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2024/25.
Ulega ameanza kwa kumshukuru Rais Samia kwa wasaidizi aliompa wakiongozwa na Mnyeti.
“Mheshimiwa Naibu Spika, (Mussa Zungu) niseme mbele ya Bunge hili, wengi wanavyomfahamu Mheshimiwa Mnyeti na yule aliyefahamika kama mtu mkorofi hivi. Lakini nataka nikuhakikishie Naibu Spika na Bunge lako, Mheshimiwa Rais ni mama mwenye maarifa makubwa sana.
Ameniletea huyu Mnyeti tufanye kazi na yeye mwenyewe amesema katika hadhara hii namna ambavyo amekutana na uungwana wa hali ya juu kabisa (katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi),” amesema.
Amesema leo wakati wanafanya mjadala wa kujadili hoja (zilizowasilishwa katika bajeti) tukiwa na Mnyeti pamoja na Katibu Mkuu, Profesa Riziki Shemdoe aliwaeleza juu ya tofauti ya ustarabu aliokuwa nao.
“(Mnyeti) akaniambia hivi waziri unafahamu miaka miwili mitatu hadi juzi tu hapa ustaarabu kwangu ulikuwa mbali sana lakini kwa hakika nimeingia mahali hapa na wewe na hii timu ya wizara niseme namshukuru Rais kwa kunileta nifanye kazi hapa timu hii,” amesema Ulega.
Amesema watu wa Jimbo la Misungwi mkoani Mwanza wamepata mbunge mzuri na kwamba Mnyeti aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Manyara ni mtu mkweli na mwenye msimamo.
“Kwa hakika mimi ananisaidia sana wakati mwingine napoona mahali panahitaji mtu mwenye haiba yake namtanguliza. Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) unifikishie salamu zangu za shukrani kuwa mchanganyiko tulionayo ni ile iliyochukua ubingwa jana,” amesema.
Kuhusu ufungaji wa Ziwa Tanganyika kuanzia kesho Jumatano, Mei 15 hadi Agosti 15, Ulega amesema mkataba ulioingiwa na nchi zinazozunguka haukuwa na ruhusa ya kufanya ufugaji wa vizimba katika ziwa hilo.
“Miongoni mwa faida ya huu mkataba katika zile protoko zilizosainiwa ni kuwa na vizimba, dunia yote inafahamu kuwa uvuvi wa asili unaanguka, hii ni hoja ya mabadiliko ya tabia nchi, hii ni hoja ya ongozeko la watu duniani,” amesema.
Amesema hakuna namna ila ni mwanadamu kutumia akili yake kupanda samaki katika ziwa hilo ili waweze kumpatia mazao na kwamba vizimba ni kitu cha uhakika zaidi kuliko uvuvi wa asili.
Amesema wakati mwingine mvuvi anatoka anakwenda katika maji hawezi kupata kabisa lakini kwa uvuvi wa vizimba anakuwa na uhakika wa kupata samaki.
Waziri huyo amesema yeye na Naibu Waziri wake (Mnyeti) watakwenda kuwaonyesha jinsi mazao ya samaki yalivyopatikana baada ya kipindi hicho cha kufungwa kwa ziwa hilo kitakuwa kimepita.
Amesema miongoni mwa changamoto waliyonayo ni upotevu mkubwa wa mazao ya samaki na kwa kuwa kipindi hicho watakuwa wamezalisha kiasi kikubwa cha mazao anawasiwasi wa kupotea kwa mazao.
Ulega amesema amejipanga watanunua magudulia ya kuhifadhia samaki ili kusudi wakagawe kwa wanawake wote wa Ziwa Tanganyika ili watakapovuna mazao yao Agosti 15, 2024 wasipoteze.
Amesema kipindi cha kati ya Mei, Juni na Julai ni kipindi cha baridi ambapo samaki anakimbia na kujificha kutokana na baridi hivyo hata kama wakiruhusiwa kwenda kuvua hawatapata mazao ya samaki ya maana.
“Nataka niwahakikishie ni jambo la utafiti, si jambo la hila kwamba tunawafanyia hiyana na kuwaonea,”amesema.
Aidha, Ulega amesema Serikali itaanza kuchanja mifugo yenyewe na katika bajeti hii wametenga Sh25 bilioni kwa ajili ya kwenda kuchanja.
Amesema hatua hiyo itawafanya wavuvi kuondokana na vishoka wengi kwa kuwa na uhakika pia na chanjo na utalaam wa wanaokwenda kuchanja tofauti na awali ambapo sekta binafsi ilikuwa ikichanja mifugo hiyo.
Amesema watatoa ajira ya muda mfupi kwa wataalamu waliosomea mifugo, kwa ajili ya shughuli hiyo ya kuchanja mifugo.
“Tumekubaliana hatuwezi kuwaacha watu wa Taifa hili kuwa watu wa kuonewa, kwasababu huko kuna vishoka wengi sana barabarani, mitaani. Mtu mmoja anatembea katika pikipiki lake daktari yeye, nesi yeye, dawa zenyewe hatuna ithibati nazo,” amesema.
Awali, Mnyeti amesema lazima wafugaji wafuate sheria wakati wa shughuli zao na kuzitaka mamlaka za Serikali za mtaa kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi.
“Sisi ni mawaziri wa ng’ombe, kondoo lakini wanaofuata sheria. Tusipofuata sheria iko siku wataingia ndani humu (bungeni). Kama hufuati sheria inakuhusu,” amesema.