Shirika la kimataifa la Nishati IEA limetangaza kuwa dola bilioni 2.2 za kimarekani zimeahidiwa na makampuni na serikali ili kuboresha upatikanaji wa nishati safi na salama barani Afrika. Taarifa hiyo imetolewa baada ya kumalizika kwa mkutano wa kilele uliowakutanisha pamoja viongozi wa mataifa 60 mjini Paris, Ufaransa. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alikuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo.
Soma zaidi.Dola Bilioni 2.2 zaahidiwa mkutano wa nishati safi ya kupikia Afrika
Zaidi ya watu bilioni mbili duniani hupika kwa kutumia majiko yanayotumia kuni na mkaa, matumizi hayo ya nishati yanatoa moshi ambao unatajwa kuwa ni miongoni mwa sababu kuu ya vifo vya mapema duniani.
Mbinu hizi za kupikia huathiri mazingira, misitu ambayo ndiyo inayofyonza Kaboni hukatwa kwa matumizi ya kuni na wataalam wanasema hali hiyo inachangia ongezeko la joto duniani.
Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la Nishati ni kwamba karibu theluthi moja ya pesa zinazohitajika ili kubadilisha na kuwahimisha watu duniani kutumia nishati safi na salama ya kupikia zinakusanywa kila mwaka.
Samia: Tunalenga kuwafikia watanzania kwa 80% mwaka 2034
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alikuwa miongoni mwa wazungumzaji katika mkutano huo wa kilele wa nishati na hapa anaeleza mipango ya Tanzania katika matumizi ya nishati safi na salama.
” Dhamira kuu ya Tanzania ni kutekeleza mkakati wetu wa Kitaifa wa miaka kumi ya ya nishati safi ya kupikia uliozinduliwa hivi karibuni ambao unalenga kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi na salama ya kupikia safi ifikapo mwaka 2034”.
Soma zaidi.Afrika inaweza kudhibiti soko la malighafi za nishati safi?
Mbali na mpango huo wa miaka kumi Rais huyo ameongeza kusema mpango huo sio tu kwamba unalenga kuboresha mazingira lakini pia kuwapunguzia mzigo wanawake ambao ndio waathirika wakubwa wa suala hilo.”
”Mfuko wa Kitaifa utaanzishwa ili kusaidia nishati safi ya kupikia na Waziri Mkuu atatoa usimamizi wa hali ya juu wa utekelezaji wa mkakati huo zaidi ya kuwapunguzia mzigo mzito wanawake wa Tanzania na Afrika na mpango sio tu utasaidia katika masuala ya mazingira na kiafya lakini pia utawawezesha wanawake kuwa mawakala wa mabadiliko ya ndani ya jamii zao”.amesema Samia.
Soma zaidi. Rais Samia azindua mkakati wa nishati safi Tanzania
Mwishoni mwa mkutano huo uliofanyika mjini Paris, mkuu wa shirika la IEA Fatih Birol amesema mkusanyiko huo umetoa ahadi ya uhakika ya kushughulikia suala hilo ambalo limepuuzwa kwa muda mrefu.
Benki ya Maendeleo ya Afrika na Shirika la kimataifa la nishati IEA zinatarajia kukusanya fedha dola bilioni 2.2 kwa ajili ya kuongeza uwekezaji katika masula ya nishati safi na salama kwa mwaka huu.