Mapambano kati ya Israel na wanamgambo yaendelea Gaza – DW – 15.05.2024

Mapigano kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo yameshuhudiwa pia katika mji wa kusini wa Rafah ambao umekuwa kimbilio la raia katika vita vya zaidi ya miezi 7 kati ya Israel na kundi la Hamas.

Kulingana na shirika la habari la AFP vita hivyo hadi sasa vimeshasababisha vifo vya zaidi ya watu 35,000 katika ukanda huo.

Hayo yakijiri, Umoja wa Ulaya umeitolea wito Israel kusitisha mara moja operesheni zake katika mji wa Rafa. Umoja huo umesema kuwa operesheni hizo zinatibua usambazaji wa misaada ya kiutu Gaza na inasababisha watu kuhama, njaa na taabu kwa raia.

Soma zaidi: Zaidi ya watu 500,000 wakimbia mapigano Rafah, UN

Wito huo wa Umoja wa Ulaya umetolewa Jumatano na mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo Josep Borell. Kupitia ukurasa wake wa X, Borrell amesema ikiwa Israel itaendelea kufanya hivyo Rafah, itaweka doa kubwa kwa uhusiano kati yake na Umoja wa Ulaya.

Naye waziri wa mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken mpango madhubuti unahitajika kwa ajili ya mustakabali wa Gaza. Blinken amesema hawataiunga mkono Israel ikiwa italikalia tena eneo hilo.

Blinken amenukuliwa akisema, “Tumekuwa wazi linapokuja suala la mustakabali wa Gaza. Hatuungi Mkono na hatutaunga mkono Israel kuitawala Gaza. Pia bila shaka hatuungi mkono Hamas kuiongoza Gaza tumeona kilichotokea kwa kufanya hivyo kwa watu wa Gaza na kwa Israel”.

Netanyahu: Kuliangamiza kundi la Hamas ni muhimu

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema kuwa, kuliangamiza kundi la Hamas ni muhimu ili kupata mbadala wa kuiongoza Palestina.

Amepuuzia ukosoaji wa mataifa ya magharibi juu ya operesheni za wanajeshi wake kwenye mji wa Rafah na kusema kuwa janga la kiutu linalotajwa kuwepo kwenye mji huo bado halijajitokeza na kamwe halitatokea.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika moja ya hotuba kwa taifa
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Gil Cohen-Magen/AP/picture alliance

Soma zaidi: Netanyahu asema Israel itapigana kufa kupona hadi ishinde

Katika hatua nyingine, waziri wa mambo ya nje wa Ireland Michael Martin amesema kuwa, Ireland inafikiria kuitambua Palestina kuwa ni taifa huru mwishoni mwa mwezi wa tano. Martins ameeleza kuwa, bado haijulikani tarehe hasa ya kufanya hivyo kwa kuwa majadiliano na mataifa mengine yanaendelea ili kufanya utambuzi huo kwa pamoja.

Juhudi za kuitambua Palestina kuwa nchi zinafanyika wakati idadi ya vifo ikiongezeka Gaza kutokana na mashambulizi ya Israeli dhidi ya kundi la Hamas.

 

Related Posts