Uzembe watajwa chanzo cha ajali iliyoua saba Morogoro

Morogoro. Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Alex Mkama amesema chanzo cha ajali iliyoua watu saba mkoani hapa ni  uzembe wa dereva wa lori aliyetaka kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari.

 Ajali hiyo imetokea leo Jumanne Mei 14, 2024 asubuhi Dakawa Wilaya ya Mvomero ikihusisha lori na gari ndogo aina ya Toyota Noah.

Hata hivyo, Kamanda Mkama amesema baada ya ajali kutokea, dereva wa lori alikimbia na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka.

“Tukio hilo limetokea maeneo ya Dakawa Wilaya ya Mvomero baada ya lori kuacha njia lilipojaribu kuyapita magari mengine, ndipo likagongana uso kwa uso na gari ndogo ya abiria aina ya Toyota Noah na kusababisha vifo hivyo saba na majeruhi, tunaendelea kumtafuta dereva wa lori ambaye amekimbia, tukimpata tutachukua hatua kali za kisheria dhidi yake,” amesema kamanda huyo.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu ajali hiyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mvomero, Francis Paul amesema wamepokea majeruhi saba na maiti sita kutokea eneo la tukio.

Hata hivyo, Dk Paul amesema kati ya majeruhi wawili waliopatiwa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro mmoja alifariki dunia akiwa njiani kuelekea hospitalini hapo.

“Saa 2:30 asubuhi tulipokea majeruhi  saba waliotokana na ajali iliyotokea Dakawa na miili sita ya marehemu ambao walifia eneo la ajali, kati yao wanawake ni wawili, mtoto mmoja wa miaka mitatu na wanaume wanne.

“Kwa majeruhi yuko mtoto wa miezi minne hata hivyo baada ya kumchunguza hajaumia sehemu yoyote, watu wawili wamepata majeraha makubwa tumewapa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro na wengine wanne tunaendelea kuwapatia matibabu,” amesema mganga mfawidhi huyo.

Akisimulia namna ajali hiyo ilivyotokea,  Maimuna Salumu, mkazi wa Dumila Kilosa ambaye ni majeruhi amesema, “tulikuwa tunatoka Dumila asubuhi kuja Morogoro Mjini, tulipanda Noah, kufika maeneo ya Bwawa la Tai mbele kidogo ile gari ya mizigo ikawa inataka kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake wakati sisi tuko karibu ndipo akawa ametufikia na tukagongana naye uso kwa uso tuliobahatika kutoka wazima ni sisi watatu wengine wako mahututi na dereva aliyekuwa anatuendesha amekufa.”

Shuhuda wa ajali hiyo, Godfrey Chacha amedai ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa dereva wa gari kubwa aliyekuwa akitaka kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.

“Barabara hii madereva wa magari makubwa wanaendesha magari bila kuchukua tahadhari, mara nyingi huwa wanaendesha mwendo kasi,” amesema Chacha.

Shuhuda mwingine Richard Joseph, mkazi wa Dakawa amesema kuna haja kwa askari wa usalama barabarani kuongeza umakini kwa kudhibiti madereva wote wanaovunja sheria kwa makusudi.

“Nimekuta ajali na magari yamegongana watu kadhaa wamekufa na magari yameharibika sana, siku hizi madereva wanaendesha magari wakiwa wamelewa ndiyo maana ajali ni nyingi,” amedai Joseph.

Related Posts