Wananchi Iringa watakiwa kulinda miundombinu ya barabara kwa matumizi endelevu

Na Mwandishi Wetu,  Iringa.

Wananchi mkoani Iringa wamehimizwa kuilinda na kuitunza vema miundombinu ya barabara ili iwe endelevu na wanufaike nazo kwa muda mrefu kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa na Meneja wa TARURA mkoa wa Iringa, Mhandisi David Tembo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi mbalimbali inayotekeleza mkoani humo.

“Serikali ya Awamu ya Sita imetoa bajeti kubwa ya matengenezo ya barabara, jukumu letu ni kuenzi jitihada hizi zinazofanywa na Serikali katika kuitunza miundombinu hii ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa lengo la kuimarisha uchumi wa nchi na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja,” amesema na kuongeza.

“Wananchi wanapaswa kufanya matumizi sahihi ya barabara ikiwemo kuepuka kupitisha ng’ombe barabarani pamoja na kufukia mifereji” amesisitiza

Amebainisha TARURA mkoani Iringa inahudumia mtandao wa barabara wenye Km 5116 ambapo Km 179 ni kiwango cha lami, Km 1800 kiwango cha changarawe na Km 3500 kiwango cha udongo, kati ya hizo Km 1800 zipo hali nzuri, Km 1900 hali ya wastani na Km 1300 zina hali mbaya.

Amesema kwa mwaka huu wa fedha 2023/24 Serikali imetenga bajeti kiasi cha Shilingi bilioni 16.9 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ili kuwezesha wananchi kufika kusikofikika.

Amebainisha kuwa wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali mkoani humo ikiwemo mradi wa RISE ambapo Serikali imetoa Shilingi bilioni 52.2 kwa ajili ya kutengeneza barabara za lami Wenda-Mgama Km 19 iliyopo wilayani Iringa na Mtili-Ifwagi Km 14 iliyopo wilayani Mufindi.

Pia amesema wanaendelea na matengenezo ya barabara kiwango cha lami Km 10.4 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa kutumia teknolojia ya “Ecoroads”.

Ameongeza kuwa wametekeleza mradi wa “Agri-Connect” barabara ya Kidabaga-Bomalang’ombe Km 19.4 kwa kiwango cha lami iliyopo wilayani Kilolo na barabara ya Sawala-Mkonge-Iyegeya Km 30.4 kiwango cha lami iliyopo wilayani Mufindi.

Naye, Bi. Julieth Mkorogwe, mkazi wa kata ya Kidabaga wilayani Kilolo amemshukuru Mhe. Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya kwani hapo awali walikuwa na shida ya usafiri na usafirishaji wa mazao yao wakati wa msimu wa mvua.

“Tunamshukuru Mhe. Rais kwa ujenzi wa barabara hii ambapo awali tulikuwa tunapata shida ya usafiri hasa msimu wa mvua nyingi, tulikuwa tunashindwa kusafirisha mazao yetu pamoja na kufika hospitali kwani kuna kituo kikubwa hapa Kidabaga ila kwasasa tunasafiri bila shida yoyote”.

Related Posts