Wavuvi walalama kufungwa Ziwa Tanganyika

Mwanza. Baadhi ya wavuvi wa mikoa ya Rukwa, Kigoma na Katavi inayozungukwa na Ziwa Tanganyika wamesema hawajui hatima yao wakati ziwa hilo likifungwa.

Imeelezwa kuwa ziwa linafungwa leo na litafunguliwa Mei 15, 2024 ili kupisha uzalishaji wa mazalia ya samaki.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akizungumza na Mwananchi leo amesema  kufungwa kwa ziwa hilo ni makubaliano yaliyoazimiwa katika kikao kilichofanyika mwaka 2022 kikihusisha nchi zinazozunguka ziwa hilo ambazo ni Zambia, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Nchi hizo zilikubaliana kwa kanuni moja ya kutambua zana haramu za uvuvi ili kuruhusu mazalia ya samaki kwa wingi na kudhibiti uvuvi haramu, uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

Ulega amesema Ibara ya 14 ya itifaki hiyo inazungumzia umuhimu wa kulipumzisha ziwa kutokana na shughuli za uvuvi kila mwaka kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15 kwa miaka mitatu mfululizo ikiwa ni kutoa nafasi kwa samaki kuzaliana.

Kwa mujibu wa ibara hiyo, katika kipindi hicho nchi wanachama wa ziwa hilo watafanya utafiti wa kiwango cha samaki, utafiti wa kibaolojia na matokeo ya kiuchumi kwa watu wanaotegemea ziwa hilo kimaendeleo.

Hata hivyo, itakumbukwa mwaka 2023 Serikali ilisitisha uamuzi wa kulifunga ziwa hilo baada ya malalamiko ya wadau wa uvuvi kutoshirikishwa katika uamuzi huo.

Lakini mapema mwaka huu, Serikali ilitangaza tena uamuzi huo wa kulifunga ziwa hilo kwa miezi mitatu licha ya pingamizi kuendelea kutoka kwa wadau wa sekta hiyo

Wakizungumza leo, wavuvi wa ziwa hilo wamesema hawajui hatma yao kwa sababu wanalitegemea ziwa Tangaznyika kuendeha maisha yao.

“Maisha yatakuwa magumu kuliko kawaida, hatuna maandalizi yoyoye katika hili na kwa bahati mbaya limekuja wakati watu tuna majanga makubwa, tumevamiwa na mafuriko, nyumba zimeathirika, watu hatuna pakushika kwa hiyo ni janga kwa kweli, linatuumiza mno,” amesema Abuu Kitangu mvuvi wa Kata ya Kabwe Sumbawanga mkoani Rukwa.

Kuhusu kupata vizimba vilivyotolewa na Serikali alisema ushirika wao wenye wavuvi takriban  280 kwenye vijiji vitano vya Kata ya Kabwe hakuna hata mmoja aliyepata wala hawana muongozo rasmi unaoonesha vizimba vinapatikana vipi.

Mvuvi wa ziwa hilo mkoani Kigoma, Kisekwa Mapunda amesema haoni tija kwenye usitishwaji wa shughuli za uvuvi kwa kipindi hicho akidai Serikali ingejikita kwanza kuzuia uvuvi haramu unaosababisha kufungwa kwa ziwa hilo.

“Mimi binafsi sioni kama italeta tija kwa sababu zana ambazo zinasababisha kupoteza mazao ya samaki Ziwa Tanganyika bado hazijadhibitiwa, kuna makila zinaitwa primayaa bado zinavua na kwenye sheria hazitambuliki. Kwa hiyo hata kama tukilifunga tukifungua mazao yataendelea kukosekana,” amesema mvuvi huyo.

Kuhusu maisha yao baada ya ziwa kufungwa amesema, “sisi hakuna tulichojipanga ni sawasawa na mtu unaambiwa hama kwenye nyumba, hujui unaenda wapi.”

Kauli ya kiongozi wa wavuvi

Kiongozi wa Wavuvi Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, Malius Kiluba amesema kikubwa kinachotakiwa kudhibitiwa ndani ya Ziwa Tanganyika ni uvuvi haramu na si kulifunga.

“Kama wadau wa uvuvi hatujashirikishwa zaidi ya kuona viongozi kutoka wizarani kuja sehemu za mikoa kukutana na utawala, wakuu wa mikoa, wilaya, madiwani, maofisa uvuvi wamekuwa wakijadiliana na kutoa maagizo lakini kama wadau wa uvuvi hatujahusishwa kutoa maoni yetu kuhusiana na msimamo huo, wanatuonea,” amedai kiongozi huyo.

