Wizara yaombwa kuchunguza ubora wa maabara za udongo

Geita. Wizara ya Madini imeombwa kuchunguza ubora wa maabara za sampuli za udongo unaosadikiwa kuwa na dhahabu kutokana na baadhi  kutoa majibu yasiyoendana na uhalisia, hivyo kuwasababishia wachimbaji hasara ya mamilioni ya fedha.

 Pia, imeombwa kuwafungia watu wanaojitambulisha kuwa ni wajiolojia na kupewa maeneo ya kutafiti kisha kutoa majibu ya uongo huku wakijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Wakizungumza  katika mafunzo ya namna ya kupata taarifa sahihi za kijiolojia yaliyoandaliwa na Shirika la Solidardad, wachimbaji hao wamesema mara kadhaa wamekuwa wakipata hasara kutokana na majibu ya uongo wanayopatiwa na baadhi ya wajiolojia.

Baraka Jackson mchimbaji mdogo kutoka wilayani Chato amesema wataalamu wamekuwa wakiwasisitiza kuachana na imani potofu na uchimbaji wa kubahatisha.

“Mtu anakuambia chimba mita 100 utakuta mwamba wa dhahabu, unatafuta mwekezaji anaweka nguvu mnafika mita 100 chini hakuna kitu mwisho wa siku anapoteza hela na mwekezaji huyo anakuona wewe tapeli, tunaomba Serikali iingilie kati,” amesema Jackson.

Katibu wa Mgodi wa Ushirika wa Mgusu, Zakaria Nshoma amesema wimbi la wajiolojia matapeli wanaoshirikiana na wenye maabara za kupima udongo, huwatapeli wachimbaji wadogo kwa kuwahadaa kuwa eneo lina dhahabu kumbe si kweli.

“Kama Serikali haitaingilia kati na kuwachukulia hatua, wachimbaji wadogo watashindwa kabisa kufanya kazi na watarudi kwenye zile imani potofu, maana kwa sasa wamekubali kutumia sayansi, lakini shida ni hawa matapeli wanaochukua fedha zetu na kujifanya wanafanya utafiti kumbe ni utapeli tu,” amesema Nshoma.

Hata hivyo, amedai kuwa baadhi ya maabara wakipeleka udongo ukafanyiwe utafiti, ndiyo hucheza mchezo mchafu wa kutoa majibu ya uongo.

Akizungumza kwa simu juu ya malalamiko hayo, Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia wachimbaji wadogo, Francis Mihayo amekiri uwepo wa wimbi la wajiolojia pori wanaoshirikiana na baadhi ya watendaji wa maabara wasio waaminifu.

“Ni kweli kuna matapeli wengi kwa sasa kwenye sekta ya madini, awali walikuwa wanatumia waganga wa kienyeji, lakini sasa wamehamia kwa wataalamu na wanakutana na matapeli,” amesema Mihayo.

Amesema Geita kuna maabara ya Serikali na za binafsi, “anakuja mtu anadai ana udongo wake kumbe ameshakaa sawa na mtu wa maabara ndio maana tunatoa elimu wapeleke maabara ya Serikali yenye sifa na wasiamini maabara moja waende zaidi ya moja kupata uhakika zaidi.”

Amesema hivi sasa Serikali inaendelea na  mchakato wa kuunda bodi ya wajiolojia itakayowatambua kama zilivyo bodi za wanasheria, madaktari na wahandisi.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Emanuel Mwajombe ambaye pia ni mjiolojia mwandamizi kutoka Solidardad, amesema hali ngumu ya maisha na wachimbaji kupenda njia za mkato inaweza kuwa sababu ya uwepo wa wajiolojia feki.

“Kweli wapo wanaojiita wajiolojia sijui kama wamesoma, lakini hali ngumu ya maisha inaweza kuchangia kuwafikisha hapo wachimbaji hawa wadogo. Sasa ili kuepuka hilo, ni vema wakaacha kupita njia za mkato na waende kwenye njia sahihi,” amesema Mwajombe.

Ofisa mradi kutoka Soldardad, Victor Kayombo amesema mafunzo yanayotolewa na shirika hilo sio tu yatawawezesha kupata taarifa sahihi, bali yatawaongezea wachimbaji hao tija na kuaminiwa na taasisi za fedha na kupatiwa mikopo ya kuendeleza kazi zao.

“Tunawapa mafunzo ili wapate taarifa sahihi za kijiolojia na waachane na uchimbaji wa kubahatisha,” amesema Kayombo.

Related Posts