Say Raymond Mwakatundu (31) mkazi wa jijini Dar es Salaam amekamatwa na Polisi mkoani Njombe akiwa na fedha kiasi cha Milioni 29,374,000 katika nyumba ya kulala wageni (Guest) mjini Makambako fedha ambayo inadaiwa ameipata kwa njia ya wizi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Mahamoud Banga amesema walimkamata Mwakatundu wakiwa wanafanya upekuzi wa kawaida katika nyumba za kulala wageni ambapo baada ya mahojiano alikiri kuipata fedha hiyo kwa njia ya uporaji.
“Tulipofika katika nyumba ya kulala wageni ambayo inaitwa Lisbon ndio tulifanikiwa kumkamata akiwa na fedha hiyo lakini baada ya kumhoji kwa kina alieleza kwamba fedha hizo amezipora katika kampuni aliyokuwa anafanyia kazi ya Interchick Dar es Salaam”amesema Kamanda Banga
Aidha amesema tayari mtuhumiwa amekwishakabidhiwa kwa jeshi la Polisi mkoani Dar Es Salaam kwa ajili ya hatua zingine za kimashtaka ili aweze kufikishwa Mahakamani.