Katekista ajiua kwa kunywa sumu baada ya mawazo yaliyotokana na mfadhili wake kufariki

Anthony Mgaya (50) aliyekuwa Katekista wa Kigango cha Moronga kata ya Kipengere wilayani Wanging’ombe amefariki dunia akidaiwa kunywa sumu kutokana na msongo wa mawazo wa muda mrefu uliotokana na kifo cha mfadhili wake ambaye alikuwa wilayani humo aliyefariki takribani miaka miwili iliyopita.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Mahamoud Banga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo

“Majira ya saa nane mchana alikutwa nyumbani kwake na mkewe anaitwa Huruma Mbilinyi akiwa ananukia harufu ya sumu aina ya daiso ambayo ilikuwa store alivyokwenda store kukagua mabaki ya ile sumu kwa ajili ya kuulia wadudu hakuikuta kwa hiyo akaamini huyu bwana ameinywa ndio wakamchukua na kumpeleka hospitalini”ameongeza kamanda Banga

Banga ametaja sababu ya kifo hicho “kwa hyo sababu kubwa ni msongo wa mawazo ambapo alikuwa akifadhiliwa na mzungu ambaye alifariki muda si mrefu sana na toka alipofariki Mzungu huyu bwana akaanza kupata shida ya msongo wa mawazo jambo ambalo limepelekea kujitoa uhai wake”

Katika mazishi ya katekista Anthony Mgaya mwenyekiti wa kijiji cha Moronga Romanus Mgaya ametoa wito kwa wananchi kushirikisha jamii juu ya changamoto zinazowakabili hususani mawazo ili waweze kukabiliana nazo kuliko kuwa kimya na kuelemewa nazo hali inayopelekea vifo na kuacha familia ikiwa tegemezi.


Related Posts