BoT yatoa angalizo mikopo ‘kausha damu’

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imewataka Watanzania kutoa taarifa juu ya uwepo wa taasisi, kampuni au watu binafsi wanaofanya biashara ya kukopesha bila kuwa na leseni au kutozingatia taratibu zilizowekwa.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni udhibiti wa watu wanaotoa mikopo kiholela ambayo baadhi imekuwa ikiwaumiza wananchi kwa kuwapa riba kubwa ikilinganisha na walichokopa, kuwadai kwa kero na hata kufilisi mali zao.

Pia, baadhi ya kampuni hizo ambazo zimekuwa zikitoa mikopo umiza zimekuwa zikitoa muda mfupi kwa wakopaji, jambo ambalo linafanya wengi washindwe kutimiza masharti ya mikopo hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na BoT na kusainiwa na Gavana Emmanuel Tutuba Mei 13, 2024, umma umetakiwa kujiepusha kufanya biashara na taasisi kampuni au watu wanaotoa huduma za kukopesha bila kuwa na leseni halali iliyotolewa na BoT.

“Napenda kuufahamisha umma kuwa chini ya kifungu cha 17 cha sheria ya huduma ndogo za fedha 2018 Benki Kuu ya Tanzania ina mamlaka ya pekee ya kutoa leseni kwa taasisi, kampuni au watu binafsi zinazojihusisha na kutoa mikopo,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imewataka Watanzania kutoa taarifa kwa BoT au vyombo vya usalama juu ya uwepo wa taasisi, kampuni au watu binafsi wanaofanya biashara ya kukopesha bila kuwa na leseni au kutozingatia taratibu zilizowekwa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Pia kwa mujibu wa kifungu cha 16 (1) cha sheria hiyo,  ni kinyume cha sheria kujihusisha na biashara ua kukopesha bila kuwa na leseni na katazo hilo linajumuisha utoaji wa mikopo kwa njia mbalimbali ikiwemi kwa njia ya kidigitali.

Kwa sasa utoaji wa mikopo kwa njia ya kidigitali umeshamiri kwenye mitandao ya kijamii ambako wahusika hujitangaza na kutafuta wateja.

Mikopo hiyo huondoa ulazima wa mtu kutembea kuifuata ofisi na badala yake hufanya kila kitu kupitia kifaa chake kinachounganisha intaneti hadi kupewa mkopo na malipo hufanyika kwa njia hiyo.

Urahisi huo hugeuka kuwa shubiri kwa baadhi ya watu ambao hushindwa kulipa mikopo hiyo kwa wakati kutoka na watu wao wa karibu kutumiwa ujumbe wa maandishi wa kuwataka kuwakumbusha jamaa zao kulipa madeni.

Katika hili, mmoja wa wakopaji ameliambia Mwananchi Digital kuwa deni la mkopo aliochukua mtandaoni lilianza kudaiwa siku mbili kabla ya siku ya kulipa kufika.

“Nilikopa Sh50,000 lakini ilikuwa ni kwa siku nane ndiyo nilipe, ilipofika siku ya sita nilianza kupigiwa simu kila dakika na kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kutakiwa kulipa deni hilo licha ya kuwa nilikuwa bado na muda,” alisema Zaituni Hajji.

Mbali na Zaituni, Mahanja John yeye amesema baada ya kupitisha siku moja bila kulipa mkopo wake, ujumbe wa kudaiwa kwake ulianza kutumwa kwa watu wake wa karibu.

“Kiukweli nilikerwa kwa sababu sikujulishwa juu ya hili, nilisema kabisa kwa hili sitalipa, maana wameshanidhalilisha na hakuna sehemu watanipeleka,” alisema Mahanja.

Katika hii BoT inawakumbusha Watanzania kusoma kwa makini na kuelewa makubalinao wanayoingia na wakopeshaji ikiwa ni pamoja na kuelewa masharti ya mikopo na kuhakikisha kwamba mkopeshaji ana leseni halali ya kufanyabiashara ya kukopesha.

Mbali na hilo pia mkopeshwaji anatakiwa kupewa nakala ya mkataba uliosainiwa kwa njia sahihi na nakala hiyo inapaswa kutolewa na kila mkopeshaji anapotoa mkopo mpya.

Mei 2, 2024, suala la mikopo umiza au kausha damu liliibuka bungeni baada ya ya Mbunge wa Viti Maalumu, Felista Njau kutaka kujua Serikali inachukua hatua gani kwa kuwa wananchi mitaani wanaadhirika kwa kusombewa mali zao wanapochelewa kulipa.

Swali hilo liliibua mjadala mpana hadi Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuwaagiza mawaziri, Dk Mwigulu Nchemba (Fedha) na Nape Nnauye (Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) kwenda kulifanyia kazi kwa kuwa riba zake zimekuwa kubwa na zinawaumiza wananchi.

Related Posts