Amesema kwa vile ziwa hilo linazungukwa na mikoa mitatu, ni vema Serikali ingekuwa inalifunga kimkoa kusudi wale wanaofungiwa wakafanye kazi ya uvuvi katika mkoa mwingene kuliko kufunga ziwa lote.

“Ebu angalia hali iliyopo Ziwa Tanganyika sasa hivi, mafuriko ni makubwa watu wengi wameharibikiwa na nyumba zao, hawajui wanaishije wala wanakula nini halafu leo unakuja na kauli ya kulifunga kabisa ..si unaenda kumuua!.”

“Mimi binafsi sioni kama ni tatizo lakini ni utaratibu gani unaweza ukatumika kwa mfano Burundi wana utaratibu kila mwezi, mwezi una wiki nne katika hizi wiki nne wiki tatu wanafanya shuguli za uvuvi wiki moja hawafanyi shuguli za uvuvi huo ni utaratibu wa Burundi..lakini sisi tuna maeneo ya hifadhi yanaweza kutengwa,” alisema.

Katibu wa Wavuvi Kigoma, Bakari Almasi amesema Serikali ilipaswa kuzuia baadhi ya hifadhi ziwani japo kilomita moja ziwa zima badalaya kusitisha kazi za uvuvi kwa miezi mitatu aliyosema ni mingi.

“Jambo hili ni gumu na linawalazimisha wavuvi walitii kwa sababu Serikali imeamua, lakini kuna vitu vingi ambavyo wavuvi hawajafanyiwa ili kuwaweka tayari kukabiliana na kipindi hiki cha ukame wa kuvua,” amesema.

Mkuzaji wa viumbe maji mkoani Kigoma, Alexander Elikado amesema, “Kufungwa kwa muda huo, samaki wataongezeka, jamii sasa inayotegemea pale ndio uchumi lazima ushuke lakini kwenye faida samaki wataongezeka, watakuwa wengi na siku likifunguliwa malalamiko yote haya hutayasikia kwa sababu watakuwa wanavua samaki wengi bila shida.”

Ziwa Tanganyika lina ukubwa wa kilometa za mraba 32,900 huku Tanzania ikimiliki kilometa za mraba 13, 489, sawa na asilimia 41 ya ziwa lote.

Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonyesha asilimia 19 ya samaki waliozalishwa nchini mwaka 2021, zilitoka Ziwa Tanganyika.

Wabunge wazungumza kufungwa ziwa

Akichangia taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2023/24 na makadirio ya mapato ya matumizi ya fedha  ya mwaka 2024/25 ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenani ameshauri kabla ziwa hilo halijafungwa itafutwe njia ya kupambana na uvuvi haramu akidai ndio chanzo cha samaki kupungua.

Ameongeza kuwa hata ugawaji vizimba unaoendelea kama mbadala wa ziwa kufungwa maandalizi yalipaswa kufanywa tangu mwaka jana akitaka elimu ya maandiko ya kuomba vizimba itolewe pamoja na kutengeneza mazingira mazuri kwa wavuvi.

 “Nachosema aproach inayotumika ndiyo sikubaliani nayo yawezekana nia ni njema tupate samaki wengi lakini kupata samaki wengi sio kufunga ziwa kwa miezi mitatu, tuandae operesheni maalumu ya kupambana na uvuvi haramu.

 “Tutafute suluhisho la uvuvi haramu sio kufunga ziwa, na mimi nashauri kama kata ina vijiji vinne msiende kufunga vyote mnaweza kufunga viwili vingine mkaacha,”amesema

Mbunge wa Kwela (CCM) Deus Sangu ameiomba Serikali iangalie jambo hilo kwa kina akidai wavuvi katika eneo lake tayari wamekumbwa na mafuriko, hali yao kiuchumi ni duni na shuguli waliyokuwa wakiitegemea ni uvuvi.

“Chanzo cha kuweka angalizo na katazo  la kutovuwa katika Ziwa Tanganyika ni uvuvi haramu, asilimia kubwa ya uvuvi haramu upo nchi jirani ya DRC Congo na Burundi…kwa bahati mbaya Serikali wameshindwa kudhibiti uvuvi haramu hata waliopewa dhamana ya kusimamia uvuvi haramu kwenye maeneo hayo ambao ni watu wa Serikali wanashindwa na wanashirikiana na hao hao ambao wanavua uvuvi haramu,” amesema.

Related Posts