Siha. Mkuu wa wilaya ya Siha, Christopher Timbuka amewataka wananchi kutoa taarifa za watumishi wa umma wanaochelewa kufika kazini, ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao.
Timbuka ametoa wito huo leo Mei 15, 2024 wakati wa mafunzo ya usambazaji na uwasilishaji wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi, watendaji wa wilaya ya Hai na Siha yaliyofanyika Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro.
Katika mafunzo hayo, baadhi ya viongozi wa dini walihoji kuhusu watumishi wa umma wanaochelewa kufika kazini, jambo linalokwamisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa wakati.
Mkuu huyo wa wilaya amesema kuchelewa vituo vya kazi ni kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
“Masuala ya kuchelewa kazini kwa watumishi wa umma, yasiletwe kama malalamiko kwenye mikutano au vikao kama hivi, mnapoona toeni taarifa kwa viongozi yafanyiwe kazi,” amesema Timbuka.
Amesema kuchelewa kwao kazini kunakwamisha mambo mengi ya maendeleo kwa Serikali na hata kwa wananchi, kwani mwananchi anawahi mapema ili apate huduma arudi kwenye majukumu yake, lakini anakaa muda mrefu, jambo ambalo amesema halitakiwi kufumbiwa macho.
Hata hivyo, amewashauri watumishi hao kuzingatia muda wa kazi ambao unafahamika kuwa ni kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 9:30 alasiri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amiri Mkalipa amesema wamepokea ushauri wa viongozi wa dini, hata hivyo amewataka kusisitiza suala la uadilifu, hivyo wasiache kukemea.
“Siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili tunapokuja misikiti au kanisani, viongozi wa dini msiache tukaenda, mtuambie Biblia au Quran inasemaje kuhusu utumishi uliotukuka kwa uadilifu, kwenye suala la nidhamu na uwajibikaji,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurudin Babu amesema lengo la semina hiyo ni kuwajengea uwezo viongozi hao kuhusu kutafsiri katika kupanga na kuelekeza kufuatilia na kuthamini utekelezaji wa sera na mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu.
“Semina hii inatuongezea ujuzi na kupata uzoefu wa namna bora ya kutumia matokeo ya sensa katika kutekeleza wajibu wetu wa matumizi sahihi ya matokeo hayo kwa mipango jumuishi ya maendeleo endelevu.”
Mshiriki wa mkutano huo ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha Sau wilayani humo, Mdoe Yambazi amepongeza mafunzo hayo akisema yamempa uelewa wa kuendelea kuhakikisha wananchi wa Siha wanapiga hatua za maendeleo hadi vijijini.